MADINI aina ya tanzanite ya thamani ya Sh bilioni 2.5 yaliyokamatwa mwaka jana yakitoroshwa nje ya nchi, yatauzwa kwa mnada wa hadhara wakati wa maonesho ya kimataifa ya madini ya vito yaliyoanza jana hapa.
Madini hayo yalikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) yakitaka kutoroshwa kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu wa kisheria na baada ya kukamatwa yametaifishwa na serikali.
Akizungumza jana jijini hapa wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo ya tano ya madini ya vito ya siku tatu, Kaimu Kamishna wa Madini nchini, Ally Samaje, alisema madini hayo yatapigwa mnada katika maonesho hayo ikiwa ni sehemu ya kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini.
Samaje alisema hakuna mtoroshaji wa madini anayekuja kutoka nje bila kuwa na mawasiliano ya Watanzania wenyewe na alisema cha msingi lazima kila mtu awe mzalendo wa nchi yake na kudhibiti utoroshwaji wa madini.
Alisema hivi sasa serikali haina mchezo na utoroshwaji wa madini hayo ya tanzanite pamoja na mengine na yeyote atakayebainika kuhusika na utoroshwaji huo, madini yake yatataifishwa na sheria kuchukua mkondo wake.
“Suala la utoroshwaji wa madini limekuwa tishio na sisi tunasema serikali ipo makini na jambo hilo na ikibainika madini yanatoroshwa yatataifishwa, tunataka madini haya ya tanzanite na mengine yanufaishe Watanzania wenyewe,” alisema Samaje.