Tulivyokuwa tukiiba almasi mgodi wa Mwadui na wenzetu kuuawa

barafu

JF-Expert Member
Apr 28, 2013
6,739
32,866
Hii ilikuwa ni miaka ya '90 mwanzoni, tukitokea pembezoni mwa mgodi wa Mwadui, tulifahamika kwa jina la "Wabeshi".

Zana zetu za kazi ilikuwa ni sululu, chepe na majembe yaliyonolewa sana, tulikabiliana na jeshi la polisi la mgodi wa Mwadui waliokuwa na kikosi cha farasi na mbwa wenye uweredi mkubwa sana na mafunzo ya hali ya juu.

Nakumbuka siku rafiki zangu wawili walivyouwawa kwa kuumwa na mbwa sehemu za siri na jirani yangu Jilingumika Masufulia alivyopigwa risasi ya kichwa akivuka fensi ya mgodi wa Mwadui.

Almasi tuliibatiza jina la "ng'ana", na ilikuwa hauwezi kwenda kuiba bila kuchanjwa chale za kwapani na matakoni. Mganga wetu mkubwa alikuwa ni Mzee maarufu sana wa Kijiji cha MWIGUMBI, Nje kidogo ya mgodi, huyu ndio mzee aliyetupa dawa na kinga wakati wa kwenda kuiba almasi,wakati huo nikiwa na miaka kama 16 tu hivi, nimemaliza darasa la saba shule ya msingi Luhumbo. Tajiri wetu mkubwa alikuwa mwarabu wa Maganzo maarufu kwa jina la Abeid, huyu alitupikia vitumbua na chai kabla ya kwenda mgodini kuiba almasi, na chote tulichokipata tulipeleka kwake kama tajili na kupata ujira wetu.

Tajiri Abeid hakuwa mtu "rahisi rahisi", yeye mganga wake alikuwa anatokea kijiji cha Idukilo, mganga hatari sana aliyekuwa na madawa ya kisukuma ambayo yaliwabadilisha watu na kuwa mbwa mwitu au nyani pindi walipoingia ndani ya mgodi kuiba, tajiri Abeid alikuwa anaishi kijiji cha Maganzo, akiwa na duka la bidhaa la kuzugia,lakini deal zake kubwa ilikuwa ni kununua almasi na kuziuza kwa matajili wakubwa wa Mwanza na Shinyanga mjini.

Almasi zote tulizopeleka kwa Abaeid zilikuwa zinatunzwa na mbuzi dume, beberu mkubwa aliyekuwa anazimeza na kuzihifadhi tumboni hadi mteja atakapokuja,hata polisi wakifika na ku-search vipi,wasiongeziona almasi kwani beberu alikuwanazo tumboni,hakuwa beberu wa kawaida maana alikuwa na chumba chake na alilala ktk godoro. Mbuzi hakula nyasi wala majani ya miti, bali vitumbua, chai, ugali na "maparage". Kipindi hicho hatukuwa na ruhusa ya kuongea juu ya mbuzi yule, tulimuogopa na kumtii zaidi hata ya kiongozi wa msafara wa wabeshi.

Tajiri wa uhakika alikuwa Fantomu wa maeneo ya Mipa,huyu hakuonana na sisi wabeshi maana tulikuwa watu "wadogo" sana, bali alipitia kwa Abeid na waarabu wengine wa Maganzo.

Maisha ya kuwa "mbeshi" yalikuwa magumu sana,maana kifo na kujeruhiwa ilikuwa ni njenje,tuliuwa na kuuwawa. Polisi, mbwa na farasi waliokuja bila tahadhari waliuwawa kwa chepe zilizonolewa na mapanga. Tukio moja nalokumbuka ni la mwenzetu Masunga kumuua mbwa wa polisi kwa kumkata na chepe mdomoni na kuutenganisha mdomo pande mbili.

Wenzetu wengi walikufa tukiwa bwawani tukiiba,wengi walizama kwenye tope liliotokana na mabaki ya kusafishwa kwa almasi ambayo sisi tulikuwa tunakwenda kuchota na kuchekecha upya,bwawa hili la tope zito lilukuwa karibu na "sorting area" ambayo ililindwa kwa kiasi kikubwa sana. Lakini kwa imani ya chale za mganga wa MWIGUMBI na Idukilo watu wengi tulikuwa na ujasiri wa kukatiza kila mahali bila hofu.

