Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,588
- 1,190
Zaidi ya Bilioni 4 Kusambaza Maji Kata za Tegeruka na Mugango - Jimbo la Musoma Vijijini
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameelekeza ifikapo Februari, 2023 utekelezaji wa mradi wa kufikisha maji kwenye Kata za Mugango na Tegeruka Wilaya ya Musoma Vijijini uwe umeanza ili ifikapo Mwezi Juni, 2023 wananchi wawe wanapata maji.
Ametoa maelekezo kwa nyakati tofauti Januari 5, 2023 mbele ya Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kwenye mikutano ya hadhara na wananchi wa Kata hizo kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji Mkoani Mara ambazo ni Mamlaka ya Maji Musoma (MUWASA), Mamlaka ya Maji Mugango-Kiabakari-Butiama na RUWASA Mkoa wa Mara.
Amesema utekelezwaji wa mradi ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Mugango-Kiabakari-Butiama tarehe 6 Februari, 2022.
“Mtakumbuka Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dokta. Samia Suluhu Hassan alifika hapa na kutuwekea jiwe la msingi la mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 70.5. Katika mradi huo palikuwa na awamu mbili za utekelezaji lakini maelekezo yake yalikuwa ni kwamba mradi uwe na awamu moja badala ya kuwa na awamu mbili,” amesema Mhandisi Sanga.
Amebainisha kuwa ziara yake wilayani humo imelenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Mugango-Kiabakari-Butiama lakini pia kutoa maelekezo mbalimbali kuhusiana na maendeleo ya mradi sambamba na kuzungumza na wananchi wa Kata za Mugango na Tegaruka ili kuwafahamisha kuhusiana na neema inayokuja ya kufikishiwa huduma ya maji.
“Nimefika hapa kuzungumza na wananchi wa vijiji vyote vya Kata za Mugango na Tegeruka kuwafahamisha kuwa Mheshimiwa Rais Dokta. Samia Suluhu Hassan ametuongezea shilingi bilioni 4.775 kwaajili ya kuhakikisha mnapata huduma ya maji kupitia mradi huu mkubwa wa Mugango-Kiabakari-Butiama,” anabainisha Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga ameelekeza wataalam watakaosimamia utekelezaji wa mradi kuhakikisha ndani ya mwezi huu wa Januari, 2023 watafute wakandarasi wengine tofauti na huyo anayetekeleza mradi mkubwa ili ikifika mwezi Februari wasaini mikataba na kuanza utekelezaji lengo likiwa ni kwamba pindi mradi mkubwa unavyokamilika mwezi Juni, 2023 nao uwe umekamilika na wananchi wanapata huduma.
Amewaasa wananchi wa kata hizo kuepuka kusikiliza maneno ya mitaani yanayotolewa na wasiopenda maendeleo ya kwamba hawatopata maji. “Kumekuwa na wapotoshaji ambao wanakuelezeni kwamba mnadanganywa, niwahakikishie ndugu zangu Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan imejipambanua vyema katika kukabiliana na kero zinazowatatiza wananchi wake,” amebainisha Mhandisi Sanga.
Aidha, alimpongeza Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kwa ufuatiliaji wake wa mara kwa mara wa miradi ya maji na aliwaomba radhi wananchi wa Kata hizo kwa kuchelewa kuanza utekelezaji kwakuwa walikuwa wakisubiri ujenzi wa mradi mkubwa usogee ambao ndio chanzo cha maji cha mradi husika ili yote ikamilike kwa pamoja.
“Tulichelewa kuanza utekelezaji kwakuwa utatoa maji kwenye mradi mkubwa sasa endapo tungelaza tu mabomba yangelikuwa hayana maji lakini kwa sasa ni wakati muafaka tuanze ili mradi mkubwa unapokamilika hapo Juni na hapa tunakuwa tumekamilisha,” anafafanua Mhandisi Sanga.
Akizungumzia mradi wa Mugango-Kiabakari-Butiama, Mhandisi Sanga amesema maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee alipofanya ziara kwenye mradi Desemba, 2022 ndiyo maelekezo ya Wizara ya Maji.
“Mtakumbuka hivi karibuni Mkuu wa Mkoa alitembelea hapa na alitoa maelekeozo kwa wakandarasi na wasimamizi kwamba ifikapo tarehe 30 Juni, 2023 mradi uwe umekamilika na hakuna muda wa nyongeza nasi tunaungana na maelekezo yake na tunasisitiza aliyoyaelekeza yabaki vilevile ifikapo tarehe 30 mradi uwe umekamilika,” amesisitiza Mhandisi Sanga.
Kwa upande wake Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amesema ameshuhudia jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji za kumtua mama ndoo ya maji kichwani ambapo amebainisha kuwa vijiji vingi vilivyoko pembezoni mwa Ziwa Victoria tayari vinahuduma ya maji.
Amebainisha kuwa baadhi ya Kata jimboni mwake zikiwemo Kata ya Etaro, Nyegina, Ifulifu, Nyakatende watatumia maji kutoka Musoma mjini na jukumu hilo tayari Wizara ya Maji imelitolea maelekezo kwa MUWSA ya kuhakikisha vinafikishiwa huduma.
“Ninaendelea kuwathibitishia namna ambavyo Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inavyopenda jimbo la Musoma Vijijini, mwaka huu tunaouanza Serikali inazidi kuwekeza fedha nyingi ndani ya jimbo letu mbali na mradi wa mugango tumeletewa miradi mingine,” amesema Profesa Muhongo.
Amebainisha kuwa kwa Kata ya Mugango tayari kuna miradi miwili mmoja ikiwa ni huo aliyouzungumzia Mhandisi Sanga na kwamba kabla ya mradi huo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwapatia fedha kiasi cha shilingi Milioni 600 ambazo walizigawana na Butiama na kwamba zimewezesha maeneo mengi kupata huduma ya maji maeneo ya Kaburabura, Bugoji, Kanderema, Saragana, Nyambono na Mikuyu kufikishiwa huduma ya maji.
Imetolewa na Mwandishi wa Habari
Wizara ya Maji
5.1.2023