Vikwazo vitatu vinavyokwamisha uchumi na maendeleo ya Tanzania

WilsonKaisary

JF-Expert Member
Apr 4, 2017
392
947
Kila nyakati katika historia inapita, Ina uthamani wake na ina utofauti wake. Nyakati moja inaweza ikawa ndio mwanzo katika mabadiliko kwa nyakati nyingine ya kibinadamu, kiutawala, kiuchumi, kisiasa na kijamii kama ilivyo tarehe 09/12/1961.

Leo sisi ni taifa huru kwa sababu waasisi wetu walifanya maamuzi sahihi ya kudai uhuru wa taifa letu katika nyakati hadi kufikia tarehe 09/12/196109/12/1961tukabidhiwa uhuru. Nyakati yao ndio ikaleta mabadiliko makubwa kisiasa ndio maana hadi kufikia leo tunajitawala.

Nyakati yetu tukifanya maamuzi sahihi na kuitumia vizuri inaweza ikawa mwanzo na msingi wa taifa hili kufika mbali kiuchumi, kidemokrasia, kisiasa, kielimu, kisayansi na kiteknolojia. Yote haya yanawezekana ila yanategemeana na maamuzi yetu ya sasa, maamuzi hayo ni usimikaji wa katiba mpya, usimikaji wa misingi na mifumo mipya ya elimu pia na usimikaji wa sera mama za uchumi zitazotambuliwa kikatiba na kila serikali iingiayo madarakani italazimika kuitekelezwa na ndio sera itayokuwa msingi wa sera nyingine za uchumi nchini.

Msingi wa kwanza kusimikwa upya ni katiba mpya, katiba ya sasa ilisimikwa tokana na mahitaji ya miaka ile ndio maana katiba imependekeza“…Mbunge ajue kusoma na kuandika…” ilikuwa sahihi sana kwa kipindi hicho maana wasomi walikuwa wachache lakini kwa sasa hivi au karne hii haina msingi tena hiyo sheria. Kwa karne yetu hata tukisema wabunge wawe na shahada au shahada mbili tutakuwa sahihi maana kuna wasomi wengi.

Tunahitajika kusimika katiba mpya itayoruhusu mihimili mitatu (bunge, serikali na mahakama) ya serikali kuu iwe huru na ifanye kazi bila kuingiliwa na mhimili mwingine kuanzia usimikwaji wa viongozi wake hadi utekelezaji wa majukumu ya kiserikali na sio kama ilivyo sasa mhimili serikali kupitia raisi unaweza teua viongozi wa mhimili bunge bila hata kushirikiana au kushauriana na wabunge.

Tunapaswa kusimika katiba mpya itayo mpunguzia raisi madaraka, na tusitarajie kuna serikali au raisi ita/ata kuja na atasema tuibadilishe katiba au nijipunguzie maadaraka kikatiba au nibadilishe sheria zinazonilinda mimi nikiwa raisi tusije tarajia kitu kama hicho. Sisi ndio wa kuibadilisha katiba na sio serikali.

Tunapaswa kusimika katiba itayozifanya tume na taasisi kama TAKUKURU, NEC, JESHI LA POLISI n.k ziwe huru ili ziweze kufanya kazi kwa weredi, viongozi wa taasisi hizo au tume hizo wanachaguliwa na raisi. Kweli TAKUKURU inaweza mchunguza raisi? Wakati mkurugenzi wake anateuliwa na raisi. Ni bora taasisi au tume hizi ziwe chini ya bunge au la sivyo zifanywe kuwa huru.

Hatuwezi kuendelea kwa kumtegemea kiongozi mmoja akuze wetu au atupeleke sehemu Fulani, maana hatujawahi kuwa taifa la kusema kiongozi au mtu Fulani atatufanyia jambo au tutatulia tatizo Fulani bali tumekuwa taifa la kusema wote tutafanya jambo Fulani na tutatua tatizo linalotukabili.

