SoC03 Watanzania tutumie 'akili mnemba' kuchochea utawala bora

Stories of Change - 2023 Competition

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,399
Kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita maneno "utawala" na "utawala bora" yametumika katika muktadha wa kuhamasisha maendeleo. Utawala mbaya unatajwa kuwa kisababishi cha maovu yote ndani ya jamii. Wafadhili na taasisi za fedha za kimataifa zinaegemeza misaada na mikopo yao kwa masharti kwamba Serikali au Taifa nufaika linahakikisha linafanya mageuzi ambayo yanachochea utawala bora.

Nini maana ya utawala bora?
Utawala bora ni mchakato wa kupima jinsi taasisi za umma zinavyoendesha shughuli za umma na kusimamia rasilimali za umma na kuhakikisha upatikanaji wa haki za binadamu kwa namna ambayo kimsingi haina dhuluma na rushwa na kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Je, akili mnemba ni nini?

Hii ni teknolojia inayowezesha mashine kufanya kazi kwa kuiga uwezo wa binadamu wa kuhisi, kuelewa na kutenda. Akili Mnemba ama waweza kuita Akili Bandia (Artificial Intelligence), ni akili au uwezo inaooneshwa na mashine, tofauti na akili ya asili inayooneshwa au kutumiwa na wanadamu au wanyama, ambayo inahusisha ufahamu na hisia.

Akili mnemba (AI) ina uwezo wa kuboresha masuala mengi ya kimaendeleo lakini Mimi nitajikita katika kuangalia namna inaweza kutusaidia kuchochea misingi ya utawala bora kwa nchi yetu Tanzania.

1687769781067.png

Picha ni ubunifu wa Kurziweil, kwa msaada wa programu tumishi (application)

Akili mnemba itatusaidia kuifanya Serikali kuwa na ufanisi zaidi katika kutoa huduma kwa Watanzania wote. teknolojia ya akili mnemba inaweza kurahisisha mwingiliano kati ya wananchi na mashirika ya serikali kuwa rahisi na ufanisi zaidi. Sote ni mashahidi kuhusu huduma zinazotolewa kwenye ofisi za umma au kupitia tovuti za Serikali sio rafiki sana. Tuboreshe kwa kuongeza teknolojia ya akili mnemba ili kuongeza tija na ufanisi katika kuwahudumia Wananchi. Mathalani matumizi ya Chatbots yanaweza kusaidia sana kutoa taarifa kwa umma kuliko kulazimisha wapige simu au kufika katika majengo ya serikali. Tutaokoa muda na fedha za usafiri.

Akili mnemba itusaidie kuchochea demokrasia kwa kupitia Demokrasia ya Kielektroniki au ‘e-Democracy’ hii itatoa fursa ya watu kushiriki michakato ya kidemokrasia kwa njia ya mtandao. Hadi mwaka 2019 watanzania milioni 42.9 ndio waliokuwa wakimiliki simu janja na hadi 2023 idadi hii itakuwa imepanda maradufu. Matumizi ya akili mnemba yatasaidia sana hata kwa uchaguzi wa 2025 kwani vijana wengi wataweza kushiriki kupiga kura kwa kutumia mifumo ya kielekriniki (e-vote) ambayo ni rafiki zaidi kwao kuliko kuwataka wajitokeze alfajiri kwenda kupanga foleni ili wapige kura jambo ambalo linaweza kuwa kero kwao.

Uwajibikaji ni sehemu nyingine ambayo akili mnemba au akili bandia inaweza kutusaidia kuleta matokeo Chanya. Tukumbuke kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977 inaitaka Serikali (viongozi na watendaji) kuwajibika kwa wananchi. Kama mifumo ya akili mnemba itaunganishwa na mifumo na tovuti za taasisi za Serikali kama vile TAKUKURU na Jeshi la Polisi itasadia sana utoaji wa taarifa za ubadhirifu ama uzembe ili TAKUKURU na Jeshi la Polisi waweze kuchukua hatua za kiuchunguzi. Endapo TAKUKURU na Jeshi la Polisi pia watazembea kuchukua hatua akili mnemba inaweza kutumika kutoa takwimu za ripoti zilizotolewa bila ya hatua kuchukuliwa.

