Serikali ya Tanzania imesema kuwa, imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya kubaka yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi wa nchi hiyo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Shirika la habari la Xinhua limewanukuu viongozi wa Tanzania wakisema jana kuwa, wameanzisha uchunguzi kuhusu wanajeshi hao wanaofanya kazi ya kulinda amani nchini Kongo DR chini ya mwavuli wa kikosi cha Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania, Hussein Ali Hassan Mwinyi amesisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimeanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.
Siku ya Ijumaa, askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walisema kuwa, wamepokea malalamiko kwamba wanajeshi wa Tanzania wametenda vitendo vya ubakaji na kinyume na maadili yao ya kazi mashariki mwa DRC.
Kamandi ya operesheni za kijeshi ya kikosi cha Umoja wa Mataifa Monusco imesema, tarehe 23 Machi mwaka huu kulitolewa madai kuwa wanajeshi wa kikosi hicho wametenda vitendo hivyo katika kijiji cha Mavivi mkoani Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC na kwamba kikosi hicho hivi sasa kimeanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.