Wengi waliojeruhiwa na kuumizwa walilazwa ktk hospitali ya Mwadui.Siku nilipoamua kuacha "kazi" hii na kurudi shule,ilikuwa ni siku hatari sana... binamu yangu kipenzi Luhende alipigwa risasi ya kichwa na ubongo kutawanyika, mbele ya macho yangu Luhende alikufa bila hata kuomba maji. Askari wakiwa umbali wa kama mita 100,sisi tukiwa na makarai yetu na chekecheke tukiambaaambaa pembeni ya reli maeneo ya SONGWA ktk njia ya mzunguko kuelekea Maganzo tuliwekwa katikati yao na kuuliwa baadhi yetu. Katika kundi la wabeshi kumi, saba walikufa hapo hapo..watatu walifia hospitali na mimi pekee nilipona baada ya kujitumbukiza kwenye bwawa la maji ya kunywea mifugo, niliogolea chinichini kwa chini na kuibukia upande wa matete, ambapo nilikaa ndani ya maji zaidi ya masaa 12 bila kutoka..nikiwa nimetoa pua tu na kujishikiza kwenye "msitu" wa matete.

Kikosi cha polisi wenye mbwa na farasi walizingira bwawa lile mpaka usiku wa kiza kinene, wakaamini nimeshakufa na kuzama hivyo wangefika kesho yake kukuta ninaelea baadaya kufa.Katikati ya kadhia ile ndipo nilpoona kazi ya ubeshi si lolote si chochote, zaidi ya mwili kujaa chale za tako mpaka kwapani.

Pesa tuliyopata ilishia mnadani Maganzo,ambapo tulikula na kunywa. Hatimaye niliamua kurudi kijijini Luhumbo,nikakariri tena darasa la saba kwa jina la mtoto wa mjomba aliyeacha shule na kwenda kuchunga na kulima vibarua maeneo ya Muhunze. Nilikuwa mkubwa kuliko wote darasani lakini sikukata tamaa. Nilisoma kwa mwaka mmoja wa darasa la saba kwa bidii na usongo na hatimaye kuchaguliwa kujiunga na shule ya Tabora Wavulana.

Kwa mara ya kwanza napanda train kwa "warrant" ya serikali, station ndogo ya Songwa kupitia Shinyanga kuelekea Tabora. Nakutana na Afande Chacha kwenye geti la Tabora boys, ananipokea kwa kichurachura na bakora za mgongo bila sababu, wakati huo Tabora Wavulana ipo chini ya jeshi. Mwanzo naona maisha ya ubeshi ni afadhali kuliko shule ya aina hii..mchakamchaka na Afande Chacha kila asubuhi kupitia Kwihala mpaka Kipalapala.Juma la kwanza natamani kutoroka lakini sijui mahali pa kuelekea, shule ipo nje ya mji na mfukoni sina nauli.Baada ya mwezi ndani ya kombati ya kijani mwanajeshi,inatangazwa disko ya "welcome form one".

Disko langu la kwanza maishani,nakutana na watu wenye lafudhi nzuri na Kiswahili kilichonyooka, mimi nashindwa kuongea mbele za watu sbb lafudhi yangu ni "ngumu" kusikika na kueleweka. Ninapata marafiki toka pande mbalimbali za Tanzania. Kapufi wa Mpanda na Mwaisengela wa Mbeya wanakuwa marafiki zangu kwenye bweni la Kimweri. Miaka minne ndani ya Tabora,wao wanaita Mboka Manyema..ninabahatika kurudishwa tena kidato cha tano na cha sita,baadae naamua kuingia Jeshi bila kwenda chuo Kikuu. Ninalitumikia jeshi kwa muda mrefu, safari yangu ya Lebanoni kusiamamia amani inanirudisha nyumbani na kukuta mke wangu akiwa na mimba ya miezi sita na mimi nilikuwa nje kwa mwaka mzima.

Nikukumbuka nilipotoka,shida na vurugu za kuwa mbeshi....Oooops!!! Naona dunia sio mahali salama pa kuishi
 
Swala la kuuwawa kwa wabeshi halijaisha hadi leo,ilikuwa mwaka -2009-2010 nilipitia kwa waganga wawili tofauti mmoja Kutoka BUBIKI na Mwingne wa NZEGA Walinihakishia nitaenda kupata ALMASI,Lakini niliposhuhudia jamaa yangu akikoswa kuuwawa kwenye lile tope..ndio ilikuwa mwisho wangu kuwa mgoni.
 
Omwise Lubumbo ki, nene nafumile mnyashimbi.

Umenikumbusha nilivokuwa nachekwa kushindwa kutamka the minasema ze kisa msukuma na lafudhi yangu ndo basi tena.

The good thing sukuma people always dont fail.
 
Sasa ana uchungu unataka nimuongezee uchungu? bora kakuta mimba kuliko angekuta mke kahonga nyumba kama ufoo saro. Haya ya mimba yanaongeleka bwana hehehe.

Wifi hajambo? muambie sie tunapima dna kwa kutemea mate kwenye kiganja, ole wake
duuh mbona unataja tena majina mkuu
 
Duh very interesting.pls proceed
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…