Riwaya ya kipelelezi: Wakala wa Siri

siri.jpg



WAKALA WA SIRI 10
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300

ILIPOISHIA
Hatimaye alimaliza kununua bidhaa zote alizoagizwa, lakini alivutiwa na matunda Fulani yaliyokuwa na maganda ya rangi ya njano, alipouliza aliambiwa yanaitwa ā€˜Sambiaā€™ aliyaonja, Dooh! Yalikuwa yana sukari na ukakasi, ndani yake yakiwa na mbegu za rangi ya huzurungi.
Muda ulikuwa umeenda sana, jua lilikuwa kali yapata mida ya saa sita. Sajenti akarudi Nkwini kwa Babu yake akiwa amefurahia safari yake, roho yake ilisuuzika, mji wa Makanya uliamsha chemchem ya uhai na ari moyoni mwake.
***************************

INAENDELEA

Usiku uliingia, giza nalo likafungua mdomo wake likaumeza mji wa Nkwini. Siku ile anga lilitawaliwa na Mawingu makubwa meusi yenye kutisha. Sajenti na Mzee Mkwizu walilala kama ilivyokuwa desturi ya wanadamu wote kulala usiku. Siku hiyo Sajenti alikuwa amechoka kuliko siku zote, alichoshwa na mizunguko ya mchana ya sokoni, Makanya. Leo alilala fofofo mithili ya pono. Hata angeota ndoto lazima ingekuwa ndoto yenye kutisha, yenye kufisha na kulegeza mwili na roho.
Huko nje Kajiru alikuwa akibweka Huu! Huuu! Wakati wengine wakiwa wamelala wasijue nje kuna zimwi linalokuja kuwala. Kajiru alibweka, sasa muda huu sauti ikiwa imeongezeka ikiwa na wehu ndani yake. Tayari mvua ilianza kunyesha hali iliyofanya sauti ya kubweka kwa Mbwa, ndiye kajiru kutosikika vizuri kutokana na bati kupiga kelele zilizosababishwa na matone ya mvua. Nje walikuwepo wanaume sita, waliovalia makoti makubwa meusi ya mvua, wakiwa wameshikilia bunduki aina ya SMG. Walishaingia kwenye uzio wa nyumba ya Mzee Mkwizu, Sauti ya Mbwa iliwafanya waongeze tahadhari, wakimtafutia shabaha ya kumlenga ili kumuua asiendelee kubweka kwani walihofia sauti yake ingewaamsha wakina Sajenti.
Wakwanza kushtuka usingizini alikuwa Mzee Mkwizu, akiwa kitandani alisikia kwa mbali Mbwa wake akilia huku Mvua kubwa ikinyesha. Aliamka kitandani na kuwasha tochi yake aliyokuwa kaiweka chini ya mto wa kitanda, kisha akachukua gobore lake, akatoka kwenda sebuleni.
Alipofika sebuleni alishtuka kuona mlango ukicheza cheza, ni kama kuna mtu alikuwa anataka kuvunja kitasa. Hapo akakoki gobore lake akimulika mlango. Mapigo ya moyo wake yalienda upesi mno, miguu na mikono yake ilianza kutetemeka. Muda huo Sajenti hana hili wala lile, kalala kwa starehe ungedhani dunia anaimiliki yeye. Asijue hatari inayowakabili.

Kitu pekee kilichowashinda ni ule mlango jinsi ulivyotengenezwa, pia ulikuwa ni mlango wa mbao ngumu ya mninga. Hivyo haikuwa rahisi kwao kuuvunja. Basi walichukua baruti ya kuvunjia wakaitega pale mlangoni, kisha wakasogea umbali wa mita kadhaa, wakati huo Mzee Mkwizu kasimama akiwa kajiandaa kumpiga yeyote atakayetangulia. Masikini, hakuwa na bahati. Mlango ulifumuliwa na baruti, Mzee Mkwizu alipigwa na kipande cha mbao kichwani akaanguka chini. Mshindo na sauti ya baruti ilimshutua Sajenti. Upesi akaamka akaichukua bastola yake.
Aliamka akiwa na kaptura, akachungulia sebuleni. Hapo macho yake hayakuamini, alimuona Babu yake akiwa kaanguka akiwa kashika tochi iliyokuwa inamulika mlangoni, alipagawa alipoona mlango umevunjwa. Hapo akajua kuna hatari kubwa inakuja. Akili yake ilimuonya, ikamuambia asifanye haraka kwenda kumuangalia Babu pale chini. Punde alishtuka kuona jitu kubwa lililovaa koti kubwa jeusi la mvua likiwa limenyeshewa likiingia kwenye ule mlango wa sebuleni. Jitu lile lilikuwa limebeba bunduki mkononi. Sajenti hakutaka kuwa na haraka kulipiga risasi, alisubiri aone kuwa lipo lenyewe ama lipo na wenzake. Punde akatokea mtu mwingine, huyu alikuwa mfupi mfupi, naye alikuwa kavaa koti la Mvua. Yule mtu wa pili aliingia akaichukua ile tochi na kuanza kumulika mulika. Kosa! Alifanya kosa ambalo hatajisamehe daima. Wote wawili walijikuta wakianguka chini baada ya Sajenti kuwapiga risasi. Jambo hilo lilifanya wale maadui wanne waliobakia nje kupiga risasi bila mpangilio. Sajenti akajua kuna maadui wengine lakini hakujua hesabu yao.
Sajenti alimuona Mzee Mkwizu akizinduka kichwani akiwa na jeraha lilokuwa linavuja damu, Mzee Mkwizu kabla hajafanya chochote wale watu walimtandika risasi tatu za kifuani wakiwa wapo kwa nje.

