Kwa wale watumiaji wa barabara za Dar es salaam bila shaka watakuwa wanamfahamu fika huyu polisi anayejulikana kwa jina la AWADH mwenye cheo cha SP ambaye mara nyingi huwa namuona kwenye barabara ya Al-Hassan Mwinyi hasa maeneo ya ubalozi wa Ufaransa na sehemu zenye utata wa foleni.
Kwanza kabisa ningependa kumpongeza kwa juhudi binafsi anazozionyesha na kujituma kwa manufaa ya watumiaji wa barabarani, lakini hata hivyo Wahenga hawakukosea waliposema ''Kizuri Hakikosi kasoro''.
Nina maana gani kusema hivyo? Labda niwape mkasa kidogo kuhusiana na huyu Askari wa Usalama barabarani ambao nimeushuhudia kwa macho yangu asubuhi kweupe pasi na kupepesa.
Nilikuwa nipo kwenye foleni naelekea City Center kwenye shughuli zangu za kujitafutia mkate wangu wa kila siku, nilipofika maeneo ya Ubalozi wa Ufaransa nikawa natazama magari yaliyokuwa yanatoka kwenye barabara ya OCTAS ambapo kwa wakati ule yalikuwa mengi.
Ghafla Awadh akawa amefika eneo la tukio akiwaelekeza madereva namna ya kuweza kupita na kupunguza msongamano, wakati akiwapa maelekezo na kuyaruhusu magari mengine kuingia kwenye barabara ya Al Hassan mwinyi, kuna mwanadada mmoja alikuwa yupo ndani ya gari yake aina ya IST rangi ya cream.
Huyu mwanadada alikuwa kwenye foleni ileile aliyokuwa ikiongozwa na Awadh, lakini katika hali ya kushangaza Awadh alimfuata yule dada akaanza kumchapa makofi na kama kuona hiyo haitoshi akamchomolea upepo wa tairi ya kulia ya gari yake na kumnyang'anya funguo.
Yule Dada akawa analia huku amelalia usukani wa gari, kusema ukweli kitendo kile kiliniuma sana hasa ukizingatia jinsia zao ni tofauti na mbaya zaidi yule ni mtoto wa kike.
Moja kwa Moja nadhubutu kusema alimfanyia unyanyasaji wa kijinsia kweupe, nilitamani nitoke kwenye usafiri wangu niende nikamtete sema kuna roho ikaniambia nisiende.
Nikawa najiuliza kama yule mwanadada amekosea, why hakufuata taratibu za kumpiga faini mpaka amdhalilishe kiasi kile?
Afande Awadh tunakuhiji ubadilike na kama huwa unafanikiwa kuingia huku bila shaka utakuwa umeshapata ujumbe wako.