Tukisema tuendelee na dhana hiyo ya kusema tumtegemee kiongozi mmoja ndie arudishe nidhamu ya serikali au utendaji wa serikali au akuze uchumi wa taifa hatutofika popote maana awamu yake ikipita atakuja mwingine, kwa nini tusiunde katiba mpya itayoirejesha nidhamu ya serikali zetu au utendaji wa serikali kwa sheria zake? Na sheria hizi ndio zitazokuja kukuza uchumi wetu na zitadumu daima kuliko kumtegemea kiongozi Fulani ndio alete maendeleo au yeye ndio arejeshe nidhamu au utendaji wa serikali na vipi akiondoka? Nidhamu na utendaji wa serikali udolole kama awamu ya nne?

Katiba ndio msingi wa nchi na msingi ukiwa mmbovu manaake chochote kitachojengwa juu yake hakitodumu, katiba ndio dira na muongozo wa taifa kama katiba ni mbovu manaake taifa zima na serikali zake zitapoteza mwelekeo ndio hicho kinachotokea Tanzania.

Msingi wa pili ni elimu, elimu yetu ni duni na yenye madhaifu ya kila aina, tunatumia mitahara mibovu ya elimu ya kikale, mifumo duni ya kutolea elimu na miundo mbinu duni kwenye taasisi zetu za elimu.

Tunataka tusimike misingi mipya ya elimu itayo na sera zitayo mpatia mwalimu kipaumbele kuanzia mazingira yake ya kazi hadi mshahara wake hamna sababu ya kuwalipa mishahara mikubwa na marupu rupu mengi viongozi serikalini na kuwasahau walimu wanaozalisha viongozi hawa, mishahara ipunguzwe kwa viongozi hawa walimu waongezewe.

Leo Tanzania hatuna teknolojia za kwetu na kama zipo basi ni duni sio serikali au vyombo vya na taasisi za kiitelejensia tunategemea teknolojia za kigeni kwenye kutekeleza majukumu ya kitaifa kwa sababu ya uwepo wa elimu duni nchini.

Serikali za wenzetu zinawekeza pesa kwenye research wakiamini research ikikamilika itaweza kutumika kwa manufaa ya taifa na wanafanikiwa ila kwetu ni tofauti sana, leo Tanzania kuupata u-professa ni kuanzia miaka 55 miaka 5 mbele unapaswa kustaafu kisheria.

Mitahara yetu ya elimu na mifumo yetu ya elimu ina msomesha mwanafunzi masomo mengi mengine hayana tija tena haitambui kukuza vipaji vya wanafunzi wetu.

Leo tunaajiii wakufunzi wengi toka nje yote haya ni kwa sababu ya utoaji wa elimu duni hapa nchini.

Badala ya kujenga vyuo nchini na kuajili wakufunzi au walimu waje kufundisha katika vyuo hivyo ili tuzalishe wasomi wengi nchini sisi tunajua kupeleka watu wakasome nje ya nchi. Kwa nini tusijenge vyuo nchini na tuajii wakufunzi/ walimu waje kufundisha hapa nchini kuliko kupeleka wachache wakasome nje ya nchi?

Viongozi wetu watoapo hoja iwe bungeni au wapi tunashikwa na mashaka juu ya elimu zao, tunashindwa tuanzie wapi kuhoji elimu kwa sababu ya uduni wa katiba yetu pia ubovu wa elimu wetu unachangia kuzalisha viongozi wabovu sana wenye maono finyu.’

Swala ya kumsimika waziri mzawa wa elimu, sayansi na teknolojia ni swala lisilo na mantiki kwa taifa hili, tulipaswa waajiri wana taaluma au mawaziri waliostaafu katika nchi zilizo endelea (marekani,uingereza,urusi, ujerumani n.k) kielimu,kisayansi na kiteknolojia wao ndio wataweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye mitahara ya elimu,mifumo ya elimu na miundo mbinu za taasisi za elimu zetu. Waziri mzawa kasoma elimu hapa hapa, kweli tutarajie mabadiliko yote ya kielimu? Sana sana ni kupandisha pass mark, sasa sijui kama pass mark zinaboresha mitahara ya elimu yetu au mifumo yetu ya elimu?