Sajenti aliumia sana. Alikumbuka maneno ya Babu yake siku alipofika aliyomwambia kuwa amekuja na mkosi. Sajenti roho yake ilizimia kwa maumivu. Alisikitika kuona maneno ya Babu yakitimia.
Akatoka kwenye ile kona akaenda kwa kunyata mpaka karibu na mlango wa sebuleni, akalala chini alafu akachungulia kwa nje, hapo akawaona watu watatu wakiwa wamesimama wakitazama ndani wakiwa wamebeba bunduki zao. Alichukua bastola yake kisha kwa upesi alijiviringa kama gunzi la mhindi na kuwapiga kwa mpigo, wote watatu wakadondoka chini. Awali niliwaambia kuwa hakuna mchezo anaoupenda na kuuweza Sajenti Warioba kama mchezo wa kutupiana risasi. Sajenti alikuwa na shabaha, hakuwahi kukosa pale atakapo kulenga mtu. Jeshini walimfahamu kama mkono wa Shabaha. Akipewa risasi kumi auwe watu kumi basi tambua kuwa kila risasi itaondoka na mtu mmoja kama alivyoagizwa. Sasa kulikuwa kimya kabisa, Sajenti akajua amemaliza kazi. Sajenti alisimama akaenda kwa Babu yake, alimkuta tayari ameshakufa. Alilia kama mtoto mdogo, alijiona yeye ndio chanzo cha kifo cha Babu yake. Kama si yeye kuja hapo basi Mzee Mkwizu asingekufa.
ā€œKweli mimi ni Mkosi, Babu mimi ni mkosi. Tazama sasa maneno yako yanatimia. Bora ningekuja kukuzika lakini sio kusababisha kifo chako. Babu yangu nisameheā€ Sajenti alilalamika mwenyewe akilia kama mwendawazimu huku Mvua ikiendelea kunyesha.
Punde akiwa kapiga magoti akilia aliduwaa baada ya kisogo chake kuguswa na kitu kigumu, ndio alikuwa kawekewa bastola kisogoni na yule mtu wa sita, masikini Sajenti alijua amewamaliza wale watu wabaya lakini kumbe alikuwa amembakiza mmoja. Huyo ndiye sasa aliyemuweka chini ya ulinzi.
ā€œMikono juu, utulie hivyo hivyo, vinginevyo leo hii utamfuata Babu yako kuzimuā€ Yule Mtu aliongea kauli ya kibabe sana sauti yake ikikaribia sauti ya jinamizi mkatili asiye na chembe ya huruma.

Sajenti aliinua mikono yake juu bila ya ubishi, sauti ile aliielewa sana. Hakutaka kuleta ubishi ambao alijua ungegharimu maisha yake. Ghafla Mbwa alitokea akamvamia Yule mtu kwa nyuma na kuanza kumshambulia yuule jambazi akiwa kaanguka chini. Sajenti akaona ile ndio nafasi ya kujinasua, alinyanyuka chapuchapu kama umeme lakini alichelewa, kabla hajafanya chochote Yule mtu aliachia risasi ikampiga na kumuua Yule Mbwa, ndiye Kajiru. Sajenti hasira zilimpanda kama mbogo wa Mikumi aliyejeruhiwa, alimpiga Yule mtu risasi mfululizo hata alipopoteza maisha Sajenti aliendelea kumpiga risasi bila kuacha, Risasi ziliisha kwenye bastola ikawa ndio mwisho wa Sajenti kumpiga risasi.
Usiku huohuo Sajenti alitoka nje akaenda kuchimba kaburi la Babu yake karibu na Zizi la ngā€™ombe huku manyunyu ya mvua yakimdondokea. Mwanga wa jua la asubuhi ulimkuta akiendelea kuchimba, ngā€™ombe, mbuzi na kondoo walimtazama Sajenti wakiwa na nyuso zenye simanzi. Leo hii Bwana wao, Mzee Mkwizu amekufa kwa kuuawa na watu wabaya wasio na huruma. Ndama mmoja mweupe alikuja karibu na kaburi akawa anamtazama Sajenti akiwa ndani ya kaburi akichimba kaburi. Sajenti alimuona yule ndama, hapo akajikuta akipatwa na huzuni.

