Watoto wote wanaozaliwa Hospitali ya Bugando kupimwa usikivu

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,591
8,810
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) imeanzisha utaratibu wa kuwapima usikivu watoto wote wanaozaliwa hospitalini hapo kwa lengo la kubaini na kudhibiti tatizo la usikivu katika hatua ya awali.

Akizungumza leo Machi 3, 2023 wakati wa maadhimisho ya 'Siku ya Usikivu' duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Hospitalini ya Bugando, Mkurugenzi Mkuu wa (BMC), Dk Fabian Massaga amesema uamuzi huo umetokana na ongezeko la wagonjwa wenye tatizo la usikivu.

“Kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi 2022, Hospitali ya Bugando imepokea na kuhudumia wagonjwa 3, 463 wenye tatizo la usikuvu ambapo mwaka 2020 iliongoza kwa kuwa na wagonjwa 1, 635,” amesema Dk Massaga

Amesema idadi ya wagonjwa wenye matatizo ya usikivu ilipungua mwaka 2021 ambapo wagonjwa 858 walipokelewa kabla ya kiwango kuongezeka hadi kufikia wagonjwa 970 mwaka 2022.

Katika kuadhimisha siku ya usikivu duniani inayoadhimishwa Machi 3, kila mwaka, Hospitali ya Bugando imeendesha kampeni kuhamasisha umma kupima uwezo wa kusikia kwa kutoa huduma ya vipimo na tiba bila malipo kwa siku nne kuanzia Februari 28 ambapo jumla ya watu 107 walihudumiwa.

“Watu 70, sawa na asilimia 65.4 ya watu 107 waliohudumiwa kupiti kampeni yetu ya siku nne wamebainika kuwa na tatizo la usikivu na kupewa matibabu bila malipo,” amesema Dk Massaga

Daktari Bingwa wa Mfumo wa Usikivu na Uwiano kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI), Dk Godlove Mfuko ametaja hitilafu ya kimaumbile kwa watoto, maambukizi ikiwemo ya ugonjwa wa kaswende, ajali na kusikiliza sauti kubwa kwa muda mrefu kuwa miongoni mwa sababu kuu za tatizo la usikivu na kuwashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya kubaini matatizo na kupata tiba mapema.

"Ulevi pia huchangia tatizo la usikivu kwa muda kwa sababu pombe huathiri majimaji yaliyoko ndani ya sikio; hivyo unywaji wa pombe kupindukia unaweza kumsababishia mhusika tatizo la usikivu kwa muda," amesema Dk Mfuko

Irene Samwel, mkazi wa Bugarika jijini Mwanza aliyepata huduma ya vipimo na matibabu ya tatizo la usikivu bila malipo ameuomba uongozi wa Hospitali ya Bugando kusogeza huduma huduma hiyo hadi vijijini ambako wananchi wengi hawana uwezo wa kulipia gharama.

Mkazi wa Nyakato jijini Mwanza, Hilda Ladislaus ambaye mtoto wake mwenye umri wa miaka saba ametibiwa tatizo la usikivu ameushukuru uongozi wa BMC kwa kumrejeshea mwanaye uwezo wa kusikia bila malipo.

“Mwanzoni alipozaliwa, hatukufahamu kama mtoto ana tatizo la usikivu; lakini tulianza kuhisi ana tatizo hilo kutokana na kufanya jambo hata anapokatazwa na wakati mwingine akiitwa haitiki. Lakini baada ya vipimo na matibabu sasa anasikia na kutekeleza anachoelekezwa,” amesema Hilda

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom