MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imesema inatafuta taarifa kuweza kubaini meli zaidi ya 65 zilizoingia na kushusha mizigo nchini bila kulipa kodi.
Hiyo ni baada ya Rais Dk. John Magufuli, kueleza madudu aliyoyakuta ndani ya Bandari ikiwamo jinsi meli 65 zilivyoingia na kushusha mizigo bila kulipa ushuru wa Serikali.
Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Gladson Urioh, alisema tangu Rais Magufuli alipotoa kauli hiyo hivi karibuni akiwa wilayani Chato, Mamlaka imekuwa ikifuatilia taarifa hizo.
“Hili suala la meli zaidi ya 65 kuingia na kutolipa kodi tunalifuatilia kwa undani sisi TPA pamoja na wadau wote vikiwamo vyombo vya ulinzi.
“Bandari ina wadau wake ambao ni pamoja na vyombo vya ulinzi, Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi kavu (Sumatra), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Idara ya Uhamiaji, Idara ya Afya na Mkemia Mkuu wa Serikali na wengine.
“Tunaamini kwa umoja wetu huu tutapata taarifa kwa undani kuhusu suala hili la meli,” alisema Urioh.
Wiki iliyopita akiwa wilayani Chato, Rais Dk. John Magufuli, alifichua zaidi madudu ndani ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) akieleza jinsi meli 65 zilivyoingia na kushusha mizigo nchini bila kulipa ushuru wa Serikali.
Alisema meli hizo zilishusha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na baada ya kupakua mizigo hiyo ziliondoka bila kujulikana zimekwenda wapi.
“Ndugu zangu tusipochukua hatua nchi itatushinda leo (juzi) pale bandari zimeingia zaidi ya meli 65 zimeshusha mizigo na hazikuonekana, hivi inawezekana vipi meli ishushe mizigo na kutokomea bila kulipa mapato ya Serikali?
“Meli zilileta mizigo zikashusha na zikapotea hivyo hivyo na Serikali ikakosa hela. Jamani ndani ya Serikali kuna madudu ya kila aina hivyo ninawaomba mniombee, nimejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa.
Source: Mtanzania