Msingi wa tatu ni sera mama za uchumi, Tanzania hatuna sera hizi ndio maana kila serikali inakuja na sera zake za uchumi awamu iliyopita ilikuwa ni kilimo kwanza na awamu hii imekuja na sera ya uchumi wa viwanda. Tusimike sera mama za uchumi zitazo kuwa za kudumu na kutekelezwa kwa muda mrefu na zitakuwa msingi kwa sera nyingine za uchumi na kila serikali itapaswa kuitekeleza sera hii hata kama itakuja na sera yake.

Hakuna anaepingana na sera ya uchumi wa viwanda maana wote tunajua umuhimu wa viwanda kuwa tukiwa na viwanda vingi tutaweza zalisha ajira nyingi nchini na hata bei za bidhaa zetu nchini zitakuwa nafuu lakini hii sera itakelezwa kwa muda? Sawa ni miaka 10, awamu ya 6 nayo ikaja na sera yake. Je juhudi la kusaka wakezaji wa viwanda zitakuwepo tena kwa kiasi kile kile? Maana Sidhani kama kilimo ni kwanza kama ilivyokuwa kwenye serikali awamu ya nne ya kilimo kwanza.

Hatuna sheria na sera za kulinda fedha yetu, kukuza fedha yetu na kuitunza fedha yetu, kila mtanzania anaweza jitunzia fedha anavyotaka na kuikunja katika mikunjo yoyote anayotaka na wa kuweka popote ataweka hii yote ni kwa sababu hatuna sera za kulinda fedha yetu.

Leo nchini kuna manunuzi au malipo yanafanyika kwa pesa za kigeni, kwa nini yasifanyike kwa kwa fedha yetu? Serikali na wizara husika hamtambui ili? Tunashindwa kuipa kipaumbele fedha yetu.?

Ewe mjane na usie mjane, msichana au mwanamke mwenye ndoto ya kuolewa ipo siku nawe utakuwa mjane nawe uliye dhurumiwa/ utakuja dhurumiwa na ndugu wa mumeo wakidai mirathi ya mumeo ambalo ni jasho lenu wewe na watoto wenu, ndugu wa mume wanahusika vipi? Haya yote ni kwa sababu ya katiba duni ya sasa, tunapaswa kuunda sheria mpya za kuvunja tamaduni hizi.

Sasa mnaposema swala la katiba ni wazo la vyama pinzani sio sahihi, kwani hakuna wajane wafuasi wa C.C.M wamewahi dhurumiwa mirathi yao au hakuna wajane wafuasi wa vyama pinzani wamedhurumiwa mirathi yao? Na mtasemaje mchakato wa kuunda sheria au katiba mpya ni wa vyama pinzani tu?

Nani asiemjua Marijani Rajabu au Baraka Mwinsheshe au Remy Ongala au Tx Moshi au Steven Kanumba au Albert Mangwea? Hawa wasanii wote ni marehemu familia zao zinanufaika na nini? Zinanufaika na jasho lao au kazi? Hamna Haki miliki familia zao au watoto wao wataanzia wapi kudai? Kazi zao zinatumika hadi sasa, yote haya ni kwa sababu ya sheria zetu hazitambui Haki miliki ya msanii. Na wasanii msitarajie BASATA au SERIKALI itakuja wasimikia haki miliki wala kiongozi yoyote atasema asimike Haki miliki ili kazi zenu zitambulike kisheria.

Nanyi wasanii mnaamini usimikwaji wa sheria au katiba mpya nchini ni swala la vyama pinzani? Kwani hapa nchini hamna wasanii wafuasi wa CCM au wa vyama pinzani wamedhurumiwa kazi zao na kulanguliwa? Wakashindwa kudai kwa kukosa haki miliki, fungueni akili zenu la sivyo mtaendela kutumika kipindi cha uchaguzi wakishinda chaguzi zao wakiingia madarakani watawaambia msiimbe siasa, tumekuwa taifa la kumpangia msanii nini aimbe na nini asiimbe? Si kuingiliana katika haki ya kuongea na mawazo huko? Mchakato wa katiba mpya ni swala la kila mtanzania nchini wa kila dini, kila kabila, kila umri, jinsia zote na vyama vyote vya siasa.

Sidhani kama kuna mtanzania anapenda shuhudia mwanae imlazimu kuwa mfuasi wa chama tawala (C.CM) ndio atimize ndoto zake kisiasa kwa kuhofia akiwa mfuasi wa vyama pinzani atapozungumza ukweli juu ya serikali au ikosoa serikali atahesabika kama mchochezi au yeye na chama chake watazuiliwa kufanya maandano hata yakiwa ya amani jeshi la polisi litaingilia kati au akiwa kiongozi wa chama pinzani atapowasilisha hoja bungeni hata kama ina manufaa kwa nchi itapingwa tu sio kwa sababu hoja yake haina msingi na manufaa kwa serikali bali ni kwa sababu yeye ni mpinzani au atapokiuka agizo la serikali atashikwa na jeshi la polisi, maana nguvu ya dola imelalia upande mmoja.

Nguvu ya dola na mahakama imeshikilia na chama tawala na inatekeleza matakwa ya viongozi wa chama tawala wao kila kitu mpaka wapewe maagizo serikalini kwani hawajui kashfa za ufisadi kama Andrew Chenge, Anna Tibaijuka wamechukua hatua gani mpaka sasa? Mahakama imechukua hatua gani? Ila wangepewa maagizo serikalini wangekamatwa na kufunguliwa mashtaka bila aibu wamepewa nyadhifa serikalini, bungeni na ndani ya chama.

Fisadi ni fisadi akiwa chama tawala akija chama pinzani sio fisadi na wala hazungumziwi Edward Lowasa alihesebika fisadi alivyokuwa chama tawala alivyohammia chama pinzani akapewa na nafasi ya kugombea uraisi, bado unaamini katika maendeleo na mabadiliko kuletwa na vyama vya siasa? Ndani ya vyama vya siasa kuna kulindana sio chama tawala wala vyama pinzani. Akiwa ndani ya chama tawala sio fisadi ila vyama pinzani watamuona kama fisadi na mtu huyo akiamia chama pinzani sio fisadi tena ila chama tawala kitamuona fisadi kama vizuizi ataletewa na kuchunguzwa au kupokonywa mali zake….Fredrick Sumaye na Lazaro Nyarandu…

Maendeleo na mabadilko yanaletwa na wananchi wenyewe ingawa wananchi hao hao ndio wanaounda vyama vya siasa na inapofikia hatua siasa zetu haziaminiki au hatuamini vyama vyetu vya siasa inabidi tuchukue hatua sisi wenyewe, moja wa hatua hizi ni kupata katiba mpya yenye sheria mpya, sheria ni msumeno lakini msumeno wetu sisi ni butu kwa sasa.

Sheria zinatekelezwa mpaka Fulani atoe maagizo na zinafanya kazi kwa kuangalia kasi ya serikali iliyopo madarakani na vyombo vya kusimamia sheria vinafanya kazi kwa kuangilia huyu ni nani? Wa chama gani? Ana kipato gani? Na kama ndio hauna chochote ndio inafanya kazi pia na unaweza uziwa kesi ukiwa hauna kitu. Mpaka hapo manaake kuna wengine wapo juu ya sheria, kuna wengine wanaweza ipindisha sheria na kuna wengine wanaweza iamrisha sheria na pia kuna wengine wameishikilia sheria na kuna wengine wapo chini ya sheria ndio maana tunadai katiba mpya itayotufanya wote tuwe chini ya sheria uwe kiongozi, tajiri, maskini, uwe mwanamke au mwanamke wote tuwe chini ya sheria.

Hata serikali ya chama tawala iwe imefanya mazuri mangapi au kinaendesha serikali vizuri kiasi gani haimaanishe ndio kusiwe na vyama pinzani, kazi ya vyama vingi ni kuhakikisha kunakuwa mshindanisho ya hoja, sera na mitazamo ya kujenga taifa na chama kitachbainikika kuwa na sera nzuri, hoja nzuri na mitazamo mizuri ndio kitapigiwa kura na wengi. Vyama pinzani hawajui kusifia wala kuipongeza serikali ya chama tawala liwe zuri au baya wanakosoa, maana ya kuwa mpinzani sio kwamba hata mazuri we unakosoa tu.

