SoC04 Maonyesho ya Kijeshi yajikite zaidi kwenye kuonyesha uvumbuzi wa silaha na vifaa vya kivita

Tanzania Tuitakayo competition threads

1idea

Member
Aug 18, 2022
11
10
Imekuwa ni jambo la kawaida kila mara zifanyikapo sherehe za kitaifa (Sherehe za Uhuru, Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar) kuambatana na maonyesho ya kijeshi. Maonyesho haya yamekua yakionyesha mbinu kadha wa kadha wanazotumia wanajeshi wakiwa vitani. Ni jambo la kuvutia na kusisimua sana machoni kwa watazamaji hasa tuonapo wanajeshi na makomandoo wetu walivyo imara na shupavu kukabiliana na adui.

Umekua ni utamaduni mzuri sana wa kijeshi, lakini kuna vitu/ubunifu zaidi unakosekana kwenye maonyesho haya jambo ambalo limenipa shauku ya kuzungumzia upande wa sekta hii nyeti sana kwenye nchi yoyote duniani. Mambo yafuatayo yamenifanya bila hiyana kuweka kambi ya muda kwenye jambo hili.

Jambo kubwa kabisa ni kwamba dunia inabadilika
Kubadilika kwa dunia kunatokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia. Kama dunia inabadilika nasi pia inaidi tubadilike tusitegemee kuna siku mabadiliko yatarudi nyuma la hasha.

Tunashuhudia kwenye maonyesho mengi ya kijeshi nchini ni marudio ya mambo mengi yaliyowahi kufanyika nyuma. Matukio kama ya uokoaji wa mateka, utulizaji wa vurugu, kushuka kwenye ndege na kamba, kupigana, kulala juu ya misumari, kupasuliwa tofali kifuani, kupasua tofali kwa kichwa/ngumi na mengineyo mengi yamekua yakirudiwa mara kwa mara.
Hii inaashiria maonyesho haya yameegemea sana kwenye kuonyesha ukakamavu wa mwili na mbinu za kukabiliana na adui ana kwa ana kuliko uvumbuzi wa kijeshi uliofanyika.

Lakini zama zimebadilika, kipindi cha nyuma vita nyingi villikua vya kupigana ana kwa ana, zama hizi watu hawapigani tena ana kwa ana, nchi zinarushiana makombora bila ya wanajeshi kutoka nje ya mikapa ya nchi yao (mfano Iran walichofanya kwa Israeli). Kwa maana hiyo majeshi mengi yamewekeza kwenye teknolojia ili kuvumbua zana nzito za kivita na namna ya kujikinga na zana nyingine za kivita.

Jambo lingine ni kukosekana kwa maonyesho ya vifaa/silaha za kivita zilizoundwa na jeshi lenyewe.
Kwenye maonyesho mengi yaliyopita, vifaa na silaha zinazotumika kwenye maonyesho zinaonekana ni silaha kutoka nje. Bunduki,ndege na magari vyote ni kutoka nje, hii inaonyesha jinsi gani tulivyo nyuma kuitumia teknolojia kuvumbua na kutengeneza vyakwetu.
Kutokana na hayo basi tubadilike, tubadilike kwa kufanya nini? Tubadilike kwa kuendana na teknolojia, tupambane tusibaki sana nyuma, tupambane kuvumbua vyakwetu.

Tuanze kwa kuvumbua vya kwetu, tutakavyojivunia navyo. Maonyesho ya kijeshi yajikite kwenye kujivunia uvumbuzi wa kijeshi upande wa silaha na vifaa vya vita.

Sio lazima kuanzia mbali, bali ni vyema kuanza na chochote. Maonyesho haya yatufanye tuwe na shauku ya kuona maonyesho ya sasa wamevumbua/wametengeneza nini? Au wameboresha kitu gani walichovumbua kwenye maonyesho yaliyopita.

Jeshi linaweza likaanza kwa kutengeneza vitu vidogo kama bunduki, hata zisipokua na uwezo mkubwa watakapoendelea kufanyia marekebisho huenda zikawa na nguvu zaidi hata ya zilizopo na zinazotumika.

