MWANANGU SITAKABARI(SIKU YA MAMA)
1.
Mwanangu ewe mwanangu, leo nataka kulonga
Kila jambo lina Mungu, heri na shari hupanga,
Tamu ligeuke chungu, asali iwe pakanga,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
2.
Mwanangu sicheke ufa, kumbuka kuna Jalia,
Siringe kutaka sifa, kiburi ukajitia
Aliye na afya hufa, mgonjwa akabakia,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
3.
Mwanangu hebu elewa, nakuomba zingatia,
Ugonjwa ni majaliwa, mauti ni yetu njia,
Hupona mkusudiwa,hufa mshika jambia,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
4.
Mwanangu naomba shika,nisemayo sio siri,
Haya yamethibitika, kitambo tena dahari,
Mbichi unanyauka, mkavu una nawiri,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari
5.
Mwanangu sifanye ngenga, usitambie ukwasi,
Mambo ukiyabananga, tamkufuru Qudusi,
Mbio hushinda kinyonga, aachwe mbali farasi,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
6.
Mwanangu usiwe chizi, cheo huwezi miliki,
Nataka ujue wazi, hakina hatimiliki,
Chifu awe mjakazi, mtumwa awe maliki,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
7.
Mwanangu yana Karima, kupanda hata kushuka,
Uwende mbele na nyuma, ufanye unavyotaka,
Mla chunga hula nyama, mla nazi hula daka,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
8.
Mwanangu sicheke mamba, nawe mto hujavuka,
Kwa kiburi ungatamba,hupindui la Rabuka,
Hukosa aliyeomba, hupata asiyetaka,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
9.
Mwanangu sifanye inda, aliyepewa kapewa,
Ujue heri ya shinda, kiumbe ulojaliwa,
Ukijua vya kutenda, sisaahu kutendewa,
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
10.
Mwanangu niendelee, ama kikomo nitie,
Nilosema sichezee, wallahi sipuuzie,
Kitaka uogelee, wasia uzingatie.
Dunia hino dunia, mwanangu sitakabari.
Pichani ni mama yangu mzazi, kwasasa ni marehemu na amefariki tangu mwaka 2000. Kwangu ndio kila kitu, nampenda sana mama yangu, ila Mungu amependa zaidi kiasi amchukue, nimetunga shairi hili maalum kwaajili yake, najua maneno hayo alitaka kuzungumza lakini muda haukuwa rafiki kwake.
Leo nayasema kwa niaba yake nikiambia nafsi yangu, naam, nafsi yangu isitakabari kwani dunia ndio hii na kwa vyovyote vila hayana budi.
Dotto Chamchua Rangimoto.(Njano5)
whatsapp/call 0622845394 Morogoro