Majimboni mkiwa na mbunge wa chama pinzani maendeleo yatacheleweshwa ili tu uchaguzi ujao angushwe jimboni, Siasa zetu bado ni duni yote haya yote ni kwa sababu ya katiba mbovu na sheria mbovu nchini na demokrasia yetu inakwamishwa na uduni wa katiba na sheria zetu za nchini huku vyombo vya kusimamia sheria vikichangia kwa kiasi kikubwa sana.

Pia sidhani kama ni sahihi sana kuwa shinikiza watoto wetu wote wasome masomo ya sayansi kwa sababu kwa sababu tupo kwenye utawala wa sera ya uchumi wa viwanda, wanafunzi wengi sio kwamba hawataki au hawawezi kusoma masomo ya sayansi bali wanaogopa juu ya miundo mbinu, mifumo na mitahara duni ya elimu na laiti kama kungekuwa na mazingira tusingekuwa na wakufunzi wachache wa masomo ya sayansi.

Nchini kuna mitahara mingi wa kufuata ya kihindi shuleni kwake atafuata na wakufuata wa Cambridge atafuata, kwa nini tusiwe na mtahara mmoja? Hawa wageni wanao kuja kwetu kufungua shule nchini wanafuata mitahara isiyo hapa nchini, mbona watanzania wakienda nchi zao wanasoma mitahara ya kwao? Kama wanakiri elimu yetu na mitahara yetu ni duni basi serikali kupitia wizara ya elimu,sayansi na teknolojia ikubali kushirikiana nao kwenye kuunda mitahara mipya ya elimu ili nchini kuwe na mtahara mmoja.

Lugha za kufundishia mashuleni ziko mbili, wanafunzi wa shule za kata shule ya msingi atafundishwa kwa Kiswahili na kiingereza litakuwa somo la ziada akienda sekondari atafundishiwa kwa kiingereza masomo yote na Kiswahili litakuwa somo za ziada na akienda chuo ni kiingereza pia huku mwanafunzi mwingine yeye kuanzia shule ya msingi hadi sekondari yeye anafundishiwa kiingereza na Kiswahili linakuwa somo la ziada akienda chuo tena ni kiingereza. Kuna haja ya kuwa na lugha mbili za kufundishia? Lugha inayotumika nje ya taasisi za elimu ni Kiswahili na Lugha ya taifa ni Kiswahili, nyaraka au shughuli za serikali za kimaandishi nyingi zina-andikwa kwa lugha ya kiingereza.

Hata tuseme “HAPA KAZI TU” mara ngapi au tufanye kazi masaa ngapi bila sheria za kazi au sera za kazi nchini ni bure, kama unaenda kwenye taasisi za serikali anaepaswa kukuhudumia yuko busy na simu yake au muda wa kazi hayupo bila sheria za kuwashtaki hatutafika popote. Na kwa uchache wa masaa ya kazi nchin nao hatuwezi kufika popote.

Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere aliacha viwanda vingapi? Na vingapi bado vinafanya kazi? Na kwa nini vimekufa? Vilishindwa kuendelea kwa ukosefu wa wakufunzi wa kuviendeleza viwanda, ukosefu wa sera nzuri za kuvilinda na kuvikuza viwanda hivi na ukosefu wa sheria nzuri za kuvilinda na kuvikuza viwanda hivyo. Ndio kama ilivyo sasa hata tujenge viwanda vingapi kama tukiendelea sheria duni, sera duni na elimu duni kama sasa vitakufa tu. Hamna sera za kuzuia uagizaji wa bidhaa (bidhaa zinazalishwa nchini ila kuna bidhaa kama hizo zinaagizwa kwa wingi kushinda hadi zile zinazozalishwa nchini) kwa nini viwanda visife? Hamna sheria za kushinikiza na kuwashitaki wataokiuka sera hizo, kwa nini viwanda visife?. Elimu duni haiwezi kuzalisha wasomi bora na wakufunzi wa kuviendeleza viwanda hivyo, kwa nini viwanda visife? Watanzania walio wengi hawana imani au elimu ya ubora wa bidhaa zetu za nchini na elimu ni duni (hawaja patiwa elimu hiyo), kwa nini viwanda visife?

