Waziri wa Nishati ya Madini, Profesa Sospeter Muhongo amepinga uamuzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutumia zaidi ya Sh15 milioni kununua transfoma katika kampuni binafsi badala ya kwenye Kiwanda cha Tanalec Limited ambacho shirika hilo lina hisa zake.
Profesa Muhongo alitoa uamuzi huo baada ya kutembelea kiwanda hicho jana akiongozana na maofisa wa Tanesco, Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) na maofisa wa wizara hiyo.
Katika ziara hiyo walibaini kuwa Tanesco hainunui transfoma katika kiwanda hicho.
“Kuacha kununua Transfoma Tanalec hakuna sababu nyingine zaidi ya rushwa na siyo kweli kuwa Sheria ya Manunuzi inawabana. Kama kweli inawazuia, suala hili nitalifikisha kwa Rais (John Magufuli) na katika ngazi nyingine za uamuzi,” alisema Profesa Muhongo.
Katika kiwanda hicho, Tanesco inamiliki asilimia 20 ya hisa, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) asilimia 10 na Kampuni ya Transcentury ya Kenya inamiliki asilimia 70.
Awali, kabla ya ubinafishaji Serikali ilikuwa ikimiliki asilimia 80 za hisa.
Kaimu Meneja Mwandamizi wa Manunuzi wa Tanesco, Jasson Katule alisema shirika hilo linashindwa kununua transfoma Tanalec kutokana na sheria kuwabana kwa kuwa inawalazimisha kutangaza zabuni.
Alisema katika zabuni, Tanalec ilishindwa na kampuni za Quality Group na Intertrade ya India.
Kampuni ya Quality Group itanunua transfoma za zaidi ya Dola 3 milioni za Marekani na Intertrade imeshinda zabuni ya Dola5 milioni za Marekani.
Awali, Meneja Mkuu wa Tanalec, Zahir Saleh alisema kiwanda hicho kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha transfoma 10,000, lakini kinazalisha 7,000 kutokana na udogo wake.
Pia, alisema wanakabiliwa na changamoto za kukosa soko la ndani huku wateja wakubwa yakiwa ni mashirika ya umeme ya Kenya, Uganda na Zambia.