Alimaliza kuchimba Kaburi, hapo akarudi ndani jua lilikuwa limeshapanda juu kabisa. Maiti Saba ya watu pamoja na mzoga wa Mbwa, ndiye kajiru zilikuwa zimelala pale chini. Aliubeba mwili wa Babu yake kisha akaenda kuusafisha vizuri bafuni. Alafu akaenda ndani akachagua nguo nzuri aliyoiona itamfaa Marehemu Babu yake kumzikia. Aliona Suti nzuri mno ya rangi nyeusi, akamvalisha Babu yake. Kisha akaendelea kukagua lile sanduku la nguo, hapo akaona kanzu nzuri ya zambarau na kikofia cha kichifu. Akaivaa ile kanzu na kile kikofia.
Akaubeba ule mwili wa Babu yake, kisha akarudi kuuchukua mzoga wa Kajiru, baadaye akauingiza mwili wa Babu yake kaburini na mzoga wa Mbwa wake. Alipoiingiza kaburini hiyo miili, akaenda kufungulia ngā€™ombe. Mbuzi na kondooo. Hao ndio walikuwa mashuhuda wa mazishi ya Mzee Mkwizu Mifugo yote ililizunguka kaburi. Kisha Sajenti akiwa kavaa kanzu ya zambarau na kofia nyekundu akiwa kama Kuhani anayeendesha maziko hayo. Sajenti aliomba dua ya kumuombea Babu yake, kisha akamzika Babu yake pamoja na Mbwa wake.
Hivyo ndivyo shujaa Mzee Mkwizu alivyozikwa kwa heshima na Sajenti pamoja na mifugo yake. Akaliliwa na Mjukuu wake na mifugo yake kwa siku tatu. Sajenti akachukua maziwa aliyoyakamua kwenye ngā€™ombe na mbuzi na kuyamwagia kwenye kaburi lake. Kisha akachukua mafuta ya mkia wa moja ya kondoo zake akayamwagia katika kaburi lake. Mwisho akachinja kuku na kuchoma manyoya yake katika kaburi lake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa, na habari zake Sajenti akazichukua ili kuziandika kama alivyozikuta katika sanduku la kuhifadhia historia ya maisha ya Mzee Mkwizu.

ITAENDELEA

Usisahua ku-like na kushare.
Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.

Kitabu Tsh 15,000


0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel.

0758216209
M-PESA
Robert Heriel
 
WAKALA WA SIRI 11
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300

ILIPOISHIA......
Hivyo ndivyo shujaa Mzee Mkwizu alivyozikwa kwa heshima na Sajenti pamoja na mifugo yake. Akaliliwa na Mjukuu wake na mifugo yake kwa siku tatu. Sajenti akachukua maziwa aliyoyakamua kwenye ngā€™ombe na mbuzi na kuyamwagia kwenye kaburi lake. Kisha akachukua mafuta ya mkia wa moja ya kondoo zake akayamwagia katika kaburi lake. Mwisho akachinja kuku na kuchoma manyoya yake katika kaburi lake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa, na habari zake Sajenti akazichukua ili kuziandika kama alivyozikuta katika sanduku la kuhifadhia historia ya maisha ya Mzee Mkwizu

INAENDELEA....

Ikawa baada ya Sajenti Kumzika Babu yake, ndiye Mzee Mkwizu. Sajenti aliondoka katika Kijiji cha Saweni akiwa kauza mifugo ya Babu yake, aliuza ngā€™ombe, mbuzi, kondoo na Kuku. Hapo akapata fedha ambazo ni shilingi milioni tisa, akiwa kauza kwa bei ya kutupa. Lakini kama angeuza kwa bei halisi basi Sajenti angekuwa amepata zaidi ya pesa hizo. Sasa alikuwa karudi Dar es Salaam, hakutaka kubaki pale kwenye Kijiji cha Saweni kwani tayari ilishagundulika kuwa anaishi pale.