Ndio maana tunataka kusimika misingi mipya ya kusaidia, kulinda, kuendeleza na kukuza kila kitu cha ndani, uwe utawala wetu au fedha yetu au uchumi wetu au elimu yetu ama demokrasia yetu tukisimika misingi hii mipya ya katiba mpya, sheria mpya, sera mpya na mifumo ya kisasa na mitahara mipya ya elimu yote hayo yatatimia.

Serikali ni watu tena wanachaguliwa na watu na ipo kwa ajili ya watu. Watu hao hao ndio binadamu na hakuna binadamu aliyekamilika manaake kama serikali ni binadamu manaake serikali inakosea na pale inapokosea inabidi kukukosolewa au kuhojiwa lakini katiba ya sasa haitoi hiyo haki au fursa. Leo tunashindwa mkosoa raisi na tunamuona Mungu mtu kwa sababu ya udhaifu wa katiba ya sasa ila tulipaswa mkosoa au mshauri ila uduni wa katiba yetu unachangia yote haya. Pia hata pale tunapokuwa na wasi wasi nae ilibidi tumchunguze lakini katiba hairuhusu.

Tulipaswa tuwe na taasisi huru za usalama na ki-intelejisia ambazo hazitokuwa chini ya serikali nazo zifanye kazi zao za uchunguzi lakini katiba ya sasa haitambui hilo.

Leo tunashindwa kuihoji au kuikosoa serikali kwenye mambo ya kitaifa kuanzia usalama wetu n.k lakini tokana na katiba mbovu tunashindwa kuanzia wapi maana hamna haki ya kutulinda kikatiba na kama ipo basi inakiuka, swala mtanzania mwenzetu kupigwa risasi kiongozi wa upinzani Tundu Lissu ni swala lilizua maswali mengine lakini hatujui wa kumuuliza nani na nani wa kutujibu .Ni nani aliyempiga risasi? Alimpiga kwa malengo au yapi au kumzima kisiasa? Na alitumwa na nani na ni nani huyo na ni wa chama gani? Waliofanya hivyo hukumu yao ni nini? Vyombo vya usalama vimefikia wapi katika uchunguzi huo?

Hawa wasiojulukana ni wakina nani? Nani anaewajua? Haturusiwe kufanya reasoning katiba yetu ya sasa haitoruhusu, tunashindwa kuhoji usalama wetu na watanzabia wenzetu wakina Ben Saa Nane na wengine.

Sisi bado ni taifa change duniani huu ni wakati wakuachana na mambo ya kitoto, tuchukue maamuzi ya kiutu uzima, tuwaze na kufikiri kama watu wazima na tuwe na mitazamo ya kiutu uzima.

Tukikubali kusimika sera mama za uchumi zitazo ruhusu wauzaji,wasambazaji na wazalishaji wa umeme wengine nchini na sio nchi nzima kutegemea shirika moja la umeme TANESCO hapo tutakuwa tumeamua kama watu wazima leo kuna huduma mbovu wa umeme, umeme unakatika bila fidia yoyote hata serikali itishie viongozi au wafanyakazi wa shirika hili bado haitasaidia lolote suluhishp hapa ni kuruhusu wawekezaji wengine wazalishe, wasambaze na kuuza umeme na ndipo tutapata kipimo bora cha huduma za TANESCO.

Watanzania wenzangu labda niwakumbushe kitu, safari ya 09/12/1965 haikuanza na Baba Hayati Mwalimu Nyerere ilianza na waasisi wengine huko kama wakina Kinjekitile Ngwale, Chief Mkwawa n.k hao wote walipigania uhuru wa mtu mweusi au uhuru wa taifa letu haid kufikia kizazi cha Baba Hayati Mwalimu Nyerere wao wakaja kumalizia kile kilichokuwa kimeanzishwa.Lakini hao waasisi nyuma ya Baba Hayati Mwalimu Nyerere walipigana na wakoloni sio kwa ajili yao tu bali kwa ajili yao na vizazi vingine.

Hata safari ya waisraeli haikuanza na Joshua ilianza na Musa ingawa Musa na kizazi chake ndio walionza safari hiyo ya kuelekea Nchi ya ahadi, kizazi cha Joshua walikuja kumalizia kile kilichokuwa kimeanzishwa na vizazi vya nyuma.

Hata sisi kizazi cha leo tunapaswa kuufanya mchakato huu sio kwa ajili yetu tu bali hata kwa vizazi vijavyo, maana ndio umekuwa utamaduni wetu. Baba Hayati Mwalimu Nyerere aliongoza jeshi letu kumshinda Idd Amin Dada baada ya kuona usalama wetu unaingiliwa na sehemu ya nchi yetu inataka chukuliwa. Kwa nini aliamua maamuzi magumu kama haya? Kwa nini asingetulia Idd Amin Dada achukue eneo letu? Na kwa nini asingewaacha watanzania wa mikoa ya kaskazini wapambane wenyewe?

Baba Hayati Mwalimu Nyerere alitambua dhahiri vizazi vijavyo vingekuja kumlaumu daima kwa kushindwa kuchukua hatua yoyote, hakuweza kumuachia Idd Amin Dada eneo letu la nchi maana alijua kuna vizazi vijavyo vinakuja na asingeweza kuwaachia watanzania wa mikoa ya kaskazini wapambane na hali zao maana nae alitambua hamna tatizo la mtanzania bali kuna tatizo la Tanzania nzima ndio maana hata wanajeshi walioenda kupigana na Idd Amin Dada hawakuwa ya mikoa ya kaskazini tu bali walikuwa katika kila sehemu,kabila, dini na watanzania wa kila aina ya hi nchi.

Na Baba Hayati Mwalimu Nyerere alimshinda Idd Amin Dada sio kwamba alikuwa na jeshi zuri au silaha za kisasa bali ni kwa sababu ya umoja wetu, utulivu wetu, ushirikiano wetu, nidhamu yetu kwa viongozi wetu na haswa pale inapofikia hatua kwenye kutatua maswala ya kitaifa.

Na sisi tunapaswa kuonyesha heshima, umoja wetu, ushirikiano wetu na nidhamu yetu kwenye Mchakato huu wa usimikaji kama walivyo-onyesha baba zetu, mama zetu, bibi zetu na babu zetu kipindi walipokuwa wanapigana na Idd Amin Dada.

Mchakato huu tusiukwamishe kwa mitazamo yetu ya dini au kisiasa au kabila zetu na tusikubali wataosema swala la katiba mpya ni wazo la vyama pinzani, kwani hii katiba ya sasa inawaumiza wafuasi vyama pinzani pekee yao? Kuna wajane, wasani na watanzania wa aina mbali wanaumia kwa ubovu wa katiba ya sasa na ni wafuasi wa vyama vyote, utasemaje swala la kusimika katiba mpya ni wazo la vyama pinzani?

Mchakato unawahusu watanzania wa makabila yote, jinsia zote, vyama vyote nchini hadi wasio na vyama, wanaomini katika siasa na wasioamini na wa dini zote hadi wasio na dini. Hakuna chama cha siasa au kiongozi kita/atasema leo tu/akubadilishie katiba wakati katiba ya sasa inawalinda wao wakiwa madarakani, tuna viongozi wengi nchini wasio na elimu na wengine elimu zao za kusuasua watakubali tusimike katiba mpya itayopendekeza “…kiongozi wa aina nchini awe na elimu kuanzia shahada na kuendelea…” hakuna kiongozi kama huyo.

Kwa kelele zote za vyama pinzani kutaka Edward Lowasa ajiuzulu akiwa waziri mkuu kwa kashfa za ufisadi ila kwa sasa wamempokea na kukaa kimya na kumfanya mgombea wao wa uraisi kweli bado unaamini katika vyama vya siasa? Fisadi ni fisadi akiwa chama tawala akija upinzani sio fisadi.

Mchakato huu kwa sasa tunaanzia mitandaoni tutajadiliana kwa hoja na kushindana kwa hoja na sio kwa mabavu au matusi kwa mtanzania asie na uelewa apewe elimu ya kutosha.

Yatupasa tusiogope vitisho vya aina yote yote yatupasa kuogopa uoga wenyewe kabla ya chochote. Najua tutapitia wakati mgumu mpaka mchakato huu ukamilike ila tusisahau waasisi wetu walipitia mengi magumu hadi kuusimika uhuru wa taifa hili wengine walichomwa, kunyongwa, kufanyia vitendo vya ukatili, kupigwa risasi na wengine walisurubiwa lakini hawakukata tamaa ndio maana leo sisi ni taifa huru, walijipa moyo ipo siku watakuwa huru hata kama sio wao basi vizazi vyao ambao ndio sisi leo tupo huru na hata kama ni uhuru wa bendera lakini waliijenga historia yao kwa namna yao.

Waasisi wetu walizuiliwa kufanya mijadala na maandamano ya kudai uhuru na wakoloni lakini hawakusita kufanya maandamano na mijadala hiyo maana ndio waliamini ndio njia pekee ya kuwafikia watanganyika walio wengi.

Na sisi yatupasa tufanye hivyo hivyo mijadala ya mitandaoni isio na kikomo tuifanye pasipo kuchoka huku tukisubiri watanzania wengi wapate uelewa wa kutosha.

Serikali itasema hatuna pesa za kutosha kufanya mabadiliko ya katiba, tusisite kuihoji nchini kuna wizara ngapi? Na kila wizara lazima iwe na waziri, naibu na katibu hawa wote wanatembelea magari ya kifahari. Tanzania kuna wakuu wa mikoa wangapi na wakuu wa wilaya wangapi? Hawa wote wanatembelea magari ya aina gani na ulaji wa mafuta ukoje? Kuna haja ya kuwa na matumizi kama haya kwa uchumi wetu huu? Au kuna siku serikali imeshindwa walipa wabunge posho zao? Au kuna siku gari la kiongozi yoyote limewahi kuishiwa mafuta na likahailisha safari zake?

Kwa nini serikali kwenye mambo ya msingi ndio iseme haina hela? Na kwenye matumizi yasio na maana serikali inagharamikia vizuri tu?

Ujumbe huu umfikie kila mtanzania wa kila aina na sisi tunamwambia “mabadiliko yanaenda kutokea nchini”, tukifanikisha mchakato huu hata vizazi vijavyo vitasema tuliikabali nyakati yetu na hata tusipomalizia kuutimiza mchakato huu basi watabakiwa na kazi ndogo sana.

Mwenyezi Mungu ndie muumba wa tawala zote duniani, tukimuita awe upande ni nani atakae-tudhuru au tutisha?

“…Nia tunayo, Nguvu tunayo na Uwezo tunao...” ni kauli iliyotamkwa na baba hayati Mwalimu Nyerere kipindi cha vita ya Idd Amin Dada.

Kauli hi naitamka tena baada ya Zaidi ya miaka 25 kutamkwa, Nia tunayo ya kusimika mifumo, mitahara na miundo mbinu ya kisasa, Nguvu tunayo ya kupata katiba mpya na uwezo tunao wa kusimika sera mama za uchumi.

Asili ya matatizo yetu ni ukosefu wa misingi thabiti ambayo ni katiba, elimu na sera mama za uchumi. Na haya matatizo sio matatizo ya chama cha kisiasa Fulani au chama pinzani bali haya ni matatizo ya watanzania wote. Na hatujagawanyika kama siasa zetu zinavyosema tumegawanyika, daima tutaendelea kuwa watanzania wa jamhuri ya muungano ya Tanzania.

Na tutakuwa taifa gani lenye uchumi mkubwa duniani? endapo tutakubali kusimika misingi hii mipya. Na tutakuwa taifa gani lenye demokrasia kubwa? kama tutakubali simika katiba mpya. Tutakuwa na elimu bora kiasi gani? kama tutakubali kubadili mitahara na mifumo yetu ya elimu

Mungu Ibariki Tanzania na Mungu Ibarikia Afrika.
 
Back
Top Bottom