Asante Kikwete kwa ongezeko la thamani ya uwekezaji nchini

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
Katika mwaka 2013 pekee, thamani ya uwekezaji nchini, total investment, ilikuwa takribani Dola za Kimarekani bilioni 11.37 ikilinganishwa na dola bilioni 8.75 mwaka 2012.

Ongezeko hili linatokana hasa na uwekezaji katika miundombinu ya usafiri, ujenzi, nishati, maji na kilimo. Aidha, uwekezaji wa mitaji ya kigeni na moja kwa moja foreign direct investment ilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 1.88 mwaka 2013, ikilinganishwa na dola bilioni 1.80 mwaka 2012.

Ongezeko hili kwa kiasi kikubwa linatokana na uwekezaji katika sekta ndogo ya gesi.
===============================


12 June 2014: Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2013 na Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015

Mheshimiwa Spika, tunamwomba mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Vile vile natoa salamu za pole kwa Wabunge na wananchi wote waliopatwa na maafa mbalimbali nchini katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, hotuba ninayoiwasilisha imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Kwanza ni maelezo mafupi kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2013. Pili ni muhtasari wa mapitio ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa taifa 2013/2014 na sehemu ya tatu ni mpango wa maendeleo wa taifa 2014/2015 unaobainisha miradi iliyopo chini ya mfumo wa matokeo makubwa sasa, miradi ya kitaifa ya kimkakati na miradi mingine ambayo Serikali inatarajia kutekeleza mwaka 2014/2015, gharama za utekelezaji wa mpango na mfumo wa uratibu ufuatiliaji na tathmini.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kueleza Hali ya Uchumi wa taifa kwa mwaka 2013 na mpango wa maendeleo wa taifa 2014/2015 naomba kuainisha kwa muhtasari maeneo muhimu ambayo Kamati ya Bunge ya Bajeti ilishauri kuzingatiwa katika mpango. Maeneo hayo ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika kilimo, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji na umeme vijijini, kuanza ujenzi wa reli mpya kwa kiwango cha kimataifa na ukarabati reli iliyopo, kuboresha huduma za bandari, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha uvuvi wa bahari kuu.

Aidha kamati ilishauri tume kufanya mapitio ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2011/2012 hadi 2015/2016 kwa kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji. Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa maeneo haya yote yamezingatiwa kikamilifu katika mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2014/2015 kama Kamati ilivyoshauri.

Vile vile Ofisi ya Rais Tume ya Mipango imeanza kufanya mapitio ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano yaani 2011/2012 hadi 2015/2016.

Mheshimiwa Spika, tangu kutokea kwa msukosuko mkubwa wa fedha na uchumi duniani mwaka 2008 ukuaji wa uchumi wa dunia umekuwa chini ya kiwango kilichokuwa kimefikiwa awali. Mwaka 2013 kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia iliendelea kupungua na kuwa asilimia tatu ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.3 mwaka 2012.

Miongoni mwa mambo yanayoendelea kuchangia kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia ni pamoja na wasiwasi uliotokana na baadhi ya nchi za jumuiya ya Ulaya kushoindwa kulipa madeni yao na utekelezaji wa sera za kubana matumizi ya Serikali hizo pamoja na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea.

Mheshimiwa Spika, kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi zilizoendelea ilipungua kutoka asilimia 1.4 mwaka 2012 hadi asilimia 1.3 mwaka 2013.

Kwa upande wa nchi zinazoendelea kasi ya ukuaji wa uchumi pia ilipungua kutoka asilimia 5 mwaka 2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2013. Kupungua kwa ukuaji huu wa uchumi kwa nchi zinazoendelea ulichangiwa na kupungua kwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi hususan huko Urusi, Amerika ya Kusini na Caribbean.

Aidha kasi ya ukuaji wa uchumi kwa nchi za Asia zinazoendelea hususan China na India ilipungua na kuwa asilimia 6.7 mwaka 2013 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.7 mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha muongo mmoja takribani theluthi mbili za nchi za Kiafrika zimekuwa na ukuaji mzuri wa uchumi kutokana na ukuaji huo fursa na kiwango cha elimu kimeongezeka, vifo vya watoto wachanga vimepungua na Bara la Afrika linaendelea kuvutia wawekezaji katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi.

Mwaka 2013 ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara ulikuwa asilimia 4.9 kama ilivyokuwa mwaka uliotangulia 2012. Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na uwekezaji hususan katika uchimbaji wa madini, miundombinu ya usafiri na mawasiliano, kilimo, uzalishaji na nishati na upanuzi wa shughuli za biashara.

Mheshimiwa Spika, uchumi wa Bara la Afrika katika mwaka 2013 ulizidi kuimarika na kuongezeka uwezo wake wa kuhimili misukosuko ya kiuchumi na kukabili changamoto zinazojitokeza.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi na maendeleo Duniani na pia sekta binafsi wanakiri kwamba, Afrika hivi sasa inainukia, (Africa is rising). Takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 Duniani, ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa, 20 fastest growing economies in the world. Wastani wa ukuaji wa Uchumi wa Tanzania kati ya mwaka 2005 mpaka 2013 ni asilimia 6.9. Nchini nyingine za Kiafrika katika orodha hii na wastani wa ukuaji wake kwa kipindi hicho ni Ethiopia asilimia 10.8, Angola asilimia 10.8, Sierra Leone asilimia 8.2, Rwanda asilimia 8.2, Ghana asilimia 7.4, Msumbiji asilimia 7.3, Uganda asilimia 6.7, Zambia asilimia 6.4 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo asilimia 6.4.

Ukuaji wa uchumi wa Nchi Wanachama wa Jamuiya ya Afrika Mashariki kati ya 2012 na 2013, unaonesha kuimarika kwa nchi zote wanachama isipokuwa Rwanda. Uchumi wa Kenya, uliongezeka kutoka asilimia 4.6 mwaka 2012 hadi asilimia 5.6 mwaka 2013, Uganda asilimia 2.8 hadi 6.0, Burundi asilimia 4.0 hadi asilimia 4.5 na Tanzania asilimia 6.9 hadi asilimia 7.0 katika kipindi hicho. Kasi ya ukuaji wa uchumi kwa nchi ya Rwanda imepungua kutoka asilimia 8.0 mwaka 2012 hadi asilimia 5.0 mwaka 2013. Kuimarika kwa uchumi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni matokeo ya utekelezaji wa sera madhubuti za usimamizi wa uchumi na mifumo taasisi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013, Pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0, ikilinganishwa na kukuaji wa asilimia 6.9 mwaka 2012. Shughuli ndogo ambazo zilikua kwa kasi kubwa katika mwaka 2013 ni mawasiliano asilimia 22.8, fedha asilimia 12.2, ujenzi asilimia 8.6; Biashara ya jumla na reja reja asilimia 8.3 na hoteli na migahawa asilimia 6.9. Licha ya viwango vikubwa vya ukuaji, shughuli ndogo za mawasiliano na fedha kila moja ilichangia chini ya asilimia 2.5 ya Pato la Taifa. Kwa upande mwingine, kasi ya ukuaji wa shughuli za kilimo ilibakia asilimia 4.3 kama ilivyokuwa mwaka 2012, hasa kutokana kupungua kwa ukuaji wa shughuli ndogo za mazao ambapo ilipungua kutoka asilimia 4.7 mwaka 2012 hadi asilimia 4.5 mwaka 2013. Hata hivyo, katika eneo hili la kilimo, kasi ya ukuaji wa shughuli ndogo za mifugo na uwindaji iliongoezeka kutoka asilimia 3.1 hadi asilimia 3.8 na misitu kutoka asilimia 2.4 hadi 3.3 katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, kasi ya ukuaji katika baadhi ya shughuli ndogo ilipungua katika mwaka 2013, ikilinganisha na mwaka 2012. Maeneo husika yanayojumuisha bidhaa za viwandani yalipungua kutoka asilimia 8.2 hadi 7.7 kutokana na kupungua kwa uzalishaji katika baadhi ya viwanda; umeme na gesi asilimia 6 ilikwenda mpaka asilimia 4.4 kutokana na uchakavu wa mitambo ya kufua umeme wa maji; uchukuzi asilimia 7.1 hadi 6.2 kutokana na kupungua kwa usafirishaji wa shehena za mizigo katika njia ya anga; na uvuvi asilimia 2.9 hadi 2.2 kwa sababu ya kupungua kwa uzalishaji wa samaki, kutokana na uharibifu wa mazingira ya mazalia ya samaki.

Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa, mwaka 2013 lilikuwa shilingi trilioni 53.17, sawa na Dola za Kimarekani bilioni 33.26 ikilinganishwa na shilingi trilioni 44.72 mwaka uliotangulia 2012, sawa na Dola za Kimarekani bilioni 25.24. Hivyo, wastani wa pato la mwananchi kwa mwaka 2013 lilikuwa shilingi 1,186,200, sawa na Dola za Kimarekani 742, ikilinganisha na shilingi 1,025,038, sawa na dola 652.1 mwaka 2012, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.7.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013, thamani ya uwekezaji nchini, total investment, ilikuwa takribani Dola za Kimarekani bilioni 11.37 ikilinganishwa na dola bilioni 8.75 mwaka 2012. Ongezeko hili linatokana hasa na uwekezaji katika miundombinu ya usafiri, ujenzi, nishati, maji na kilimo. Aidha, uwekezaji wa mitaji ya kigeni na moja kwa moja foreign direct investment ilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 1.88 mwaka 2013, ikilinganishwa na dola bilioni 1.80 mwaka 2012. Ongezeko hili kwa kiasi kikubwa linatokana na uwekezaji katika sekta ndogo ya gesi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na uchumi kukua, umaskini haujapungua kwa kiwango cha kuridhisha. Kwa kiasi kikubwa hali hii inatokana na tija ndogo katika sekta mama ya kilimo, ambayo inaajiri Wananchi wengi. Kilimo kimeendelea kuendeshwa katika mfumo usio rasmihususan kwa kujikimu pamoja na kutumia zana, mbinu na teknolojia duni na hivyo kuchelewesha Mapinduzi ya Kijani. Vilevile sekta hii imeendelea kuvutia kiasi kidogo cha mitaji na mikopo kutoka katika mabenki.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya 2011/2013, yaani household budget survey, kwa Tanzania Bara yaliyoonesha kuwa idadi ya Watanzania wanaoishi chini ya kiwango cha mahitaji ya msingi, yaani basic needs poverty line, ilipungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2011/2012. Katika Jiji la Dar es Salaam idadi ya kaya maskini ilipungua kutoka asilimia 14.1 mwaka 2007 hadi asilimia 4.1 mwaka 2011/2012. Kwa maeneo mengine ya mijini kiwango hicho kilipungua kutoka asilimia 22.7 hadi asilimia 21.7 katika kipindi hicho. Aidha, matokeo yanaonesha kuwa, asilimia 9.7 ya watu wote waishio Tanzania Bara, wapo chini ya mstari wa umaskini wa chakula, yaani food poverty line, ikilinganishwa na asilimia 16.6 kwa kigezo hicho mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, utafiti huo pia umeonesha kuwepo na mafanikio katika maendeleo ya makazi na umiliki wa rasilimali. Hivi sasa takribani asilimia 73 ya kaya zinaishi katika nyumba zilizojengwa kwa matofali ya saruji au kuchomwa au mawe ikilinganishwa na asilimia 33 mwaka 2007. Aidha, asilimia 66 ya Watanzania wanaishi kwenye nyumba zinazoezekwa kwa bati ikilinganishwa na asilimia 55 na mwaka 2007. Vilevile utafiti unaonesha kuwa idadi za kaya zinazomiliki vyombo vya usafiri na mawasiliano iliongezeka kati ya mwaka 2007 na 2012. Kwa mfano, idadi ya kaya zinazomiliki pikipiki imeongezeka kutoka asilimia 1.5 mwaka 2007 hadi asilimia 4 mwaka 2011/2014 na takribani asilimia 57 ya kaya zina mtu mmoja anayemiliki simu ya mkononi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mafanikio katika kudhibiti mfumuko wa bei. Mfumuko wa bei kwa mwaka 2013 ulipungua kufikia wastani wa asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 16 mwaka 2012. Hali hiyo ilichangiwa na kushuka kwa bei za chakula hususan mchele na aina nyingine za nafaka, kufuatia kuimarika kwa upatikanaji na usambazaji wa chakula katika masoko. Mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Aprili, 2014 ulifikia wastani wa asilimia 6.3. Kwa upande wa nchi nyingine za Afrika Mashariki mfumuko wa bei kwa mwezi Aprili nchini Burundi ulikuwa asilimia 3.8, Kenya asilimia 6.4, Rwanda asilimia 2.8, na Uganda asilimia 6.7.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013, Serikali inaendelea na sera ya kudhibiti ujazi wa fedha ili uende sambamba na ukuaji wa uchumi. Ujazi wa fedha kwa tafasiri pana zaidi, yaani M3, ulikuwa shilingi bilioni 16,106.8 ikilinganishwa na shilingi bilioni 14,647.1 mwaka 2012, sawa na aongezeko la asilimia 10.0. Hata hivyo, ukuaji huu ulikuwa chini ya lengo lililowekwa kwa mwaka 2013 la asilimia 15. Hii ilitokana na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa rasilimali halisi za ndani katika benki, net domestic assets, ikiwa imeongezeka kwa asilimia 15.8 mwaka 2013 ikilinganisha na asilimia 22.3 mwaka 2012. Aidha, katika kipindi hicho kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi nayo ilipungua na kuwa asilimia 15.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 18.2 mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2013, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana, M2, uliongezeka na kufikia shilingi bilioni 11,890.6 kutoka shilingi bilioni 10,724.5 mwaka 2012, sawa na ongezeko la asilimia 10.9. Aidha, mikopo nchini iliongezeka kwa asilimia 18.8 kutoka shilingi bilioni 13,719.4 mwaka 2012 hadi shilingi bilioni 16 mwaka 2013. Kati ya hizo, shilingi bilioni 5,900.4 zilikuwa mikopo kwa Serikali Kuu na shilingi bilioni 10,386.9 zilikuwa mikopo kwa sekta binafsi. Udhibiti wa ujazi wa fedha ni nyenzo ya Serikali kudhibiti mfumuko wa bei hususan usiokuwa wa chakula. Aidha, kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi ni kielelezo cha kuongezeka kwa uwezekaji, ajira na kuimarika kwa kipato cha mwananchi.

Mheshimiwa Spika, viwango vya riba; mwenendo wa riba za amana mbalimbali na za mikopo kwa mwaka 2013 uliimarika ikilinganishwa na mwaka 2012. Kiwango cha riba ya mikopo kwa mwaka mmoja kilipungua kutoka wastani wa asilimia 14.09 Desemba, 2012 hadi asilimia 13.78 Desemba, 2013. Riba za amana za mwaka mmoja ziliongezeka kufikia wastani wa asilimia 11.12 Desemba, 2013 kutoka asilimia 11.06 mwaka 2012. Kutokana na mwenendo huo, tofauti kati ya riba za amana na mikopo ya mwaka mmoja ilipungua kutoka wastani wa asilimia 3.03 Desemba, 2013 kufikia asilimia 2.66 Desemba, 2013. Kupungua riba kwa mikopo na kuongezeka kwa riba za amana za mwaka mmoja ni dhahiri kuwa Wananchi wengi wameanza kunufaika na mikopo kwa ajili ya kuendeshea shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, riba zinazotozwa katika soko la fedha za kigeni baina ya mabenki, yaani interbank foreign exchange market ziliongezeka kufikia wastani wa asilimia 8.58 Desemba, 2013 ikilinganisha na asilimia 5.8 Desemba, 2012 kutokana na kupungua kwa ukwasi wa mabenki. Aidha, riba kwa dhamana za Serikali ziliongezeka kufikia wastani wa asilimia 16.20 mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 12.8 mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzani dhidi ya Dola za Marekani ilishuka kwa wastani 1.7 mwaka 2013, ikilinganishwa na asilimia 0.9 mwaka 2012. Dola ya Kimarekani ilinunuliwa kwa wastani wa shilingi za Tanzania 1,598 mwaka 2013 ikilinganishwa na shilingi 1571.70 mwaka 2012. Vilevile Dola ya Marekani iliuzwa kwa shilingi 1,578.57 Desemba, 2013 ikilinganishwa na shilingi 1,571.62 Desemba 2012. Kushuka kwa thamani ya shilingi kunatokana na kuongezeka mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya uagizaji wa bidhaa mbalimbali kutoka nje, ambayo yalikuwa zaidi ya mauzo ya bidhaa za Tanzania. Aidha, thamani ya Shilingi ya Tanzania iliendelea kushuka ambapo kufikia Aprili, 2014 Dola ya Marekani ilinunuliwa kwa wastani wa shilingi 1,637.38.

Mheshimiwa Spika, sekta ya nje; katika mwaka 2013, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ilipungua kwa asilimia 1.7 kutoka Dola za Kimarekani milioni 8,675.6 mwaka 2012 hadi dola milioni 8,532. Upungufu huu ulichangiwa zaidi na kushuka kwa mauzo ya dhahabu na bidhaa nyingine asilia ikiwa ni pamoja na tumbaku, kahawa, pamba, katani, kushuka kwa bei za uzalishaji wa baadhi ya mazao katika Soko la Dunia. Aidha, thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje iliongezeka kwa asilimia 6.6 kutoka Dola za Kimarekani milioni 13,517.6 kutoka Dola milioni 12,678 mwaka uliotangulia. Ongezeko hili lilitokana na uagizaji wa mafuta ambapo kiwango cha uagizaji kiliongezeka kwa asilimia 27.4.

Mheshimiwa Sika, maeneo ambayo Tanzania ilifanya vizuri katika biashara ya nje kwa mwaka 2013 ni yafuatayo; huduma za utalii ambayo mapato yake yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani bilioni 1.37 mwaka 2012 hadi dola bilioni 1.81 mwaka 2013; huduma za usafirishaji bidhaa kupitia Tanzania kwenda nchi jirani, yaani transit trade, ambapo mapato yake yalikadiriwa kuongezeka kutoka dola milioni 497.3 mwaka 2012 hadi dola milioni 576.8, mwaka 2013. Aidha, mizigo iliyopitishwa nchini kwenda nchi jirani iliongezeka kutoka tani 1,175,484 hadi tani 1,386,705 katika kipindi hicho. Thamani ya mauzo ya bidhaa za viwandani pia iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,037.3 mwaka 2012 hadi dola milioni 1,072.1 mwaka 2013. Serikali inaipongeza sana juhudi za Wananchi na wadau waliochangia ongezeko hili katika sekta nilizozitaja.

Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuimraika. Katika kipindi kinachoishia Desemba, 2013, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Kimarekani milioni 4,676.2 ikilinganishwa na dola milioni 4,069.1 mwaka 2012. Kiasi hiki cha akiba ya fedha za kigeni kinatosheleza uagizaji bidhaa kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.5 ikilinganisha na miezi 3.9 mwaka 2012. Aidha, akiba ya fedha za kigeni katika benki za biashara ilipungua kwa asilimia 2.2 kufikia Dola za Marekani milioni 876.3 kutoka dola milioni 887 mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, mapato na matumizi ya Serikali: Mapato ya ndani kwa mwaka 2012, yalikuwa ni shilingi bilioni 8,586, sawa na asilimia 17.6 ya Pato la Taifa. Aidha, matumizi yalikuwa shilingi bilioni 12,817 sawa na asilimia 26.3 ya pato la Taifa. Hivyo, nakisi ya bajeti, ikijumuisha na misaada ilikuwa asilimia 6.5 ya Pato la Taifa katika mwaka 2012/2013. Mwaka 2013/2014 Serikali ilikadiria kukusanya mapato ya ndani jumla ya shilingi bilioni 11,174.07, sawa na asilimia 18.3 ya Pato la Taifa. Matumizi yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 18,248.9 sawa na asilimia 27 ya Pato la Taifa. Kufuatia hali hii, nakisi ya bajeti, ikijumulisha misaada, inakadiriwa kuwa asilimia 5.5 ya Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, hadi Desemba, 2013, Deni la Taifa lilifikia Dola za Marekani bilioni 17.10, sawa na shilingi trilioni 27.04 ikilinganishwa na shilingi trilioni 22 katika kipindi kama hicho mwaka 2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.1. Ongezeko hilo lilitokana na mikopo mipya hasa ya masharti nafuu na ya kibiashara pamoja na kukua kwa malimbikizo ya riba kwa madeni ya nje hususan kwa nchi ziziso wanachama wa kundi la Paris, ambazo hazitoi misamaha. Mikopo hii ilitumika katika kugharimia miradi mbalimbali kuhusu maendeleo ya Taifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, ujenzi na ukarabati wa barabara, ujenzi wa miundombinu ya umeme na ujenzi wa miundombinu ya maji kwa Miradi ya Ruvu Juu na Chini. Pamoja na ongezeko hilo, Deni la Taifa linahimilika.

Mheshimiwa Spika, katika Kikao cha 15 cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kilichofanyika Uganda Novemba, 2013, pamoja na mambo mengine Itifaki ya kuanzisha sarafu moja kwa nchi za Afrika Mashariki ilisainiwa. Masuala ya msingi yanayotakiwa kutekelezwa ni kuwa na sarafu moja, ni kufikia vigezo vya muunganiko wa uchumi mpana, Micro Economic Convergence Criteria na kuanzisha Taasisi muhimu ya kusimamia utekelezaji wa sarafu moja kwa nchi husika, ambazo ni Taasisi za Fedha za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Takwimu ya Afrika Mashariki na Kamisheni ya Huduma ya Fedha ya Afrika Mashariki ili kufikia hatua hiyo Nchi Wanachama wanatakiwa kukamilisha hatua za awali za mtengamano za umoja wa forodha na soko la pamoja ikijumuisha kurekebisha sheria na kuweka mfumo wa pamoja wa kielektroniki wa kufuatilia usafirishaji wa mizigo ndani ya Nchi Wanachama.

Mheshimiwa Spika, pamekuwa na hatua za kuridhisha katika utekelezaji wa Miradi na Programu za pamoja za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika uendelezaji wa barabara na reli zinazounganisha Tanzania na Nchi Wanachama, usanifu wa kina wa barabara za Arusha, Holili - Taveta, Voi ulikamilika na mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulitiwa sahihi kati ya Benki ya Maendeleo ya Afrika na nchi za Kenya na Tanzania. Aidha, katika kutekeleza mpango kambambe wa kuendeleza reli ya Dar es Salaam, Isaka, Kigali/Keza, Gitegi, Musongati inayojumuisha nchi za Burundi, Rwanda na Tanzania, upembuzi wa kina umekamilika.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada za utekelezaji wa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI nchini, mwaka 2013 Serikali ilianzisha mpango unaoitwa Option B plus, unaolenga kuwapatia wajawazito wenye maambukizi ya VVU, dawa ya kupunguza makali ya VVU kwa wakati. Hii ni katika kuetekeleza mpango wa kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Aidha, mafunzo na warsha zilizotolewa kwa watoa huduma na viongozi wa ngazi ya Mikoa na Wilaya kwa lengo la kuwawezesha kuandaa mpango endelevu wa kutokomeza maambukizi mapya ya VVU.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2013 Serikali iliendelea kutekeleza Sera ya Mazingira ya Mwaka, 1977 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 ili kuleta maendeleo endelevu. Katika kipindi hiki miongozo mitatu kwa ajili ya kutekeleza Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 iliandaliwa na hivyo kufanya Sheria iwe na miongozo saba kati ya 19 inayohitajika kulinganisha na miongozo minne iliyoandaliwa mwaka 2012. Miongozo hiyo ni mwongozo wa kuandaa tathmini ya kimkakati ya mazingira, mwongozo wa kuhusisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika Sera na Mipango na muongozo wa maandalizi ya mipango ya mizingira ya kisekta na Serikali za Mitaa. Hii ni rai ya Serikali kuwa, miongozo hii itumike ipasavyo ili isaidie katika jitihada za kunusuru nchi yetu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali iliendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mkakati huo unatoa mwongozo wa hatua ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, zinazotakiwa kuchukuliwa na sekta mbalimbali na kutoa mwongozo wa kuziwezesha sekta kuandaa mpango wake kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Sekta za mtaji za maji na kilimo zimeanza utekelezaji wa mkakati huu kwa kuandaa mipango yake ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Spika, upangaji na uendelezaji wa miji na vijiji. Katika mwaka 2013 Serikali iliendelea kuandaa mpango wa kusimamia uendelezaji na udhibiti wa ukuaji wa miji nchini. Mipango hiyo ya aina mbili, mipango kabambe ambayo hutoa mwongozo na uendelezaji miji kwa muda mrefu wa miaka 20 na mipango ya muda wa kati na matumizi ya ardhi ambayo hutoa mwongozo kwa uendelezaji wa miji kwa muda wa miaka kumi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam ziliendelea kuandaa Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam, ambapo rasimu ya mwisho iliwasilishwa kwa wadau na mtaalam mwelekezi anayeendeleza kuboresha kwa kutumia maoni na mapendekezo yanayotolewa na wadau. Aidha, Halmashauri ya Mji Mdogo wa Bagamoyo ilikamilisha maandalizi ya rasimu ya awali ya Mpango Kabambe ya Mji huo. Pia, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, ilikamilisha maandalizi ya rasimu ya mpango wa muda wa kati na matumizi ya ardhi kwa Mji wa Kilindoni. Vilevile Serikali inaendelea kushirikiana na Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga na Mji wa Bariadi kuandaa mpango kabambe wa miji hiyo.

Mheshimiwa Spika, hali ya usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali hapa nchini imeendelea kuimarika. Kwa upande wa ushiriki wa wanawake katika ngazi za siasa na maamuzi, idadi ya Mawaziri Wanawake imeongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2005 hadi asilimia 30 mwaka 2013. Wakuu wa Mikoa Wanawake kutoka asilimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 24 mwaka 2013. Majaji Wanawake pia wameongezeka kutoka asilimia 33 hadi asilimia 61 kwa kipindi hicho. Uwakilishi wa Wanawake Bungeni umeongezeka kutoka asilimia 30.3 mwaka 2005 na kufikia asilimia 36 ya Wabunge wote mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi, mwaka 2013/2014, Serikali ilitenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Katika kipindi hicho, Julai mpaka Desemba, Mfuko huo ulikuwa umepatiwa shilingi 515,000,000. Aidha, taasisi za kifedha zimeendelea kutoa mikopo ya fedha na mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake. Baadhi ya Taasisi hizo ni Benki ya Wanawake Tanzania, Women Covenant Bank, SACCOS na VICOBA.

Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa MKUKUTA na Malengo ya Milenia. Utekelezaji wa MKUKUTA umekuwa na mafaniko ya kuridhisha licha ya changamoto mbalimbali. Katika kupunguza umaskini wa kipato, Serikali iliendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuongeza fursa za ajira nchini na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kuwawezesha kujiajiri wenyewe. Kutokana na hatua hizo, jumla ya nafasi za ajira 274,030 zilipatikana mwaka 2012/2013, ikilinganisha na ajira 250,000 mwaka 2011/2012. Aidha, Serikali ilibaini na kuhakiki vikundi 502 vikiwa na jumla ya wanachama 5,385; wanawake 2,519 na wanaume 2,866, katika Mikoa 17 kwa ajili ya kuviendeleza na kuvipatia mitaji na mfunzo ya ujasiriamali.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, utafiti wa mapato na matumizi ya kaya, Household Budget Survey, uliofanyika mwaka 2011/2012, umeonesha kuwa idadi ya kaya maskini zilizo chini ya kiwango cha mahitaji, yaani basic needs poverty, kimepungua kwa asilimia 6.2 kati ya mwaka 2007 na 2012. Utafiti huo pia umeonesha mafanikio katika upatikanaji wa huduma za Afya, Elimu na Maji. Kwa upande wa Afya, Tanzania imefanikiwa kufikia Lengo la Milenia Namba Nne ikiwa imepunguza vifo vya watoto wachanga toka 191 mwaka 2000 mpaka vifo 51 kati ya watoto 1000 mwaka 2013. Aidha, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vilipungua kutoka 115 mwaka 2000 hadi vifo 54 kati ya watoto 1000 mwaka 2013.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa jitihada zake za kipekee katika eneo hili hapa nchini na nje ya nchi. Katika hili ameonesha ukereketwa na utumishi uliotukuka, ambapo yeye pamoja na Mwenyekiti mweza Mheshimwia Stephen Harper, Waziri Mkuu wa Canada, imebidi wapewe pongezi za kipekee na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki-Moon, kwa ufanisi mkubwa waliouonesha tangu walipoteuliwa kuongoza Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala la afya ya mama na mtoto Duniani. Pongezi hizo zilitolewa tarehe 29 Mei, 2014 huko
Toronto Canada. Hii ni heshima kubwa kwake na kwa Taifa ketu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, utafiti kuhusu Malaria na Ukimwi (HIV and Malaria Indicator Survey) wa mwaka 2012, umeonesha kuwa kasi ya maambukizi ya malaria ilipungua kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 9 mwaka 2011/2012. Maambukizi ya UKIMWI katika kundi la watu wenye umri kati ya miaka 15 na 49 kutoka asilimia 7.7 mwaka 2007 na 2008 hadi asilimia 5 mwaka 2011/12. Haya ni mafanikio ya kutia moyo. Hata hivyo, naomba nisisitize kwa Watanzania wote kuwa, janga hili la Ukimwi na Ugonjwa wa Malaria bado ni changamoto kubwa. Hivyo, tunapaswa kuongeza jitihada zaidi ili hatimaye tuweze kufikia azma yetu kuwa, Tanzania bila UKIMWI na Malaria inawezekana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Sekta ya Elimu na Maji ni sehemu ya maeneo yaliyo chini ya Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa; mafanikio yaliyopatikana katika sekta hizo yameelezwa katika sehemu ya utekelezaji wa Miradi hiyo ya BRN. Mheshimiwa Spika, sasa nijikite katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo 2013/2014.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mawaziri wa Sekta wameshaeleza kwa kina utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa sekta zao kwa kipindi cha Julai, 2013 hadi Machi, 2014, naomba nieleze kwa kifupi sana, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2013/2014. Maelezo yangu yatajikita katika maeneo ya kimkakati ambayo Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulipanga kuyatekeleza. Kwa ujumla katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/2014 umekuwa na mfanikio ya kuridhisha.

Mheshimiwa Spika, Miradi chini ya Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Napenda kulikumbusha Bunge lako Tukufu kuwa, mwaka 2013/2014 Serikali ilianza kutekeleza baadhi ya miradi kwa kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Matokeo Makubwa Sasa. Katika mwaka 2013/2014 Ofisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Miradi (President's Delivery Bureau - PDB), ilifuatilia miradi iliyoaainishwa kupitia awamu ya kwanza ya uchambuzi wa kimaabara katika Sekta ya Kilimo, Elimu, Nishati, Maji, Uchukuzi na Ukusanyaji wa Mapato.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Kilimo, baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa chini ya MNS ni pamoja na kutoa mafunzo ya kuendesha scheme za umwagiliaji kwa Maafisa Ugani 95 na Wakulima 95. Kupata hati miliki kwa mashamba makubwa mawili ya Bagamoyo na Mkulazi, Rufiji na Hati ya Kimila kwa Mashamba madogo 185 na kutoa mafunzo kuhusu biashara, kilimo bora na kuunda vyama vya wakulima katika Miradi ya Bagamoyo, Lukulilo na Ngalimila na maghala 50 yameendelea kufanyiwa tathmini kwa ajili ya ukarabati. Pamoja na mafanikio haya, ipo Miradi mingi ya Sekta ya Kilimo inayotekelezwa kama nitakavyoeleza katika eneo la Miradi ya Kitaifa ya Kimkakati.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Elimu, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa uandikishaji katika ngazi zote za elimu, kuongezeka kwa ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne kutoka asilimia 43.08 mwaka 72 hadi 58.25 mwaka 2013. Katika ngazi ya Elimu ya Msingi kutoka asilimia 31 mwaka 2013 hadi asilimia 50.3 mwaka 2015. Kiwango cha kihitumu elemu ya msingi kiliongezeka kutoka asilimia 54.8 mwaka 2012 hadi asilimia 55.3 mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine katika Sekta ya Elimu ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika shule 56 kati ya 264 za awamu ya kwanza na kutoa tuzo kwa shule 3,000 zilizofanya vizuri na zile zinazoonesha kupiga hatua kulingana na ufaulu katika mwaka 2012/2013. Kuongeza maabara katika shule za kata ili kuimarisha elimu ya sayansi na ufundi. Kuanza ukarabati wa shule kongwe za kitaifa na kufanyika kwa upimaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la pili katika sampuli ya shule 200 na kuandaa mwongozo wa kufundisha KKK. Pamoja na mafanikio hayo, napenda nikiri kuwa changamoto katika eneo hili bado zipo na ni kubwa. Kwa hiyo, ni dhahiri tunahitaji kuimarisha upatikanaji wa elimu bora katika ngazi zote. Uwezo wa Tanzania ya kesho katika ulimwengu wenye ushindani mkali kiuchumi, unategemea upatikanaji wa elimu bora, ujuzi, ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika nyanja zote.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Nishati, baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni kuunganishwa umeme wateja wapya 138,931 dhidi ya lengo la kuunganisha wateja 150,000 kwa mwaka 2013/2014 na kupunguza upotevu wa umeme kutoka asilimia 21 mwaka 2012 hadi asilimia 19 mwaka 2013.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilometa 542 na kipenyo cha nchi 36 kutoka Mradi wa Mnazi Bay -Mtwara na Songosongo - Lindi hadi Dar es Salaam uliendelea kutekelezwa. Kazi zilizofanyika hadi Aprili, 2014 ni pamoja na kuwasili na kupokelewa kwa mabomba yote ya gesi, kuunganisha mabomba yenye urefu wa kilometa 362 sawa na asilimia 70, kufukia bomba la gesi kwa umbali wa kilometa 182 sawa na asilimia 34 na kujenga bomba la gesi chini ya Bahari kwa kilometa 25.6.
Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Uchukuzi, mafanikio ni pamoja na kuanzishwa kwa mradi wa kielektroniki wa kufuatilia usafirishaji wa mizigo, ambapo magari yenye kifaa hiki hayana haja ya kusimama katika baadhi ya vituo vya ukaguzi na hivyo kuokoa muda wao barabarani na kuongezeka kwa ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuhudumia zaidi ya tani milioni 13, Desemba, 2013 ikilinganisha na tani milioni 12 mwezi Desemba, 2012. Vilevile katika Reli ya Kati, Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja matatu yaliyopo kilometa 293, kilometa 303 na kilometa 517 kutoka Dar es Salaam. Uundwaji upya wa vichwa vitatu vya treni katika karakana ya Morogoro na uundwaji wa vichwa vingine vitano upo katika hatua mbalimbali. Aidha, malipo ya vichwa vipya 13, mabehewa ya abiria 22 na mabehewa ya breki 34 na mabahewa ya kokoto 25 yamekamilika na malipo ya mabehewa 274 ya mizigoyamefanyika kwa asilimia 50.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi zilizofanyika za kurejesha ufanisi wa mtandao wa Reli, kumekuwa na matukio ya hujuma ikiwa ni pamoja na kung'oa mataluma ya njia za Reli. Matukio haya yanaturudisha nyuma. Naomba nitumie fursa hii kuwaonya na kuwataka wanaofanya hujuma hii kuacha mara moja na pia kuwaomba Wananchi kutimiza wajibu wao wa kulinda miundombinu ambayo inatutumikia sisi wote.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Maji, mafanikio yaliyopatikana ni kukamilika kwa ujenzi wa Miradi ya Maji 228 katika vijiji 243 na Halmashauri 98 na hivyo kutuwezesha jumla ya vituo vya kuchotea maji 10,560 kujengwa na kuundwa kwa Jumuiya za Watumiaji Maji 373 hadi Machi, 2014. Matokeo yake ni kuwa, Wananchi 2,640,000 waishio vijijini, wamepatiwa maji safi katika kipindi cha miezi sita, ikilinganishwa na idadi kati ya Wananchi 300,000 na 500,000 waliokuwa wanaweza kuunganishiwa huduma ya maji safi na salama kwa mwaka hapo awali. Matokeo haya yamechangiwa na kupunguza muda wa mchakato wa ununuzi wa umma, kutoka siku 265 hadi siku 90. Aidha, Miradi 538 ya miundombinu ya maji vijijini itakayohusisha vituo 9,630 vya kuchotea maji katika vijiji 587 yenye uwezo wa kuhudumia wanavijiji milioni mbili na arobaini elfu inaendelea kujengwa. Sambamba na hilo, mikataba ya Miradi 707 inayohusisha vituo 13,050 katika vijiji 725 yenye uwezo wa kuhudumia wanavijiji 3,262,000 imesainiwa. Naomba nitumie fursa hii kuwajulisha Wananchi kuwa ili Serikali itimize wajibu wake vizuri wa kuwafikishia Wananchi maji baada ya miradi hii kukamilika, ni wajibu wa msingi kwa kila Mwananchi kuhakikisha hifadhi endelevu ya vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, hadi Aprili, 2014 ukusanyaji wa mapato yaliyotokana na vyanzo vilivyoibuliwa chini ya Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) ulikuwa umefikia shilingi bilioni 338, sawa na asilimia 29.14 ya lengo la kukusanya shilingi tilioni moja nukta moja sita katika Mwaka wa Fedha 2013/2014. Matokeo yasiyoridhisha yanatokana na baadhi ya mapendekezo ya BRN kutotekelezwa katika mwaka 2013/2014. Mapendekezo hayo ni kubadilisha mfumo wa ushuru wa bidhaa zisizo za petrol kutoka specific kwenda advalorem makisio shilingi bilioni 386, kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia tano kwenye bidhaa zinazotoka nje ya nchi, makisio shilingi bilioni 225.6. Kwa kuwa ukusanyaji mapato ndiyo msingi wa kufanikisha kwa BRN, Serikali inachambua vyanzo mbadala vya kufidia mapato haya ili kuhakikisha lengo kuu la kuongeza mapato kwa shilingi trilioni 3.48 linafanikiwa ifikapo mwaka 2015/2016. Aidha, katika juhudi za kuimarisha makusanyo ya kodi, Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya mashine za EFD ambazo mamlaka inayohusika inaendelea na zoezi la kuwasajili wafanyabiashara wote wanaostahili kuanza kutumia mashine hii.

