Umejipambanua kuwa ni mtu tofauti kimaneno na kimatendo. Umekuwa ukisema ukweli na kufuatilia jambo kwa makini, undani na kwa dhati ya moyo wako. Tumekuwa tukikuzongazonga tu kwa manenomaneno pale ambapo unasema 'zaidi' ya yale ya kuyasema.
Hata wewe Rais unajua kuwa CCM ni chama chenye makandokando mengi. Kwakuwa chama ni wanachama, CCM haijawahi kukwepa kashfa zote za kifisadi tabgu kuanzishwa kwake hadi sasa. CCM inahusika na vyote ambavyo sasa unapambana navyo. Kila wakitajwa, ni makada.
Aliyekuwa Rais wa Malawi, Hayati Bingu wa Mutharika alitoa mpya kwa siasa za Afrika. Alichaguliwa Rais kupitia chama kiitwacho United Democratic Front mwaka 2004. Mwaka mmoja tu, mwaka 2005, Hayati Mutharika akaanzisha chama chake cha Democratic Progressive Party na akashinda uchaguzi kwa chama kipya.
Chema chajiuza! Hayati Bingu alihama kwakuwa mtangulizi wake katika Urais, Bakili Muluzi alikuwa akimuingilia katika utendaji wake kupitia uongozi wa Muluzi kwenye UDF. Mutharika alitaka kufanya mambo makubwa bila kuingiliwa.
Kutokana na 'kuchafuka' kwa kutosha na kutisha kwa CCM, nakushauri Rais Magufuli uunde chama chako na kuhama CCM. CCM inakugharimu katika kutenda kwako kwakuwa kila uchao utawakuta wale wale wakiwa wamefanya yale yale. Ndimo utakutana na watu kama Mtemi Chenge. CCM itakulazimu kuilinda.
Kuilinda CCM ni kulinda mabaya yake. Kuilinda CCM ni kupambana kimaneno na kimatendo na wakosoaji wake. Kuilinda CCM ni kuaminisha watu kuwa sasa CCM inajisafisha na 'inatubu' hata kama ni kwa tabu. CCM inakuchafua na inachefua. Walioaminiwa kichama na hata Bungeni ndiyo waliotufikisha hapa tulipo.
Jambo la busara na lisilo na hasara ni kuanzisha chama chako na kuhama CCM. Wazalendo wenzako tutakufuata huko. Tutakurejesha Ikulu kwa nguvu zaidi na ukiwa unajiamini zaidi kwakuwa hautakuwa na 'urafiki'. CCM, ilipofikia na vinavyoendelea, haisafishiki wala hailindiki. Hata overhaul ni kupoteza nguvu tu.
Hama CCM mzalendo, linda mali za Tanzania yetu!
Mzee Tupatupa wa Lumumba, Dar es Salaam