Baadhi ya Wafanyakazi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania( Bakwata) waliopo makao makuu Dar es salaam, wamelalamikia hatua ya kutolipwa kwa miezi minne, jambo linalowafanya waishi kwa shida
Mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, alisema kukosa mishahara yao kumewafanya waishi kwa kukopa na kujikuta wakidaiwa madeni mengi mitaani
"Tangu Julai mwaka jana hatujalipwa, tunaishi kwa kukopa. Hapa tulipo tuna madeni kila kona, hata futari kwa familia zetu hatuna", alisema
Alisema kuchelewa kulipwa mishahara yao kumewafanya waingie kwenye mfungo wa Ramadhani wakiwa katika hali ngumu
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka alisema suala hilo lipo chini ya ofisi ya Katibu Mkuu ambaye alishaanza kulifanyia kazi
"Tatizo hilo liko chini ya Katibu Mkuu, lakini lilikuwa linafanyiwa kazi na ninaamini kuwa kwa sasa litakuwa limetatuliwa", alisema Mataka
Lakini Mkurugenzi wa Habari wa Bakwata, Tabutabu Kawambwa alikanusha uwepo wa madai hayo na kusema kuwa hakuna mfanyakazi anadai mshahara, kwani wote walishalipwa tangu ulipoanza mfungo wa Ramadhani
"Hakuna mfanyakazi anayedai mshahara, wote wamelipwa walichokuwa wakidai ilikuwa ni posho ndogo ndogo na tayari wamelipwa", alisema Kawambwa
Alisema anaamini taarifa hizo zimetolewa na watu ambao wana nia ovu ya kulichafua baraza kutokana na kukosa madaraka, kwani wapo waliokuwa wakitarajia kupata vyeo ndani ya baraza hilo na sasa wamevikosa.
My take: Sasa mbona Mwenyekiti wa Bakwata amesema suala hilo linafanyiwa kazi. Na huyu Mkurugenzi anasema hakuna mfanyakazi kazi anayedai mshahara. Inamaana hakuna mawasiliano? Acheni mambo hayo, kama tatizo lipo ni vema likashughulikiwa
Chanzo: Mtanzania