Mheshimiwa Spika, Miradi ya Kitaifa na Kimkakati. Katika eneo la reli, kazi zilizopangwa kubadilisha reli nyepesi na kuweka nzito ya ratili themanini kwa yadi kwa umbali wa kilometa themanini na tisa kati ya Kitaraka na Malongwe na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi mbalimbali. Kazi zilizotekelezwa hadi Aprili 14 ni pamoja na kutandikwa kwa reli yeynye uzito wa ratili themanini kwa yadi kwa urefu wa kilometa arobaini na saba na kufikisha jumla ya kilometa themanini na tisa zilizopangwa; na upembuzi yakinifu kwa Mradi wa Reli ya Isaka - Mwanza, Tanga - Arusha - Musoma, Mtwara - Mbamba Bay uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na upembuzi wa kina kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Dar es Salaam - Isaka - Kigali - Keza - Msongati umekamilika.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara kazi zilizofanyika ni kukamilisha ujenzi wa kilometa mia sita nukta moja saba za barabara kuu kwa kiwango cha lami, sawa na asilimia 121 ya lengo la kilometa 495 na kukamilisha ukarabati wa kilometa 193.5 za barabara kuu kwa kiwango cha lami, sawa na asilimia 102 ya lengo la kilometa 190. Kukamilisha ujenzi wa kilometa 59.25 za barabara za mkoa kwa kiwango cha lami, sawa na asilimia 90 ya lengo la kilometa 66.1; na kukamilisha ukarabati wa kilometa 424.5; kiwango cha changarawe sawa na asilimia 49 ya lengo la kilometa 867 kwa mwaka. Kwa upande wa madaraja na vivuko kazi zilizofanyika ni kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Malagarasi Kigoma na Nanganga na Nangoo Mtwara na kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Maligusu Mwanza asilimia 90, Mbutu Tabora asilimia 96 na Kigamboni Dar es Salaam asilimia 44.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Bandari kazi zilizopangwa ni kuboresha Gati Namba Moja hadi Saba na kuanza ujenzi wa Gati Namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam. Kukamilisha usanifu wa kina, kuandaa michoro na kuendelea kutafuta wawekezaji kwa Bandari ya Mwambani Tanga na kukamilisha uthamini wa mali na ulipaji fidia kwa Bandari ya Mbegani Bagamoyo. Kazi zilizofanyika ni kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa Gati Namba Moja hadi Saba na kukamilika kwa hydrographic na topographic survey katika Gati Namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam. Hatua iliyofikiwa katika kuendeleza Bandari ya Mwambani Tanga ni kutangazwa kwa zabuni ya kumpata mwekezaji mwenye uwezo wa kuendeleza Bandari hiyo baada ya kupatikana kwa eneo la Mradi, hekta 174, ambapo kati ya hizo hekta 92 zina hati miliki na malipo ya awali ya Shilingi bilioni moja nukta saba yamelipwa kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga ili Wananchi walipwe fidia.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa usafiri wa anga, malengo ya mwaka 2013/2014 yalikuwa ni kukamilisha awamu ya kwanza ya uikarabati wa viwanja vya ndege Kigoma na Tabora na kuanza awamu ya pili; kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Songwe, Mwanza, Bukoba na Mafya; kuanza ujezi wa jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere; na kuanza ujenzi wa viwanja vya Sumbawanga na Sumbawanga, pamoja na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara na Arusha. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ukarabati wa viwanja vya Kigoma na Tabora na kuanza maandalizi ya awamu ya pili kuendelea na ujenzi wa viwanja vya Songwe, Mwanza na Bukoba; kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja cha Mafia; kuanza ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha Julius Nyerere; na kuanza kwa maandalizi ya viwanja vya ndege Sumbawanga na Shinyanga.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la nishati, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuvutia uwekezaji katika sekta ya nishati, hususan nishati mbadala na makaa ya mawe; kufuatia jitihada mahususi za Serikali, ikiwemo punguzo la gharama za kuunganisha umeme, pamoja na uwezeshaji chini ya Mfuko wa Nishati Vijijini (Rural Energy Fund). Hadi mwezi Machi, 2014 kiwango cha uunganishaji wa umeme kimeongezeka na kufikia asilimia 24, ambapo kiwango cha uunganishaji umeme vijijini kimeongezeka kutoka asilimia mbili mwaka 2005 hadi asilimia saba. Lengo la Serikali ni kuwawezesha Watanzania asilimia 30 kuunganisha umeme ifikapo mwaka 2015/2016.

Katika juhudi za Serikali za kuongeza upatikanaji wa umeme, Miradi ya Ufuaji Umeme ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi hiyo ni pamoja na mitambo ya kufua umeme Kinyerezi I megawati 150 na Kinyerezi II megawati 240, itakayotumia gesi asilia. Miradi mingine itatekelezwa kwa njia ya ubia kati ya Serikali na mwekezaji binafsi, ambayo ni Mradi wa Gesi ya Kinyerezi megawati 300 na Kinyerezi IV megawati 500. Miradi ya Upepo (Wind Power) megawati 50 Singida na Mradi wa Makaa ya Mawe ya Kiwira Megawati 200, Ngaka megawati 400 na Mchuchuma megawati 600.

Mheshimiwa Spika, kwa Mradi wa Maji Safi na Maji Taka malengo ya 2013/2014 yalikuwa ni kujenga na kukarabati miundombinu ya maji mijini na vijijini, hususan kuboresha upatikanaji wa maji Jijini Dar es Salaam. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji Ruvu Chini umekamilika, utandazaji wa mabomba kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam uliendelea ambapo kilometa 35.16 zilikamilika kati ya kilometa 55.93 na mradi wote, sawa na asilimia 62.

Kwa upande wa Mradi wa Maji Ruvu Juu kazi zilizofanyika ni kusaini mkataba wa ujenzi na Kampuni ya VA-TECH WABAG ya India na utekelezaji umeanza. Serikali inaendelea kuboresha huduma za maji kwa kukarabati miundombinu ya kugharimia malipo ya umeme kwa ajili ya kuendesha mitambo ya maji katika Miradi ya Maji ya Kitaifa ya Makonde - Mtwara, Wanging'ombe - Njombe, Kahama - Shinyanga, Maswa - Simiyu, Chalinze - Pwani, Mgango Kiabakali - Mara na Handeni Trank Main Tanga.

Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kilimo malengo yalikuwa ni kutenga ardhi kwa kilimo cha miwa, kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika eneo la SAGCOT, kuanzisha kambi ya mafunzo ya kilimo ya vijana, kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini na kukamilisha ujenzi wa Ghala la Songea na kuanza ujenzi wa maghala mawili ya Songea na Mbozi yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5000 za nafaka kila moja. Mafanikio yaliyofikiwa ni pamoja na kuhakiki jumla ya hekta 254,675, ambapo mashamba mawili yenye jumla ya hekta 85,000 yalipata hati miliki. Kukamilisha utayarishaji wa mipango na matumizi bora ya ardhi kwa vijiji katika Wilaya za Kilombero na Rufiji.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Miradi ya Umwagiliaji katika eneo la SAGCOT, kazi ya kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Sonjo na Lupiro Mkoani Morogoro inaendelea na ujenzi wa banio katika Skimu ya Umwagiliaji ya Itete umefikia asilimia 60, na ujenzi wa Ofisi ya Mradi imekamilika. Aidha, ujenzi wa ukarabati wa skimu 14 zenye jumla ya hekta 4,186 umekamilika. Katika ujenzi wa Kambi ya Vijana Mkongo Rufiji, ukarabati wa majengo umekamilika na kambi kuzinduliwa rasmi tarehe 5 Oktoba, 2013, ambapo vijana 50 wanaendelea kupatiwa mafunzo. Kwa upande wa maghala ya kuhifadhi nafaka, ujenzi wa Ghala la Songea umefikia katika hatua ya kuweka paa.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Viwanda, malengo ya mwaka 2014 yalikuwa ni kuendeleza Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZ/SEZ); kuendelea na Miradi ya Makaa ya Mawe na Chuma ya Mchuchuma na Liganga na kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza viuadudu Kibaha; na kukamilisha tafiti za kitaalam kuhusu magadi-soda katika Bonde la Engaruka na Ziwa Natron. Kazi zilizotekelezwa ni kulipa fidia ya Shilingi bilioni ishirini katika eneo la Kurasini kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Biashara na Huduma na hivyo kufanya jumla ya fidia iliyolipwa kufikia Shilingi bilioni arobaini na nne nukta saba; na kulipa fidia ya Shilingi bilioni tatu katika eneo la Bagamoyo na Shilingi bilioni tatu katika eneo la Tanga. Mafanikio mengine ni kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa miundombinu wezeshi katika kiwanda cha kuzalisha viuadudu Kibaha; kuendelea na tafiti za magadi-soda katika Ziwa Natron na kutafiti teknolojia bora ya uchimbaji wa magadi-soda katika Bonde la Engaruka na kuanza ununuzi wa mitambo kwa ajili ya ujenzi wa mgodi wa chuma katika eneo la Liganga.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta binafsi, yamekuwepo mafanikio mengi. Kwa mfano, katika Sekta ya Viwanda kwa mwaka 2013/2014, miradi inayoendelezwa na sekta binafsi ni pamoja na kiwanda cha ngozi cha Meru Tanneries Arusha, Kiwanda cha Nguo cha Dahong Shinyanga, kiwanda cha ngozi huko Shinyanga na kiwanda cha saruji cha Dangote Mtwara. Hatua zilizofikiwa ni kukamilika kwa kiwanda cha ngozi Arusha chenye uwezo wa kusindika vipande 159,000 vya ngozi ya ng'ombe na vipande 468,000 vya ngozi ya mbuzi na kondoo. Kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha ngozi Shinyanga chenye uwezo wa kusindika vipande 936,000 vya ngozi ya ng'ombe na vipande 2,200,000 kwa ngozi ya mbuzi na kondoo na kuajiri watu 500.

Kiwanda kingine kinachoendelea kujengwa ni kiwanda cha nguo Shinyanga ambacho kinatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba, 2014 na kitatumia pamba tani 30,000 kwa mwaka na kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha Saruji cha Dangote Mtwara. Maeneo mengine yenye uwekezaji mkubwa katika sekta binafsi ni pamoja na huduma za jamii hususan elimu na mafunzo ya ufundi na afya, mabenki na huduma za afya, mawasiliano, uchukuzi na usafirishaji, kilimo, nyumba na makazi na nishati.

Naomba kutumia fursa hii kuipongeza kwa dhati sekta binafsi kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu. Serikali kwa upande wake inaahidi kuongeza msukumo zaidi kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara nchini ili kuwezesha sekta binafsi ichangie zaidi ukuaji wa Uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maendeleo ya rasilimali watu, Serikali katika mwaka 2013/2014 ilipanga kuboresha miundombinu ya Vyuo Vikuu na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA). Kazi zilizotekelezwa ni pamoja ukarabati wa Chuo Kikuu Huria katika Mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga, ukarabati wa hosteli na kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa kumbi za mihadhara katika Chuo Kikuu Mzumbe, kukamilika kwa asilimia 65 ya ujenzi wa madarasa na maabara katika Vyuo Vikuu vya Ardhi na Dodoma na kuanza kwa ujenzi wa miundombinu wezeshi. Kupatikana kwa mkandarasi kwa ujenzi wa hospitali katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mlonganzila.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vyuo vya ufundi stadi, kazi zilizofanyika ni kuendelea na ujenzi wa majengo ya utawala na karakana mbili za useremala katika Chuo cha Kihonda Morogoro na kuanza mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika kuweza kupata mkopo wa Dola za Kimarekani milioni ishirini na tatu kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya Mkoa wa Geita, Njombe, Simiyu na Rukwa, ikiwa ni hatua ya kutekeleza azma ya kuwa na Vyuo vya VETA kila Wilaya nchini. Sambamba na hii, Serikali iliongeza fursa ya wanafunzi ambao hawajapata nafasi ya kujiunga na kidato cha sita ili kusaidia kutoa mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo 25 vya maendeleo ya Wananchi. Vyuo hivyo vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi vilipatiwa vifaa vya kujifunzia na kufundishia masomo ya ufundi stadi na kwa mwaka 2013/2014 vilisajili wanafunzi 2,722 na fani mbalimbali za ufundi. Vilevile Serikali iliendelea kukarabati miundombinu katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya Tarime, Kilwa Masoko, Masasi na Chilala. Nitumie nafasi hii kutoa rai kwa Halmashauri za Wilaya kuwa na utaratibu wa kutenga maeneo kwa utekelezaji wa Miradi hii kama michango yao. Utaratibu huu pamoja na kupunguza muda wa maandalizi, utasaidia sana kupunguza gharama za Serikali katika kulipa fidia kwa watu kupisha ujenzi wa Miradi.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Fedha, malengo ya 2013 yalikuwa ni kuziongezea mtaji Benki za Maendeleo (TIB), Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na Benki ya Wanawake. Hadi kufikia Machi, TIB na Benki ya Kilimo ziliongezewa mtaji wa Shilingi bilioni kumi kila moja na Benki ya Wanawake iliongezewa Shilingi bilioni mia nne hamsini. Aidha, Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Kilimo ilizinduliwa na kuanza kufanya kazi na usaili wa Mtendaji Mkuu na Wafanyakazi wa Benki hiyo umefanyika Mwezi Machi, 2014.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa huduma za utalii, malengo yalikuwa ni kuboresha huduma za utalii ili kuvutia watalii wengi zaidi na hivyo kuongeza mapato yatokanayo na utalii. Idadi ya watalii kutoka nje ya nchi iliongezeka kutoka wastani wa 930,753 mwaka 2012 hadi 1,090,905 mwaka 2013. Mapato yaliyopatikana kutokana na utalii yanakadiriwa kufikia Dola za Kimarekani bilioni moja nukta nane moja mwaka 2013 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani bilioni moja nukta tatu saba mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyoelezwa, changamoto zifuatazo zilijitokeza na kuathiri utekelezaji. Moja ni ufinyu wa rasilimali fedha kuwezesha Miradi ya maendeleo kutekelezwa kama ilivyopangwa. Pili, ushiriki mdogo wa sekta binafsi katika uwekezaji unaozingatia vipaumbele vya mpango wa mwaka.

Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kuendelea na juhudi za kuboresha upatikanaji wa mapato ya ndani na kuwahimiza wafadhili kutimiza ahadi zao na kuzingatia mzunguko wa bajeti; na kufanya uchambuzi wa kimaabara kuhusu kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie juu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015. Maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015 yamezingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 hadi 2016) na Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2014/2015 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2010 - 2015.


Mheshimiwa Spika, napenda kulikumbusha Bunge lako Tukufu kuwa, katika Ilani ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2010 - 2015, malengo yalikuwa ni kujenga uchumi wa kisasa kwa kuboresha utoaji wa elimu, kuandaa rasilimali watu katika maarifa na mwelekeo, kufanya mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi, kufanya mapinduzi ya viwanda, kuinua matumizi ya maarifa, yaani teknolojia katika uchumi wa nchi, upatikanaji wa nishati yenye uhakika na nishati mbadala na ujenzi wa miundombinu ya kisasa. Maeneo haya ya kipaumbele yalizingatiwa na kufafanuliwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 hadi 16), ambapo sasa tuko katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2014/2015 ni wa nne katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011 hadi 16). Miradi mingi imezingatia vipaumbele vya mpango wa maendeleo wa miaka mitano na hivyo ni mwendelezo wa ile iliyokuwepo katika mpango wa mwaka 2013/2014, ambayo ina uhusiano wa moja kwa moja na maeneo ya Dira ya Taifa na Maendeleo 2025. Msisitizo umewekwa katika kuhakikisha rasilimali chache zilizopo zinatumika katika maeneo ya kipaumbele, hususan Miradi iliyo chini ya Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa. Aidha, mfumo wa ugharimiaji na utekelezaji utaimarishwa kuwezesha Miradi ya Maendeleo kutekelezwa kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Spika, Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla. Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2013/2014 umeandaliwa kwa kuzingatia shabaha na malengo ya uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2013/2014 mpaka 16, ambayo yameainishwa kwa kina katika Kitabu cha Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2014/2015. Kwa kifupi napenda kugusia yafuatayo:-

Shabaha, pato halisi la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2014, asilimia 7.4 mwaka 2015, asilimia 7.7 mwaka 2016 na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 8 mwaka 2017. Kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja, ambapo mfumuko wa bei unatarajiwa kushuka zaidi kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015. Kuongezeka kwa mapato ya ndani kufikia uwiano wa Pato la Taifa kwa asilimia 18.8 kwa mwaka 2014/2015 na kuimarisha thamani ya shilingi na kuwa na kiwango imara cha ubadilishaji wa fedha kutokana na mwenendo wa soko la fedha.

Mheshimiwa Spika, malengo: Kuendelea kuimarisha utengemavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii, kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika, kuendelea kutekeleza vipaumbele vya mpango wa kwanza wa maendeleo wa miaka mitano chini ya dhana ya Matokeo Makubwa Sasa; kuendelea kuimarisha mahusiano na Washirika wa Maendeleo; kuendelea kutekeleza sera ya upelekaji madaraka kwa Wananchi; kuendelea na utekelezaji wa maboresho katika sekta ya umma; na kupunguza utegemezi.

Mheshimiwa Spika, vipaumbele katika Mpango wa Mwaka 2014/2015: Miradi ya Maendeleo katika mwaka 2014/2015 imegawanyika katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni Miradi iliyopo chini ya Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa iliyoibuliwa kupitia awamu ya kwanza ya uchambuzi wa kimaabara katika sekta za nishati, uchukuzi, kilimo, elimu, maji na utafutaji rasilimali fedha. Kundi la pili linahusisha Miradi ya Kitaifa ya Kimkakati. Miradi ya Makundi haya mawili inalenga kutekeleza dhamira kuu ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa kutanzua vikwazo vikuu ili kufungulia fursa za ukuaji wa uchumi. Kundi la tatu linahusisha Miradi mingine muhimu kwa ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuboresha huduma za maji vijijini na mijini. Maji vijijini ambayo ni Miradi iliyo chini ya Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa; Serikali itaendelea kumalizia Miradi inayoendelea na kuanza Miradi mipya ya Maji Vijijini. Miradi ya maji mijini itakayotekelezwa ni pamoja na kumalizia kilometa 20.77 za ulazaji wa mabomba ya maji kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam na kuanza ujenzi wa miundombinu ya maji katika Mradi wa Ruvu Juu; kulipa fidia ili kupisha ujenzi wa barabara yenye km 76 kutoka Ngerengere hadi eneo la Bwawa la Kidunda; kuendelea na uchimbaji wa visima 20 katika Mradi wa Kimbiji na Mpera na kuandaa miundombinu ya kusambaza maji; kuendeleza ujenzi wa Mradi wa Kupeleka Maji Katika Miji ya Same, Mwanga na Korogwe; na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nishati, Miradi ya Kipaumbele ni pamoja na ile ya kusambaza umeme vijijini, ujenzi wa bomba la gesi (Mtwara - Dar es Salaam); mitambo ya kufua umeme Kinyerezi (MW 150 na MW 240) na Miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma (MW 600), Ngaka (MW 400) na Kiwira (MW 200). Aidha, kwa upande wa usafirishaji wa umeme, Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na uimarishaji wa njia za umeme wa msongo; kV 400 North - West Grid; kV 400 Iringa - Shinyanga; kV 400 Dar es Salaam - Tanga - Arusha; kV 400 Singida - Arusha - Namanga na kV 220 Makambako - Songea.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la miundombinu ya reli, Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na kutandika reli na mataruma ya uzito wa ratili 80/yadi kati ya Igalula - Tabora - km 37; kujenga upya vichwa 8; kununua vichwa 11; kununua mabehewa mapya 204 ya mizigo; kutafuta wawekezaji kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa reli (Dar es Salaam - Isaka - Kigali); kukamilisha usanifu kwa Reli ya Tanga - Arusha - Musoma na kukamilisha upembuzi yakinifu kwa ajli ya Reli ya Mtwara - Mbambabay na Liganga - Mchuchuma. Katika eneo la barabara, maeneo yaliyopewa kipaumbele ni barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi, zinazounganisha Tanzania na nchi jirani na zinazosaidia kupunguza msongamano mijini. Hii itajumuisha ujenzi wa km 539 na ukarabati wa km 165 wa barabara kuu kwa kiwango cha lami; ujenzi wa km 20.8 za kiwango cha lami na ukarabati wa km 914.8 za changarawe kwa barabara za mikoa; madaraja na vivuko, yakiwemo madaraja ya Mbutu - Tabora, Maligisu - Mwanza, Kilombero - Morogoro na Kigamboni - Dar es Salaam. Vivuko vitakavyopewa kipaumbele ni pamoja na kununua kivuko kipya cha Magogoni - Kigamboni na Kivuko kipya kitakachotumika kati ya Dar es Salaam - Bagamoyo, ukarabati wa vivuko vya MV Mwanza (Mwanza), MV Pangani II (Pangani - Tanga), MV Kiu (Kilombero) na MV Magogoni (Dar es Salaam).

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bandari, Miradi iliyopangwa
kutekelezwa ni pamoja na uendelezaji wa Gati Namba Moja hadi Saba katika Bandari ya Dar es Salaam; ujenzi wa bandari kavu Kisarawe; kutafuta wawekezaji kwa ajili ya Bandari yaMwambani - Tanga na ile ya Mtwara na Gati 13 hadi 14 Bandari ya Dar es Salaam; na kulipa fidia kupisha ujenzi wa Bandari ya Mbegani - Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, katika usafiri wa anga, maeneo ya kipaumbele ni kuendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria na miundobinu yake katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere na Kiwanja cha Songwe. Malengo mengine ni kuendelea kukamilisha ujenzi/ukarabati wa viwanja vya Bukoba, Shinyanga, Mwanza, Kigoma, Mpanda, Tabora, Mafia, Arusha, Mtwara na Kilimanjaro. Aidha, Serikali kwa mwaka 2014/2015 itaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja 11 vya Iringa, Musoma, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Moshi, Lindi, Njombe, Songea, Singida, Bariadi na Tanga kwa msaada wa Benki ya Dunia.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Kilimo, Miradi itakayopewa, kipaumbele ni pamoja na ile iliyo katika Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa, ambayo ni uanzishwaji wa mashamba makubwa 25 kwa ajili ya uwekezaji wa miwa na mpunga; usimamizi wa kitaalamu wa skimu 78 za umwagiliaji za mpunga na kuboresha mfumo wa soko katika skimu hizo; na kuanzishwa kwa maghala biashara (commercial warehouses) 275 ya mahindi katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi wa maghala ya nafaka Songea na Mbozi yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na kuanza na ujenzi wa maghala mengine katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uvuvi hususan eneo la bahari kuu, Serikali itajenga Bandari ya uvuvi ambapo kwa mwaka 2014/2015 itaendelea na utafiti wa kupata eneo kwa ajili hiyo na kuanza kufanya upembuzi yakinifu. Aidha, uratibu wa shughuli za uvuvi katika eneo la bahari kuu utaimarishwa ikiwa ni pamoja na kukamilisha marekebisho ya Sheria na Kanuni za Uvuvi wa Bahari Kuu.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la viwanda, Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na kuendeleza eneo maalum la uwekezaji Bagamoyo, ambapo kazi ziakazofanyika ni kufanya tathmini ya ardhi na mali, kuendelea kulipa fidia na kufanya usanifu wa kina wa miundombinu ya msingi; kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha VIUADUDU Kibaha ukihusisha kuweka miundombinu wezeshi na kuanza uzalishaji; mradi wa chuma Liganga utakaohusisha ujenzi wa mgodi na usanifu wa kina kwa ajli ya ujenzi wa kiwanda cha chuma; na ujenzi wa Kituo cha Biashara na Huduma, Kurasini, ukihusisha ulipaji wa fidia.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maendeleo ya rasilimali watu, Serikali itaendelea kuboresha ujuzi katika fani mbalimbali hususan za maeneo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Aidha, jitihada za kuwezesha vijana kusomea fani za mafuta na gesi zitaendeleea kupewa kipaumbele. Katika mwaka 2014/2015, jumla ya wanafunzi 159 watadhaminiwa katika fani za mafuta na gesi ndani na nje ya nchi. Kati ya hao, Wanafunzi 124 watadhaminiwa na Serikali na 35 watadhaminiwa na wahisani. Miradi mingine itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu, ufundi, ustawi wa jamii na ualimu; na kukamilisha mpango kabambe wa uendelezaji wa Kampasi ya Mlonganzila. Aidha, msukumo utawekwa katika mafunzo ya ufundi stadi, yanayokidhi mahitaji ya soko pamoja na mafunzo ya kuongeza ujuzi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuboresha huduma za utalii na fedha; ikiwa ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuanza kutoa huduma, kuimarisha Benki ya Rasilimali Tanzania na Benki ya Wanawake Tanzania. Aidha,
Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya utalii katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kutekeleza Miradi ya Matokeo Makubwa Sasa na ile ya Kitaifa ya kimkakati, Miradi mingine muhimu inayochangia ukuaji wa uchumi itakayozingatiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu na mafunzo; mifugo na uvuvi; afya na maendeleo ya jamii; misitu na wanyamapori; ardhi, nyumba na makazi; usafiri wa anga na majini; hali ya hewa; madini; utawala bora ukihusisha masuala ya Bunge na Mahakama; utambulisho wa kitaifa; mchakato wa kupata Katiba Mpya; uimarishaji wa biashara na masoko; uhifadhi wa mazingira; na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu na nafasi ya sekta binafsi katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji katika sekta binafsi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza utekelezaji wa mapenekezo yaliyotokana na uchambuzi wa kimaabara wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, Serikali itaelekeza rasilimali fedha zaidi katika miradi mahususi ya kufungua uwekezaji wa sekta binafsi (last mile investments). Aidha, Serikali itaendelea na juhudi za kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wa shughuli ndogondogo za kati (SMEs) kwa kuwezesha vikundi vya usindikaji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo; kuendelea kuboresha huduma na miundombinu ya usafirishaji, nishati na mawasiliano na kuendelea kuboresha mfumo wa usimamizi na kuvutia sekta binafsi ktika utoaji wa huduma hasa elimu na afya.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015 Serikali imekadiria kutumia jumla ya shilingi trilioni 6.44, sawa na asilimia 32.8 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 4.42 sawa na asilimia 68.7 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.02 sawa na asilimia 33.3 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za nje. Serikali itaendelea kugharimia Miradi ya Maendeleo kupitia vyanzo vingine vya fedha kama vile ubia katika ya sekta ya umma na binafsi pamoja na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kuwekeza katika maeneo ya kipaumbele ya mpango.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali itaendelea na utaratibu wa ufuatiliaji kama ilivyoainishwa katika mwongozo wa Mpango na Bajeti 2014/2015. Katika utaratibu huo, suala la ufuatiliaji na tathmini kwa miradi ya kimkakati litabaki kuwa jukumu la Tume ya Mipango na Sekta husika. Miradi ya Matokeo Makubwa Sasa itafuatiliwa na PDB; na Miradi ya ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa itakuwa ni jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na mikoa husika. Vilevile, Serikali itaendelea kutumia mfumo mpya wa usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya Miradi ya Maendeleo katika mwaka 2014/2015 ili kuleta matokeo makubwa kwa haraka.