Jambo hili ni jambo linalowezekana kwakua tumeshuhudia kama sio kwa kusikia baadhi ya raia nchini waliokamatwa na bunduki(gobole) walizotengeneza kienyeji. Kama imewezekana kwa raia wa kawaida kutengeneza bunduki bila shaka itawezekana kwa wanajeshi kuziboresha na kuziongezea uwezo zaidi.

Pia jeshi la anga lijikite kwenye uundaji ndege zisizo na rubani (drones) zenye uwezo wa kubeba mizigo na makombora madogomadogo. Hizi ndizo silaha za kisasa zinazotumika miaka ya sasa, lakini pia ndege hizo zinauwezo wa kupeleka misaada ya chakula na silaha iwapo kuna waliozingirwa na adui bila kuhatarisha maisha ya watu wanaoziongoza.

Jeshi lijikite pia kwenye kuonyesha wanyama waliopewa mafunzo ya kijeshi na wenye uwezo wa kusaidia kwenye uwanja wa vita. Wanyama kama mbwa na panya ni miongoni mwa wanyama ambao ni rahisi sana kuelewa wanapopatiwa mafunzo na wataalamu.

Mfano mwepesi tu kupitia panya Magawa, ambaye alikua ni panya mbobezi kutoka tanzania mwenye uwezo wa kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini. Kutoakana na uwezo aliokua nao panya huyu aliweza kubaini mabomu mengi yaliyotegwa ardhini nchini Cambodia. Jambo hili lilimfanya atunukiwe medali ya dhahabu na shirika la matibabu ya wanyama la uingereza PSDA kwa kzi aliyoifanya. Hii inaonyesha ni kwa namna gani wanyama wakipatiwa mafunzo wanaweza kua na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na haraka kuliko hata mwanadamu na vifaa vyake.

Ingawa mwanzo ni mgumu, lakini ikiwekwa nia kwenye jambo hili huenda siku za mbeleni wanajeshi wetu wakawa na uwezo wa kuunda silaha nzito za kivita iwe ni bunduki, mabomu, makombora, magari, meli na hata ndege za kivita. Jambo ambalo litaipa heshima jeshi letu na kupunguza kutegemea silaha nyingi na vifaa kutoka nje.

Tukitazama nchi zenye nguvu kubwa kijeshi duniani, Marekani, Urusi na china zimewekeza zaidi kwenye kuvumbua na kuunda silaha zao wenyewe jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza nguvu zao kijeshi.

Kinachotakiwa ni serikali kuongeza bajeti kwenye sekta ya ulinzi. Na pia kusambaza wataalamu wa kijeshi kwenye nchi mbalimbali zenye uwezo mkubwa kijeshi kwa ajili ya kupata ujuzi. Hii itasaidia kupata ujuzi kutoka nchi mbalimbali na wataalamu hao watakapo ungana watajua wa pakuanzia.

Pia kuunda kamati tofauti tofauti za utafiti wa kijeshi, zitakazokua na wataalamu wabobezi. Hii itazisaidia kila kamati kujikita kwenye jambo lao moja, kulifanyia utafiti na kuja na uvumbuzi au maboresho kwenye jambo hilo.

Kwa kuhitimisha napenda niwapongeze jeshi kwa majukumu yao wanayofanya ya kulinda amani nchini na nchi jirani. Lakini kiujumla maoni haya ni kupenda kuona jeshi la Tanzania linafika mbali zaidi upande wa uvumbuzi na ubunifu wa vifaa vitumikavyo vitani ikiwemo silaha. Jeshi litakapoweza kujihudumia kwa baadhi ya silaha na vifaa itakua ni jambo la kufurahisha na kujivunia kwa nchi na pindi watakapowasilisha kwa raia kupitia maonyesho ya kitaifa.​
 
Unazungumzia kuunda kitu kipya au kukopi ?

Tanzania kuwa watu wenye wishful thinking, hakuna brains za kuunda au kubuni vitu vipya zaidi ya kukopi mambo waliyobuni wengine.
Kwa dunia ya sasaivi hakuna anayeunda kitu kipya, wote wanatengeneza na kuboresha vile vilivyoko. Ninachomaanisha tuanze walau kujitengenezea wenyewe vyakwetu ili siku zijazo tupunguze utegemezi wa kununua silaha na hivyo vifaa kutoka nje. Utakuta tu hata visu, kamba n.k vinavyotumiwa jeshini vinatoka nje.
 