Utawala wa sheria pia unaweza kuboresha na teknolojia ya akili mnemba hii inawezekana kupitia teknolojia ya ‘Chatbots’. Mwananchi anaweza kuuliza na kujifunza haki zake za kikatiba na hivyo anaweza kufuatilia kama huduma anayopewa inakidhi vigezo vya usawa mbele ya sheria au kuchambua kama uendeshaji wa shughuli za umma pamoja na maamuzi yanafanyika kwa kufuata sheria za nchi. Elimu ni silaha kubwa katika kudai haki, ‘chatbots’ ni rahisi mno.

Pia akili mnemba inanafasi kubwa ya kutusaidia kulinda haki za binadamu: teknolojia hii inaweza kutumika kufuatilia na kuandika taarifa na takwimu sahihi za ukiukaji wa haki za binadamu, kama vile ukatili wa polisi, ubaguzi wa kisiasa, na udhibiti wa wanaharakati. Hii inaweza kusaidia kuwawajibisha wahusika na kutoa ushahidi kwa hatua za kisheria.

Matumizi ya akili mnemba au akili bandia katika huduma ya afya zinaweza kutushangaza kama tutaweza kuitumia ipasavyo. Matumizi ya teknolojia hii katika huduma ya afya yatasaidia sana katika kuboresha jinsi tunavyochakata data ya huduma ya afya, kutambua magonjwa, kuendeleza matibabu na hata kukomesha kabisa magonjwa ya mlipuko. Kwa kutumia akili bandia katika huduma za afya, wataalamu wa matibabu wanaweza kufanya maamuzi yenye ufanisi zaidi kulingana na taarifa sahihi Zaidi wanazozipata kwenye akili mnemba, wataokoa muda, watapunguza gharama na kuboresha usimamizi wa rekodi za matibabu kwa ujumla.

1687769148490.png

Picha ni ubunifu wa Kurziweil, kwa msaada wa programu tumishi (application)

Kwasasa ukifuatilia muda ambao mgonjwa anautumia katika hospitali zetu kuanzia hatua ya kupokelewa, kujiandikisha, kumuona daktari, kufanyiwa vipimo na kuanza matibabu ni takribani saa 8. Tukianza kutumia akili mnemba kwenye sekta ya afya basi ni dhahiri wagonjwa watapokea huduma bora kwa haraka na kwa usahihi zaidi kuliko hivi sasa.

Kuboresha upatianaji wa haki ya kupata habari: teknolojia ya ‘Chatbots’ na barua pepe zinazoendeshwa kwa akili mnemba zinaweza kutumika kuwapa wananchi taarifa sahihi na za kisasa kuhusu sera, huduma na taratibu za serikali. Hii inaweza kusaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji, na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu zaidi katika mchakato wa kidemokrasia.

Uwazi ni hali ya kuendesha shughuli za umma bila usiri na kificho ili wananchi wawe na uwezo wa kupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria. Teknolojia ya akili mnemba ikiunganishwa na mifumo ya Serikali inaweza kutumika kuhifadhi, kupanga, na kuwapa fursa wananchi na wadau kufuatilia nyaraka muhimu, kama vile taarifa za fedha za Serikali kwa ngazi zote na mikataba mbalimbali ambayo viongozi wameingia au wanakusudia kutia saini.

Hitimisho,
Matumizi ya akili mnemba na teknolojia ya mawasiliano kwa ujumla wake hayaepukiki kabisa kwa Tanzania ya leo. Tukumbuke kuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) hivi karibuni imepewa dhamana ya kuhakikisha inapanua mkongo wa Taifa baada ya kusaini mkataba wa Sh37.3 bilioni na na Kampuni ya Huawei Tanzania kwa ajili ya upanuzi wa kuzifikia wilaya 23 nchini. Serikali inaamini kwamba upanuzi huu utaleta mabadiliko makubwa katika maeneo hayo, ambayo baadhi hayana mawasiliano kabisa.

Lakini ili teknolojia ifikie uwezo wake kamili tunahitaji kubadilisha kwanza mitazamo ya watu tuliowachagua na kuwaamini kuendesha serikali yenyewe kwa niaba ya Wanzania 59,851,357 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022, baadhi ya sera na sheria zinazohusu maendeleo ya TEHAMA.​
 
Back
Top Bottom