Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni imemhukumu kifungo cha miaka 7 jela na kuchapwa viboko 12 mkazi wa Manzese, Ally Tox (19) baada ya kupatikana hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hakimu Mkazi, Obadia Bwegoge akitoa hukumu hiyo jana alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka, vielelezo pamoja na utetezi uliotolewa na mshtakiwa mwenyewe atatumikia kifungo hicho jela na kuchapwa viboko 12 katika kosa hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha na kumwibia Asma Hajji.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Nancy Mushumbusi aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo na kwa upande wa mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu hilo ni kosa lake la kwanza.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Tox alikuwa ni tishio mtaani kwa kuwaibia watu na kuwajeruhi hivyo akashtakiwa chini ya kifungu cha 285 na 286 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika kesi hiyo Tox anadaiwa kuwa Septemba 26, 2016 katika eneo la Manzese Madizini alimchoma kisu usoni Asma Hajji na kumuibia simu ya mkononi aina Sumsung.