Ubunifu na weredi uliopo sekta binafsi, ni mkubwa kuliko serikalini, mathalani, niliwahi, kufanya kqzi voda, tigo, Airtel, kule wahandisi, wanachapa kazi kwa weredi sana, kutatua changamoto za kila siku, pale ttcl,wafanye wasifanye,salary ipo tu, hata kampuni isipoingiza mapato, mishahara itatoka hazina!wakati kwenye sekta binafsi, kampuni isipopata mapato,hapo ni redundancy, hakuna bonus, nk,
Sasa may be jeshi lingekuwa binafsi, ubunifu ungekuwa mkubwa, kilicho pale jwtz,wakuu wote wanawaza jinsi ya kupiga maokoto kwa njia halari na haramu! Wizi tu, kukusanya ukwasi, architecture, majumba, nk, unakuta eti na mtoto wa mabeyo nae anakimbizna kutafuta ajira za takukuru! Kwanini asiwe na kampuni ya kuagiza siraha kwa, ajiri ya nchi za, Burundi, Rwanda, Zambia nk!
Kweli kabisa, watu wanabweteka kwakua wanajua malipo yapo tu.Inabidi kubalika na kuweka mikakati ambayo itasaidia kuongeza ufanisi kwenye sekta za serikali.
 
Kwa dunia ya sasaivi hakuna anayeunda kitu kipya, wote wanatengeneza na kuboresha vile vilivyoko. Ninachomaanisha tuanze walau kujitengenezea wenyewe vyakwetu ili siku zijazo tupunguze utegemezi wa kununua silaha na hivyo vifaa kutoka nje. Utakuta tu hata visu, kamba n.k vinavyotumiwa jeshini vinatoka nje.
Hizo akili za kujitengenezea vya kwenu au hata hiyo unayoita kuboresha nyie hamna, nyie cha msingi tafuteni hela nyingi mfanye importation na si zaidi ya hapo.
 
Hizo akili za kujitengenezea vya kwenu au hata hiyo unayoita kuboresha nyie hamna, nyie cha msingi tafuteni hela nyingi mfanye importation na si zaidi ya hapo.
Kama wewe hauna hiyo akili usione kwamba kila mtu hana, Mtaani tu watu hawana elimu lakini wanatengeneza magobole, hivi unafikiri wakipata elimu na vifaa hawataweza kutengeneza silaha nzuri zaidi?
Kilichopo ni watu kubweteka na kuridhika na walipo, Kuagiza nje utaagiza mpaka lini. Kama silaha zote unaagiza kutoka nje utawezaje kuwaaminisha watu kwamba una jeshi imara.

Zamani hizo tu, mababu zetu silaha zao walikua wanajitengenezea wenyewe alafu leo hii kila kitu tunaagiza kutoka nje.
 
Kama wewe hauna hiyo akili usione kwamba kila mtu hana, Mtaani tu watu hawana elimu lakini wanatengeneza magobole, hivi unafikiri wakipata elimu na vifaa hawataweza kutengeneza silaha nzuri zaidi?
Kilichopo ni watu kubweteka na kuridhika na walipo, Kuagiza nje utaagiza mpaka lini. Kama silaha zote unaagiza kutoka nje utawezaje kuwaaminisha watu kwamba una jeshi imara.

Zamani hizo tu, mababu zetu silaha zao walikua wanajitengenezea wenyewe alafu leo hii kila kitu tunaagiza kutoka nje.
Dunia ya leo unajisifia kutengeneza magobore, na nikisema hamna akili mnakuwa wabishi kama nungungu. Na hao waliosoma sijui mnaita wasomi ndio wanaongoza wizi, ufisadi na uviv

Wala usipoteze muda wako kuniandikia insha zako. Ukweli utabaki palepale wewe na hao jamaa zao hamna hizo akili za kuunda au hata kuboresha kilichoundwa na wengine, sana sana mna akili za uharibifu ndio maana kwenye ofisi zenu za umma yamejaa magari yasiyotumika na yanaweza kutumika huku pesa nyingi mkitumia kununua latest cars.
 
Back
Top Bottom