Hali ya Sekta ya Afya hasa katika Afya ya Mama na Mtoto si ya kuridhisha nchini. Hii inaonekana katika takwimu mbalimbali za mwaka uliopita kama ifuatavyo:-
Wanawake wanaojifungua katika vituo vya kutoa huduma ya Afya wameongezeka kutoka 50% - 60%. Hii hairidhishi kwani ili hali iwe angalau nzuri inapaswa 80% au zaidi ya wanawake waweze kujifungua katika vituo vya kutoa huduma ya afya.
Vifo vya watoto wachanga vimeendelea kuwa pale pale kwani vimepungua kutoka vifo 26 hadi 25 kwa kila vizazi hai 1000. Hii inaashiria kuwa kazi bado ni kubwa katika kuhakikisha watoto wanazaliwa na kukua salama.
Vifo vya wajawazito vimeongezeka kutoka 454 hadi 556 kwa kila vizazi hai 100,000 ambayo ni sawa na vifo 30 kila siku au 11000 kila mwaka kulingana na takwimu za mwaka 2015/16.
Takwimu za ugonjwa wa fistula ya uzazi:
Zaidi ya wanawake Milioni 2 duniani wana fistula ya uzazi huku kukiwa na ongezeko la wagonjwa 50,000 hadi 100,000 kila mwaka ambapo 33,000 kati yao wanapatikana Kusini mwa jangwa la Sahara.
Nchini Tanzania kila mwaka kuna wagonjwa wapya takribani 3000 wa fistula. Kati ya hao ni 1500 hadi 2000 tu wanatibiwa kila mwaka huku nusu wakibaki hila matibabu.
Hadi mwaka 2014 kulikuwa na wagonjwa takribani 20,000 wa fistula nchini huku wengi wakiwa ni mabinti wadogo (Chini ya miaka 18).
Mbali na huduma ya matibabu kutolewa bure na wafadhili, serikali inapaswa kuweka nguvu zaidi katika kuzuia ongezeko la wagonjwa wa fistula kwa kuhakikisha huduma nzuri ya uzazi inafika hadi vijijini. Hii itasaidia kwa wanawake kuweza kupewa huduma stahiki kwa wakati na kuzuia fistula.