Alichukua chumba Mtoni Mtongani, akanunua kitanda na Godoro. Sasa alianza maisha mapya ya kujificha, maisha kama panya ndiyo aliyoanza kuyaishi. Aligeuka popo, akawa analala mchana na kutoka usiku kwenda kuzunguka zunguka katikati ya mji.
Mtoni Mtongani mpaka kwa AZIZI ALLY alikutana na Mateja wengi wa Unga, alisikitika kuona vijana wengi wakiteketea kwa madawa ya kulevya.
ā€œ Hii yote ni nguvu kazi ya taifa inayopotea bure, laiti vijana hawa wangekuwa hawajajiingiza kwenye uraibu huu. Basi familia zao zingenufaika na nguvu zaoā€
Sajenti alijiwazia mwenyewe akiwa anatembea yapata mida ya saa tano usiku akiwa maeneo ya Uhasibu akirudi Ghetoni kwake. Magari yalikuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa. Mtu mmoja mmoja ndiye aliyekuwa anaonekana akitembea, Ghafla bin vuu Sajenti alishtuka kuona kundi la vijana wapatao saba wakiwa wamesimama mbele yake. Walikuwa vibaka, mateja wa Temeke ambao kundi lao waliliita CHURA MAJI YA MOTO. Vijana hawa walikuwa ni moja ya makundi tishio katika jiji la Dar es salaam. Walijulikana kwa uporaji, ubakaji, uvunjaji na hata mara nyingine walikuwa wakisababisha mauaji kwa watu walioonekana wabishi wakiwapora.
Leo walikutana na Sajenti, mtu hatari mwenye rekodi chafu ya mauaji, komando mwenye mafunzo ya kiwango cha juu ngazi ya kimataifa. Hawakujua mtu waliyemtaitisha, lati wangemjua huenda wasingethubutu hata kupita njia hiyo achilia mbali kumsimamisha. Walifanana kama kikundi cha mbwa mbele ya simba dume lenye hasira ya kupokonywa ufalme.
ā€œ Oyaaa! Toa kila kitu ulichonacho jombaa!ā€ kiongozi wa wale vijana alimuamrisha Sajenti.
ā€œ Salama wakubwa, uungwana ni kupeana salama kwanzaā€ Sajenti alisema akiwa anajiandaa kuwakabili.
ā€œ Hizo sisi hazituhusu, tunachotaka ni pesa. Toa pesa, simu weka chini haraka, vinginevyo tukugeuze mishikakiā€ Kiongozi wao aliongea wakati tayari wamemzunguka na kumkaribia wakiwa wameshika silaha za jadi.
ā€œ Sina chochote wakubwaā€¦.ā€

ā€œ wee fala nini..! Huna chochote nini kimekufanya utembee sasa hivi, hatutaki kujua umetoka wapi, tunachotaka ni pesaā€ kijana mmoja aliongea akiwa amemchapa kirungu cha mgongo.
Sajenti hakutaka kupoteza muda, alianza na Yule aliyempiga kirungu aliyekuwa upande wa nyuma yake. Alimrushia teke kwa upesi usiotarajiwa, teke likampiga kwenye shingo Yule kijana akadondoka chini. Walishikwa na butwaa na kabla akili yao haijakaa sawa Sajenti alimrukia kiongozi wa wale vijana teke la kifua akadondoka chini, hapo kizaazaa kikaanza. Moto ukalipuka. Sajenti alikuwa amechochea kuni kwenye tanuru la moto. Wale vijana walimfuata na kumshambulia kwa pamoja wakiwa na silaha zao za jadi. Sajenti kwa nguvu aliwapangua, na kuwaangusha wote chini.
Jambo moja nisisahau kulieleza ni hili; Vijana wale wengi wao walikuwa ni mateja, Afya mgogoro. Walikuwa na miili dhaifu ambayo kwa macho tuu walionekana ni watu wasiopata milo mitatu kwa siku. Hii ilifanya wawe na miili dhoofu na ngozi zilizofubaa. Walikuwa wana kila dalili za hali ngumu ya maisha, mafukara wasiohitaji kujitambulisha.
Hiyo ndio sababu ya Sajenti kuwashinda nguvu, Sajenti aliwapiga mpaka wengine wakakimbia huku wengine wakiwa wamezirai pale chini, mmoja ndiye alikuwa yupo mikononi mwa Sajenti. Sajenti alimchukua.
ā€œ Nisamehe Mjeda, nikaushie brother. Tafadhali Broo!ā€ Yule kijana aliyebebwa na Sajenti aliongea kwa sauti ya kuonewa huruma lakini Sajenti alimchapa kofi zito la uso kisha akafoka;
ā€œ Kelele..! Ukisema tena natoa roho yakoā€
Hapo kijana akashika adabu huku akishika uso wake wenye maumivu ya kibao alichopigwa na Sajenti. Kibao kile kilikuwa kizito mno, pengine hicho ndicho kilimfanya aielewe kauli ya Sajenti kuwa aache kelele vinginevyo atatolewa roho yake. Sajenti alimchukua Yule kijana mpaka kwenye chumba alichokuwa amepanga, akaingia naye ndani. Kisha akainama uvunguni mwa kitanda akatoa maembe mawili, akampa embe moja Yule kijana, na wote wakaanza kula maembe.