Mheshimiwa Spiia, baada ya kuelezea hali ya Uchumi wa Taifa, matarajio, misingi na malengo, mwenendo wa ukuaji wa uchumi jumla kwa mwaka 2013 na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2013/2014, ni dhahiri kuwa, Serikali imepiga hatua za kuridhisha katika kutekeleza Programu/Miradi mbalimbali ya maendeleo. Changamoto kubwa iliyopo ni kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ili ukuaji wa uchumi uweze kuwiana na maendeleo kwa kumnufaisha Mwananchi wa kawaida kuondokana na umaskini.

Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015 umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kwa namna ambayo ni shirikishi ili kupunguza umaskini. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Benki ya Kilimo Tanzania inaanza kufanya kazi ili kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa mikopo kwa wakulima; kuhusisha programu na mikakati ya kinga ya jamii inayosimamiwa na TASAF, ikijumuisha uhawilishaji fedha kwa masharti maalum (conditional cash transfers) kwa makundi yenye umaskini uliokithiri; kutekeleza programu za kuwawezesha Wananchi kiuchumi; kuwezesha taasisi za wakulima wadogo kupitia vyama vya ushirika na kilimo cha mkataba; na kuendelea kutekeleza Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge kupitia MKUTABITA.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri wa rasilimali ya gesi asilia. Kuna haja ya kujipanga vizuri kutumia utajiri huu kwa manufaa ya Wananchi. Katika kufanikisha hili, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kutayarisha nchi kuingia katika uchumi wa gesi ikiwa ni pamoja na kukamilisha Sera ya Gesi Asilia; kuendelea na maandalizi ya Sheria ya Gesi Asilia; Mkakati Kabambe wa Matumizi ya Gesi na Sera ya Ushirikishaji Wananchi Kwenye Biashara ya Gesi (Local Content Policy). Aidha, Serikali inapitia Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (Public - Private Partnership - PPP) kwa nia ya kuweka mazingira mazuri zaidi ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika Miradi ya Maendeleo hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, dalili nzuri za kuwekeza katika Ukanda wa Kusini (Lindi na Mtwara) zimeanza kuonekana, ambapo ujenzi wa viwanda vya Saruji vya Dangote (Mtwara) na METS (Lindi) unaendelea. Vilevile, maandalizi ya uwekezaji katika viwanda vya mbolea, Liquified Natural Gas (LNG), mitambo ya kufua umeme kutumia gesi asilia na njia za usafirishaji wa umeme katika Ukanda wa Kusini yameanza.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hili, Serikali katika mwaka 2014/2015 itaanza kutekeleza Programu ya Kukuza Ajira kwa Vijana, ili kuboresha upatikanaji wa ajira kwa vijana. Programu hii ni ya miaka mitatu (2014/2015 - 2016/2017), inatarajiwa kusaidia upatikanaji wa mafunzo ya ujasiriamali na mikopo kwa vijana wanaomaliza elimu katika ngazi mbalimbali. Aidha, programu hii imelenga kuainisha mikakati na hatua mbalimbali za kuchukua ikiwa ni pamoja na kuweka mgawanyo wa majukumu ya kutekelezwa na sekta na tasisi mbalimbali kuwezesha vijana wengi zaidi kuajiriwa na kujiajiri. Vilevile, Serikali imelenga kuendeleza vijana kwa kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu, naomba kuwashukuru Watendaji wote wa Ofisi ya Rais (Tume ya Mipango), wakiongozwa na Katibu Mtendaji, Dkt. Philip I. Mpango na Naibu Makatibu Watendaji, kwa kusimamia vizuri kazi za kila siku za Tume ya Mipango na katika mandalizi ya Hotuba hii. Pia Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (Mb), Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Watenaji wote wa Wizara ya Fedha, kwa kufanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Aidha, nawashukuru Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Gavana wa Benki Kuu, Mtendaji Mkuu wa PDB, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja na Watendaji wao wote, kwa ushirikiano waliotupatia. Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, nitoe shukrani za pekee kwa Wananchi wa Jimbo la Bunda, kwa kuendelea kunipa ushirikiano katika kazi za Jimbo pamoja na majukumu mengine ya Kitaifa.

Mheshimiwa Spika naomba sasa Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2013/2014 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015. Kabla sijatoa hoja, ninaomba kuwatakia heri washabiki wote wa mpira, kwa kazi inayoendelea kule Brazil.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Wasira, Stephen Masatu[CCM]
 
Pato la Taifa, mwaka 2013 lilikuwa shilingi trilioni 53.17, sawa na Dola za Kimarekani bilioni 33.26 ikilinganishwa na shilingi trilioni 44.72 mwaka uliotangulia 2012, sawa na Dola za Kimarekani bilioni 25.24. Hivyo, wastani wa pato la mwananchi kwa mwaka 2013 lilikuwa shilingi 1,186,200, sawa na Dola za Kimarekani 742, ikilinganisha na shilingi 1,025,038, sawa na dola 652.1 mwaka 2012, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.7.
 
Katika mwaka 2013 pekee, thamani ya uwekezaji nchini, total investment, ilikuwa takribani Dola za Kimarekani bilioni 11.37 ikilinganishwa na dola bilioni 8.75 mwaka 2012. Ongezeko hili linatokana hasa na uwekezaji katika miundombinu ya usafiri, ujenzi, nishati, maji na kilimo. Aidha, uwekezaji wa mitaji ya kigeni na moja kwa moja foreign direct investment ilikuwa Dola za Kimarekani bilioni 1.88 mwaka 2013, ikilinganishwa na dola bilioni 1.80 mwaka 2012. Ongezeko hili kwa kiasi kikubwa linatokana na uwekezaji katika sekta ndogo ya gesi.

Nina mambo mawili nomba uyaweke wazi ii nasi wananchi tuhisi hilo ongezeko
1. Ni vipi ongezko hilo linamtoa mawananchi kutoka katika lindi la umaskini?
2. Mkuu nikusihi ubadilishe hizo figure kutoka USD kuwa Tshs. itapendeza, si kwamba sijui ili kwa kuwasaidia wasiojua kwani kwa sasa mwanachi ukimwambia tilioni au bilioni anakulewa. Ni hayo tu mkuu
 
amefanikiwa pia katika upatikanaji wa huduma za Afya, Elimu na Maji. Kwa upande wa Afya, Tanzania imefanikiwa kufikia Lengo la Milenia Namba Nne ikiwa imepunguza vifo vya watoto wachanga toka 191 mwaka 2000 mpaka vifo 51 kati ya watoto 1000 mwaka 2013. Aidha, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vilipungua kutoka 115 mwaka 2000 hadi vifo 54 kati ya watoto 1000 mwaka 2013.
 
kwenye ardhi ni vurugu tupu,foreigners wamepora ardhi ya wazawa wakishirikiana na mafisadi!
 
Tutamkumbuka sana Rais Kikwete. Kafanya mengi mazuri kwa taifa hili. Anang'ara kitaifa na kimataifa
 
Back
Top Bottom