KATIKA kuitikia wito wa Serikali ya Rais John Magufuli wa kuifanya Tanzania nchi ya viwanda, Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania (TSSA), unakusudia kufufua viwanda 25 ambavyo vimeshindwa kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 baada ya Serikali kuvibinafsisha.
Hatua hiyo inalenga kusaidia kukuza uchumi wa nchi, lakini pia kuibua ajira zaidi, ikiwezekana asilimia 40 ya ajira katika sekta ya viwanda Tanzania itokane na uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii, huku bidhaa zake zikiwa za kiwango cha juu kwa ajili ya soko la ndani na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Katibu wa TSSA, Meshack Bandawe ambaye ni Meneja wa Mfuko wa Pensheni wa PPF katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.
Bandawe amesema mbali ya kufufua viwanda hivyo, pia mifuko ya hifadhi za jamii inatarajiwa kujenga viwanda vipya katika sehemu mbalimbali za nchi ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
Alitoa mfano kuwa mbali ya mfuko mmoja mmoja, kuna miradi ya pamoja ukiwamo wa Kiwanda cha Morogoro Canvas ambacho ni cha kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa utengenezaji wa nguo ngumu, zikiwemo sare za majeshi, shuka za hospitali, sare za wafungwa na maturubai.
Kiwanda hicho kitakapoanza tena uzalishaji wakati wowote kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao, kinatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 700. “Tumeiona hiyo fursa, hivyo lazima tuchangamkie kukifufua na kuzalisha bidhaa hizi kwa ajili ya soko la Afrika Mashariki,” alisema Bandawe.
Aliitaja mifuko inayoshiriki katika mradi huo kuwa ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), PPF, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Serikali Kuu (GEPF) na Shirika la Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Umoja wa mifuko pia umeweka nguvu ya pamoja na kuelekeza katika kufufua vinu vya pamba, ikianza na vitatu ambavyo vinatarajiwa kuzalisha ajira za viwandani 1,200, lakini wakulima zaidi ya 7,000 wakitarajiwa kunufaika kutokana na umoja huo kulenga kufufua mashamba makubwa ya pamba.
Wanakusudia pia kuwekeza katika viwanda vya nguo vya Urafiki kilichopo Dar es Salaam na Mwatex cha Mwanza, achilia mbali katika sekta ya ngozi ambako wanatarajia kuwa na kiwanda kikubwa cha bidhaa za ngozi.
“Kwa ujumla tunataka kuitikia wito wa Rais wa kuwa na viwanda vitakavyoajiri wengi, vitakavyokuwa na mnyororo mrefu wa thamani kuanzia kilimo, malighafi na kadhalika kutoka hapahapa nchini, lakini bidhaa zikivuka mipaka.
Hii ina maana tutahakikisha pia vinakuwa na ubora wa kimataifa,” alisema na kuongeza kuwa, kwa kuanzia, ikianza kabla ya mwaka 2019, itatoa ajira zaidi ya 200,000. Akizungumzia viwanda 25, alisema 15 vimeshapata idhini ya kuendelezwa huku vingine 13 vikiwa katika hatua ya upembuzi yakinifu.
Alitoa mfano kuwa NSSF imewekeza katika kiwanda cha kuua viuatilifu vya malaria kilicho Kibaha mkoa wa Pwani, imefufua vinu vya kusindika nafaka vya Shirika la Taifa la Usagishaji (NMC) vya Iringa, Dodoma na Mwanza vitakavyotoa ajira 30,000, Kiwanda cha Matairi cha General Tyre mkoani Arusha, kinacholenga kutengeneza matairi ya kisasa kwa ajili ya soko la ndani nanje ya nchi.
NSSF itawekeza pia katika Kiwanda cha Chaki cha Maswa mkoani Simiyu, Kiwanda cha Sukari cha Lulanzi kitakachozalisha pia umeme. Inaelekeza pia nguvu katika kilimo cha katani na kuboresha uzalishaji za bidhaa za katani, huku ikishirikiana PPF na Magereza katika kilimo cha miwa na kufufua viwanda vya sukari vya Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro.
Kwa upande wa PPF, mbali ya ubia na NSSF katika mashamba na viwanda vya Mkulazi na Mbigiri, pia inawekeza katika kiwanda cha viatu na bidhaa za ngozi kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza mkoani Kilimanjaro, huku ikiwa na mipango ya kujenga kiwanda cha kuchakata ngozi kinachotarajiwa kuanza kazi mwishoni mwa mwaka kesho.
Nayo PSPF, pamoja na kufufua Kiwanda cha Dawa cha TPI cha Arusha, itajenga pia kiwanda cha matofali na kuchoma vigae Dodoma, kiwanda cha vifaa ya umeme na nguzo za zege, lakini pia soko la kisasa la kuuza mazao.
Kwa upande wa LAPF inakusudia kujenga machinjio ya kisasa ya Nguru, Mvomero mkoani Morogoro itakayokuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 300 kwa siku, lakini pia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa Kiwanda cha Tangawizi cha Same mkoani Kilimanjaro.
NHIF inawekeza katika ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za pamba kwa matumizi ya hospitali, kiwanda cha maji-tiba, vyote vikiwa mkoani Simiyu. WCF inawekeza kwa kushirikiana na GEPF katika kujenga viwanda vya juisi na mvinyo kutokana na zabibu, wakati ZSSF inajikita katika viwanda vya kisasa vya usindikaji wa samaki. GEPF itafufua pia kiwanda cha zana za viwandani cha Kilimanjaro
Chanzo: HabariLeo