ā€œSitaki kukudhuru, wala sijapenda kukupiga lakini sikuwa na njia nyingine kutokana na uovu wenu. Naitwa Peter Mirambo, ukipenda niite PM. Wewe waitwa nani rafiki?ā€ Sajenti alifukuza ukimya wa kile chumba akamuuliza swali Yule kijana.
ā€œ Naitwa Feisal Athumani Alimaarufu kama Osama, sina jina jingine Brooā€ Kijana alijitambulisha mara hii hofu ikiwa imepungua.
ā€œ Vizuri. Umefikaje hapa ukaweza kuwa kibaka, hujui huo ni uhalifu Osama? Huogopi kukamatwa na vyombo vya dola?ā€ Sajenti aliuliza.
ā€œ Vyombo vya Dola..! Hahahaa! Broo unachekesha, vyombo vya dola ningeviogopa kama kusingekuwa na Rushwa.ā€ Osama alijibu akiwa ananyonya kokwa la embe alilopewa na Sajenti.
ā€œ Kwa hiyo wewe huogopi kabisa polisi?ā€
ā€œ Mbona huamini kama siviogopi, au broo wewe ni polisi?ā€ Osama aliuliza hofu ikiwa imeshika uso wake.
ā€œ Hapana, ila nimeshangazwa na maelezo yako,..ā€ Sajenti aliongea lakini akakatishwa;
ā€œ Sisi vibaka hofu yetu ni kuuawa na raia lakini kuhusu polisi kwa kweli hatuogopi hata kidogo. Nimeshaingia sero mara kibao na kutoka nikiwa na kosa la ukabaji, wizi na uvunjajiā€ Osama aliongea kama mtu anayejisifu huku akimtazama Sajenti kama mtu aliyekuja mjini siku ile asiyejua mambo ya mjini.
ā€œKwa nini hamuwaogopi polisi wakati nyie ni wahalifu? ā€œ Sajenti aliuliza kwa msisitizo.
ā€œ Broo PM, nikujibuje uelewe.. Nimekuambia Rushwa ndio mbeleko yetu. Siku Rushwa ikitoweka nasi tutawahofia polisi. Mimi hata sasa hivi unikamate na kunipeleka polisi, nakuhakikishia kesi haitofika mahakamani, tutahonga polisi na nitaachiwa. Mara ngapi nimefanya hayoā€ Osama aliongea muda huu akitoa maelezo yaliyomfanya sajenti aridhike.
ā€œ Haya nimekuelewa, hujanijibu swali la piliā€
ā€œ lipi tena, kwani uliniuliza mangapi?ā€
ā€œNilikuuliza imekuwaje mpaka unaishi maisha haya ya uhalifu? Umekumbuka sasa?ā€ Sajenti alimuuliza Osama akiwa anaosha mikono yake baada ya kumaliza kula embe.

ā€œ Nimekumbuka. Broo.. Tamaa mbaya. Kupenda mambo ya mkato ndio kuliko nifikisha hapa. Kama sio kupenda mkato huenda leo nisingekuwa hapa. Ningekuwa mtu msomi ninayeheshimiwaā€ Hapo akatoa sigara yake iliyokuwa mfukoni, ilikuwa imevunjika, nadhani ni kutokana na mbilinge mbilienge ya kupigwa mabuti na Sajenti muda ule.
ā€œ Unaniruhusu niwashe na kuvuta..ā€ Akamuuliza Sajenti;
ā€œ Hamna shida, endelea; tamaa ilikufanyaje mpaka leo hii umekuwa mhalifu?ā€
ā€œ Tamaa ya kuwa na maisha mazuri iliniingia nilipofika kidato cha pili, nilipokuwa nasoma shule ya sekondari Mugabe pale Sinza. Rafiki zangu niliokuwa natembea nao ndio walionishawishi kuingia kwenye uuzaji wa madawa ya kulevya. Wao walikuwa wakivaa nguo nzuri, viatu vizuri pia walikuwa na simu nzuri mno za bei ya juu, mwanzoni nilikataa kwani nilijua kujiingiza katika biashara hiyo ni kuhatarisha maisha yangu. Lakini rafiki zangu waliniwekea vikwazo mno, hawakutaka tena kunilipia pesa za chai na chapati, wala hawakutaka kunipa pesa ya chakula cha mchana..ā€
ā€œ Kwani hukuwa unapewa pesa na wazazi wako?ā€ Sajenti alimkatisha Osama kwa swali.
ā€œMama alikuwa ananipa pesa ya nauli tuu, shilingi mia nne. Mia mbili kwenda, mia mbili kurudi. Kwetu tulikuwa masikini. Mama yangu alikuwa anatembeza mchicha, kipato hakikuwa kinamkidhi. Najua unafikiria habari za Baba yangu, sikulelewa na Baba. Mara ya mwisho kumuona Baba nilikuwa na miaka sita, Mama alinambia alienda South Afrika kutafuta maishaā€ Osama aliongea kama mtu mahiri sasa wa kusimulia stori. Alikuwa ametulia uso wake ukikumbuka mengi sana. Sajenti naye alijikausha akimsikiliza ungedhani anasikiliza mahubiri ya siku za mwisho.

ā€œ Basi ningefanya nini, nikajiunga na rafiki yangu ambaye kwa sasa nasikia yupo kwenye Meli ya Ambagon..ā€
ā€œ Meli ya Ambagonā€¦?ā€ Sajenti alishtuka kusikia habari za Meli ya Ambagon. Alipoteza umakini na kujikuta akihamaki kwa sauti kubwa. Ni kama alisikia jambo kubwa linalotisha. Hakutegemea kabisa kama angesikia habari za Meli ya Ambagon kutoka kwa Osama. Sasa akajua Osama atakuwa na taarifa nyingi za siri ambazo alikuwa akizitafuta kwa muda mrefu.
ā€œ Mbona umeshtuka unaifahamu Meli hiyo?ā€ Osama aliuliza baada ya kumuona Sajenti akiwa ameshtuka.

ITAENDELEA.....

Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.

Kitabu Tsh 15,000


0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel

0758216209
M-PESA
Robert Robert Ng'apos Heriel
 
WAKALA WA SIRI 12
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300

ILIPOISHIA
ā€œ Meli ya Ambagonā€¦?ā€ Sajenti alishtuka kusikia habari za Meli ya Ambagon. Alipoteza umakini na kujikuta akihamaki kwa sauti kubwa. Ni kama alisikia jambo kubwa linalotisha. Hakutegemea kabisa kama angesikia habari za Meli ya Ambagon kutoka kwa Osama. Sasa akajua Osama atakuwa na taarifa nyingi za siri ambazo alikuwa akizitafuta kwa muda mrefu.

INAENDELEA

ā€œ Mbona umeshtuka unaifahamu Meli hiyo?ā€ Osama aliuliza baada ya kumuona Sajenti akiwa ameshtuka.
ā€œ Hapana Dogo, eehe! Endelea, huyo rafiki yako anaitwa nani?ā€
ā€œ Omary Saidiā€ Osama alijibu,
Moyo wa Sajenti ukapiga paa! Alimkumbuka Omary aliyekutana naye ndani ya Meli ya Ambagon. Sasa hapo akajihakikishia kuwa maneno ya Osama yalikuwa ni kweli kabisa. Hapo akataka kujua zaidi, aliona kuna kitu anaweza kukipata kutoka kwa Osama.
Osama akaendelea kusimulia;
ā€œ Mama yake Omari alikuwa ni konda wa Mbagala kwenda Makumbusho, alikuwa ni rafiki yake mama yangu. Urafiki wa Mama zetu ndio ulitufanya mimi na Omary tuwe marafiki, tena ndugu. Omary akanipeleka kwenye vilinge vya madawa ya kulevya, huko wanapouzia na wanapovutia. Basi nikapewa elimu ya biashara hiyo hatari. Mimi nilianzia kuwa msambazaji wa dawa za kulevya palepale mtaa wa Tandale, bahati nzuri mji wa Dar nilikuwa naufahamu vizuri. Hivyo mitaa yote yenye wateja wetu nilikuwa nasambazaā€ Hapo akameza mate huku akiwafukuza mbu waliokuwa wanamngā€™ata miguuni.
ā€œ Nami nilianza kupata vijisenti ambavyo vilinisaidia shuleni na pale nyumbani. Hiyo ikanifanya niingie rasmi na kuongeza juhudi ya uuzaji wa madawa ya kulevya. Pengine ungetaka kujua ni aina ipi ya madawa nilikuwa nauza, nilikuwa nauza Cocaine na heroine, Bangi na mirungiā€
ā€œ Samahani kwa kukukatisha, hukuweza kutambua madawa hayo yanatoka wapi, na mpaka yanafika kwako yamepitia wapi?ā€ Sajenti aliuliza.
ā€œ Cocaine na heroine nilisikia zinatoka Mexico, na Brazil huko, alinambia Omary kuwa, kwenye ile meli ya Ambagon. Lakini Mirungi na Bangi nyingi huzalishiwa hapahapa nchini. Cocaine na Heroine huingia nchini kwa njia tatu, Viwanja vya ndege, bandari bubu, na njia ya magari. Mara nyingi hupenda kutumia njia ya magari na bandari Bubu kwani huku hakuna ukakuguzi mkubwa tofauti na kwenye viwanja vya ndege. Madereva wengi wa malori ndio hutumiwa zaidi, hawa wanaotoka nchi moja kwenda nchi nyingine. Pia baadhi ya misafarsa ya vongozi wakubwa wa kitaifa hutumiwa kama fursa na baadhi ya viongozi wasiowaaminifu. Wasanii wakubwa baadhi yao husafirisha madawa kwa kumeza, wengine huagizwa na viongozi wa nchi. Unakuta msanii mkubwa kutoka marekani anakuja hapa nchini kufanya tamasha la burudani lakini nyuma yake kaja na mzigo wa maanaā€ Osama alimeza mate, Sajenti alikuwa anamsikiliza kwa umakini mkubwa sana. Ilikuwa simulizi ambayo Kwa Sajenti ilikuwa na msaada kwa sehemu kubwa kutokana na kazi yake ya upelelezi.
ā€œ Pia wachungaji wakubwa baadhi yao ni wauzaji wazuri wa dawa za kulenya, Kupitia mikutano yao kimataifa husafirisha madawa hayo kutoka nchi moja kwenda nchi nyingineā€
ā€œAisee! Mabona unajua mambo mengi na makubwa kiasi hicho, ehee! Inakufikiaje wewe?ā€ Sajenti aliongea akiwa amemkatisha Osama.

