Hali ya upigaji kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji leo tarehe 27, Novemba 2024 mpaka muda huu wa saa 8 kamili mchana.
TUKIO LA SHAMBULIZI
Kwa masikitiko makubwa tunapenda kuujulisha umma kuhusu tukio la kusikitisha lililotokea ambapo Katibu wa Jimbo la Igunga Ndugu Erick Yugalila Venance majira ya saa 3 asubuhi leo tarehe 27 Novemba ameshambuliwa na kuumizwa vibaya na vijana waliokuwa na pikipiki za CCM. Lakini pia kupigwa kwa mawakala Jimbo la Arusha Mjini Kata ya Osunyai. Tunalaani vikali vitendo hivi vya kihalifu na tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa haraka na wahusika wafikishwe mbele ya sharia.
KUKAMATWA KWA KURA ZILIZOPIGWA
Tumepokea taarifa ya kukamatwa kwa kura feki majira ya saa 12 alfajiri eneo la Mwandiga. Aliyekamatwa na kura hizo ni mgombea na alipohojiwa alisema kuwa kura hizo amepewa ili azifikishe kituoni.
Kituo cha Nyamalele na Nkome Center huko Jimbo la Geita Vijijini nako watu wamekamatwa na karatasi zilizopigwa kura tayari.
MAWAKALA KUTOPEWA BARUA ZA UTAMBULISHO NA KUTOKURUHUSIWA KUINGIA VITUONI.
Mawakala wameripoti kutopewa barua za utambulisho asubuhi na badala yake wasimamizi wa vituo wanawaambia wafuate barua hizo kwenye Ofisi ya Mtendaji huku zoezi la upigaji kura likiwa linaendelea kwenye vituo.
Arusha nako mawakala wameambiwa wakae nje ya kituo wakati maboksi ya kura yako ndani ikiwa ni kinyume na kanuni na utaratibu. Mawakala wamegoma na badala yake wameitiwa polisi wawakamate. Maeneo mengine ni Kijiji cha Njopeka kata ya Lukanga Mkuranga na Kijiji cha Mandaka Mnono kilichopo kata ya Old Moshi Magharibi, mawakala hawajaruhusiwa kuingia kwenye chumba cha kupigia kura licha ya kuwa na nakala za kiapo zenye muhuri wa Mtendaji Kata. Mbeya kata ya Mpemba mtaa wa Nasele mawakala 8 wameondolewa kwenye kituo.
WAGOMBEA WA ACT WAZALENDO KUTOLEWA KWENYE KARATASI YA KUPIGIA KURA
Maeneo mengi tumepokea taarifa ya kuwa wagombea wa ACT Wazalendo wameondolewa kwenye karatasi ya kupigia kura; hawa ni wagombea ambao wamethibitishwa na barua kuwa ni wagombea. Hili limetokea kwenye Kitongoji cha Bwejuu Kata ya Kilindoni Mafia Mgombea wa Nafasi ya Uwenyekiti wa Kitongoji.
Sebastiani Philipo Kimita wa Kata ya Itebula kitongoji cha Lugongoni B Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma. Kata ya Mganza mgombea nafasi ya uwenyekiti katika kijiji cha Kasisi naye ameondolewa. Mgombea wa uwenyekiti Kitongoji cha Mambwe katika kijiji cha Iyebula, Masasi kata ya Lulindi, Muheza Kijiji cha Mbwembwera kata ya Bwembwera na tunaendelea kupokea taarifa za maeneo mengine.
MATUKIO LA KUKAMATWA NA POLISI
Zaidi ya hayo, tumepokea taarifa ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Ndugu Yassin Mohammed Mawila pamoja na dereva wa chama Ndugu Dubai Mchondo katika Kijiji cha Kajima Kata ya Jakika wakiwa katika harakati ya kuzuia kuondolewa kwa mawakala wa ACT wazalendo vituoni. Pia Mwenyekiti wa kata ya Mandaga jimbo la Pangani naye amekamatwa na polisi.
Tunalaani vikali matendo yote yanayofanyika kinyume na kanuni na taratibu za uchaguzi na tunaitaka mamlaka zinazohusika kuchukua hatua zinazostahili ili kuruhusu uchaguzi uwe huru na haki. Tutaendelea kutoa taarifa kadri tutakavyopokea katika maeneo ambayo yanapitia changamoto.
Imetolewa na;
Rahma Mwita,
Msemaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ACT Wazalendo.
27 Novemba 2024