ā€œ Mimi mzigo nauchukulia kwenye vilinge vya madawa ya kulevya, hapo ndio sokoni. Unaweza kwenda kuuza au kununua. Unaweza kwenda ukakuta kilinge hakina mzigo ukauza, au ukaenda kununua mzigo na kwenda kuuza sehemu nyingineā€ Osama alijibu kisha akamtazama Sajenti kama mtu anayemwambia aulize swali jingine.
ā€œ Masoko ya mitumba ya nguo yanafahamika, mbogamboga tunayajua, sasa mtu atajuaje kuwa hili ni soko la Madawa ya kulevya?ā€ Sajenti aliuliza kama mwanafunzi mwenye nidhamu.
ā€œ Vizuri. Kuna ishara kadhaa huwekwa na wauzaji na watumiaji wa madawa ya kulevya. Ishara ya kwanza ni kuningā€™niza viatu juu ya waya za nguzo za umeme. Uliwahi kuona viatu vilivyoningā€™inizwa juu ya waya za nguzo za umeme Broo?ā€ Osama alimuulzia Sajenti.
ā€œ Ndio Osama, nimewahi kuonaā€
ā€œUlijiuliza inamaana gani?ā€ Osama alimuuliza akitabasamu.
ā€œ Kwa kweli naonaga, ila sijawahi kujiuliza, mimi najua ni wahuni tuu ndio hufanya hivyo, kumbe ni ishara!ā€
ā€œ Hiyo ni ishara ya kuwa eneo hilo ni soko la madawa ya kulevyaā€
ā€œLooh! Sikuwahi kufikiri hata kidogo..ā€ Sajenti alizungumza akiwa ameshangazwa na ishara hiyo ya soko la madawa ya kulevya.
ā€œ Basi ipo hivyo. Sehemu nyingi zenye ishara hiyo ni masoko ya madawa ya kulevya. Japo sio kila sehemu kutokana na kuwa wengine hurusha viatu juu ya nyaya za nguzo za umeme bila ya kujua maana yake. Ila tambua sehemu nyingi humaanisha ni masoko ya madawa ya kulevyaā€ Hapo akanyamaza akajilaza akilalia mgongo. Kisha akaendelea;
ā€œ Ishara ya pili, majengo yenye michoro na maandishi yakihuni, michoro hii huwa kwenye kuta na majengo yasiyokaliwa na watu, majengo ambayo hayajaisha, hapa huwa ni soko la watumiaji asilimia kubwaā€ Osama aliongea muda huu akipiga miayo, alikuwa amechoka yapata saa nane za usiku.
Sajenti baada ya kutosheka na maelezo ya Osama alimruhusu akaondoka, akabaki akitafakari mambo yote aliyokuwa amesimuliwa na Osama. Yalikuwa mambo mazito sana ambayo hakutegemea kama angeyasikia, Kilichomshtusha zaidi ni kusikia habari za Omary, hakutegemea kabisa kwamba siku moja angekutana na mtu anayemfahamu Omary kwa undani kabisa.
********************

Upepo wenye ubaridi ulimpiga kwenye kifua wakati akiwa anaendesha pikipiki, bado giza lilikuwa limefunika dunia huku nyota zikiwa zimepamba anga, hiyo ilikuwa saa tisa na nusu za usiku wakati Sajenti Warioba akiwa juu ya pikipiki akiwa maeneo ya Kongowe akielekea Mwembe Mtengu. Alikatisha kushoto barabara ielekeayo Kigamboni ambapo ndipo Mwembe Mtengu ilipo.
Hiyo ilikuwa ni mara yake ya pili kupita katika barabara hiyo, mara ya kwanza ilikuwa kipindi kile akiwa anamfukuzia Yule mtu mweusi kama msudani aliyekuwa ndani ya gari aina ya Subaru. Ni miaka mitatu imepita tangu apite barabara hiyo, mazingira kwa sehemu kubwa yalikuwa yamebadilika, na hicho ndicho kilimfanya aendeshe pikipiki kwa mashaka ya kupotea, alihisi amepasahau lakini alipofika eneo linaloitwa Twangoma alikumbuka kuwa bado alikuwa hajapapita Mwembe Mtengu.
Hatimaye alifika Mwembe Mtengu, kisha akakata upande wa kulia, moyo wake ulilipuka baada ya kuona jumba kubwa lenye geti jeusi. Alilikumbuka jumba lile ambalo miaka mitatu iliyopita almanusura lingeondoa roho yake. Alipunguza mwendo kisha akasimamisha pikipiki mahali ambapo anakumbuka Kijana Joseph alipigwa risasi. Sasa alikumbuka kila kitu baada ya kushuka na kuchukua udongo pale chini mahali alipopigiwa Joseph risasi. Alikumbuka maneno aliyoambiwa na Joseph; Mtafute BLM umuue. Maneno hayo ndiyo yalimkumbusha maneno ya Nasoro aliyemuua kwenye ndege iliyotekwa na Kundi baya la Ambagon.

Sajenti akaamka, kisha akaikokota pikipiki yake bila kuiwasha na kuificha kwenye moja ya vichaka vilivyokuwa karibu na lile jumba ambalo lilikuwa na uzio. Sasa kazi ilikuwa imeanza, kwa wepesi bila kesi akaurukia ukuta kama paka asiye na shaka, Tayari alikuwa juu ya ukuta mrefu ambao juu yake ulikuwa na nyaya za umeme, akachungulia kwa ndani akaona mazingira yalikuwa yaleyale isipokuwa kulikuwa ongezeko la magari manne. Moja lilikuwa Toyota Pick Up, Land Cruiser Mkonga V8, Pajero na RAUM ya rangi ya samawati. Taa za nje zilikuwa zinawaka kama kawaida.
Kwa ndani vyumba vya chini vyote vilikuwa na giza isipokuwa sebuleni ambapo kulikuwa na mwanga wa taa huku mapazi marefu yakiwa dirishani yaliyomfanya Sajenti asione chochote sebuleni. Sajenti bado alikuwa juu ya Ukuta akidadisi eneo la ndani la jumba lile. Kwa upande wa ghorofani vyumba vyote vilikuwa vinawaka taa kwa ndani isipokuwa chumba kimoja ambacho kilikuwa na giza. Sajenti alishuka taratibu kwa adabu isiyo ya adhabu mpaka chini asitoe mshindo.
Alinyata mithili ya paka aviziapo panya, akaende kuchungulia kwenye dirisha la sebuleni lakini hakufanikiwa kuona chochote kutokana na pazia kuziba dirisha lote, tena dirisha lilikuwa la grili lenye vioo. Sajenti aliutazama Mlango wa kuingilia sebuleni ambao ulikuwa chini ya kinoki alafu kulikuwa na taa. Alihofia jambo moja, nalo ni uwepo wa kamera au vifaa vya kunasia sauti au mienendo ya mtu atakayekaribia mlango ule. Alikagua eneo la Kinoki na kwenye ile taa akiwa amesimama karibu na dirisha kwa nje, macho yake ya udadisi yaliukagua mlango, hapo akajiridhisha kuwa hakuna kamera yoyote iliyokuwa imetegwa.

Sasa alikuwa amefika kwenye mlango wa sebuleni, akachungulia kwenye kitundu cha kitasa, hapo macho yake yakaona masofa meusi, akapeleka macho upande wa pili, akashtuka kumuona mzee mmoja mwenye ndefu nyingi akiwa amesinzia akiwa kakaa chini kwenye kapeti huku ameegemea sofa, aligundua mzee Yule alikuwa amelewa pombe baada ya kuona glass na chupa ya bia ikiwa pembeni yake. Sajenti alikitekenya kitasa cha mlango kuona kama mlango utafunguka, kwa mshangao asioutarajia, mlango ulifunguka kumbe ulikuwa wazi. Hapo akafungua mlango nusu akiwa kaingiza kichwa ndani akichungulia huku akihofia isijekuwa ulikuwa mtego kwake. Polepole akaingia akinyata huku uso wake ukikagua sebule ile. Haikuwa na mabadiliko makubwa, luninga ilikuwa ni ileile, masofa yaleyale, kabati pamoja na jokofu kubwa, kilichokuwa kimebadilika ni zulia ambalo lilikuwa la manyoya lenye rangi nyeusi na nyeupe.
Alipanda ghorofa ya pili akiwa kashika bastola yake mkononi, alipofika juu ghafla akasimama baada ya kusikia sauti ya watu wakizungumza. Alitulia kisha akasikiliza;
ā€œ Haiwezekani mpaka sasa hivi hatujaipata Chipu ya Darubini, mwezi sasa umeisha bado mnahangaika bila mafanikio yoyote. Ingekuwa bora kama mngekosa hizi sampo na Cadava kuliko kukosa chipu ya darubini ya hospitaliniā€ Maneno hayo yalimchanganya sana Sajenti akiwa kajificha kwenye korido pembeni ya mlango wa kuingilia kwenye chumba ambacho kulikuwa na kikao cha siri.

ITAENDELEA

Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.

Kitabu Tsh 15,000


0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel

0758216209
M-PESA
Robert Heriel
 
Nawashukuru wote mnaoendelea kunisapoti katika kazi yangu.

Kwa wale ambao mpo nje ya nchi, utaratibu wenu tunauandaa ili nanyi mjipatie kitabu hiki.

Kwa wapenzi wa Stori za Kichawi kazi nimewaandalia riwaya yenu iitwayo " MIMI NI MTOTO WA MSUKULE"
Kitabu hiko kimesimulia stori za kutisha na kusisimua za kichawi ambazo huenda hujawahi kuzisikia mahali popote pale.

Kwa Wapenzi wa Adventure Novels ipo Riwaya yenu iitwayo " SIKU YANGU YA KUFA ILIPITA" Ni simulizi ya ajabu mno ambayo itakufanya uburudike.

Mtachagua niilrtr ipi hapa JF Kati ya Riwaya hizo mbili.

Kwa wale ambao hamjapata nakala ya Riwaya ya Mlio wa Risasi Harusini, nawakumbusha tuu.

Ipo Ofa mpaka 14/10/2021 kitabu hiko kitauzwa kwa bei ya Tsh 10,000/= Tofauti na bei yake ya awali ambayo ni Tsh 15,000/=
zodo.jpg
zodo.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom