Simulizi ya Kijasusi: Salamu Kutoka Kuzimu

Abdallahking

JF-Expert Member
Mar 19, 2018
3,983
10,821
2010143000065_1.jpg



Simulizi : SALAMU KUTOKA KUZIMU
Mwandishi : BEN R. MTOBWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES

SEHEMU YA 1


KIFO kaja duniani kwa kazi moja tu. Akikukuta umekwisha... Akikusalimia umekwisha... Hana mdhaha. Lakini sasa huyu anataka watu mashuhuri, watu wakubwa zaidi. Anataka kuifanya Afrika nzima iangue kilio na maombolezo ambayo hayajapata kutokea duniani. Na anataka hilo litokee siku moja, saa moja... "Bendera zote duniani zipepee nusu mlingoti", anasema huku akichekelea. "Sijawahi kushindwa..." Jasho linawatoka watu mashuhuri. Damu inamwagika kama mchezo. Inspekta Kombora machozi yanamtoka. Joram Kiango anabaki kaduwaa.

SURA YA KWANZA

"Bado nasisitiza kuwa tusithubutu wala kujaribu kufanya lolote kabla ya kuhakikisha kuwa Joram Kiango yu marehemu", ilidai sauti moja nzito.

"Naam, lazima afe", sauti nyingine iliunga mkono. "Afe kabla hatujainua mikono kufanya lolote tulilokusudia. Hakuna asiyefahamu jinsi kijana huyu alivyo hatari anusaye shari na kuingilia kati kuharibu harakati zote. Hajasahaulika alivyowakorofisha wale mashujaa waliotaka kuuangusha utawala wa nchi ya Ngoko katika tukio lile lililoitwa Dimbwi la damu. Kadhalika bado hatujasahau alivyosababisha vifo na kuharibu mipango ya majasusi waliotaka kuiharibu nchi hii katika mkasa ambao mtu mmoja aliuandikia kitabu na kuuita Najisikia kuua tena. Kwa kila hali Joram Kiango ni mtu hatari zaidi ya hatari zote zinazoweza kutokea, Hana budi kufa".

Kicheko kikavu kikasikika kidogo, kikafuatwa na sauti iliyokwaruza ikisema.

"Atakufa. Lazima afe. Na atakufa kifo cha kisayansi kabisa. Mpango huu tumeuandaa kwa uangalifu mkubwa, Na watekelezaji wake pia ni watu ambao
 
SEHEMU YA 2

wamehitimu vizuri katika nyanja zote zinazohusika na kazi hii, Tuondoe shaka kabisa. Mpango huu utafanikiwa kwa asilimia mia".

"Kwa hiyo ndugu Mwemyekiti", ilisema sauti ya mtu wa kwanza. "Niwie radhi kwa kukukata kauli. Ninachokuomba ni kuuahilisha mkutano huu na tusisubutu kukutana tena hadi hapo Joram Kiango atakapokuwa kaburini, Pengine mtaniona mwoga kupindukia, Lakni mimi sipedi kabisa kufanya jambo lolote wakati kijana yule akiwa hai. Mnajua jinsi alivyo na miujiza. Anaweza kuwa hapa akisikiliza mazungumzo yetu, kesho tukajikuta mahakamani bila kutegemea".

Ilizuka minong'ono, sauti mbili tatu zilimuunga mkono msemaji aliyemaliza kusema. Jina la Joram liliamsha hofu katika mioyo yao. Wakatazamana...

Walipenda pia kumwona Mwenyekiti wao uso kwa uso. Kwa bahati mbaya, hawakuweza kuona uso wake isipokuwa kiwiliwili tu, ambacho kilifunikwa kwa mavazi ya thamani kama walivyokuwa wamevaa wao. Mwanga mkali uliotokana na taa ya umeme iliyowekwa kwa namna iliwachoma macho kila walipotamani kumtazama Mwenyekiti usoni. Ni yeye tu aliyekuwa na nafasi nzuri ya kuwatazama wote mmoja baada ya mwinginge kikamilifu na kuwasoma nyuso zao. Wakati wa kumtambua Mwenyekiti ulikuwa bado haujawadia hivyo hawakupaswa kumuona kabisa isipokuwa sauti yake tu.

Mkutano huo ulifanyika katika chumba cha siri, chini ya ardhi katika mojawapo ya majumba ya kifahari yaliyoko Jijini Dar es salaam.

Kila aina ya tahadhari iliwekwa kuhakikisha usalama wa mkutano huu wa awali. Mkutano ambao ulikuwa umeitishwa ghafla, kwa njia za kutatanisha,
 
SEHEMU YA 3

hata wajumbe hao walijikuta wamefika kwenye mkutano bila kufahamu kilichowaleta hapo.

Mwenyekiti akaufungua mkutano huo kwa maneno machache akisema: "Tunataka kuitetemesha Afrika na kuishangaza dunia. Tunataka kuachia pigo ambalo halitafutika katika historia ya Ulimwengu". Wajumbe wakaelewa kinachoendelea. Ndipo mjume mmoja alipotoa rai ya kumaliza kikao hadi watakaposikia Joram Kiango amekuwa marehemu.

Tahadhari kubwa ilikuwa imechukuliwa wakati wa kuandaa mkutano huo. Wajumbe waliingia kwa siri kubwa wakipita milango tofauti, katika eneo hilo vilitegwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhakikisha kila mshiriki wa mkutano huo wa siri anahusika kwa njia moja ama nyingine. Walihakikisha pia hakuna kifaa au chombo chochote cha kunasa sauti ama kusikiliza maongezi hayo ya siri. Vinginevyo chumba hicho kingeweza kutoweka kisayansi kisionekane mlango wowote zaidi ya kuta za kawaida. Zaidi ya yote silaha za kisasa, hewa za sumu, buduki zisizotoa mlio, madawa ya kulevya na mbinu zingine zilikuwa tayari kutumika endapo lolote lingetokea. Kwa bahati mbaya, ni Mwenyekiti peke yake ndiye aliyejua mpango mzima kuhusu mkanda huo.

Kulikuwa na kila sababu ya kuweka tahadhari au uangalifu huo. Watu waliokutana katika mkutano huu hawakuwa watu wenye njaa ya pesa wala kiu ya utajiri. Ni watu mashuhuri walioshiba na kudhamiria kulinda shibe yao. Wote walikuwa na hadhi mitaani, nyadhifa serikalini, na heshima katika chama. Waliokutana hapa wote walikuwa na matarajio ya kuvuna matunda
 
SEHEMU YA 4

matamu. Matunda ambayo yangetokana na mkutano huo. Hakuna mjumbe aliyependa kukosa utamu wa matunda hayo. Hivyo wote walikuwa na dhamira moja.

"Inaonyesha kuwa Joram ni tishio kwa kila mtu hapa", Sauti nzito ya Mwenyekiti ilisema. "Hilo linanifanya nizidi kuwa na imani juu ya dhamira yenu. Joram anaogopwa kuliko Polisi na jeshi zima la nchi hii, Kwanini? Wanajeshi mko hapa, polisi mko hapa, Chama tawala kiko hapa. Serikali iko hapa. Anayekosekana hapa ni mtu huyo anayejiita Joram Kiango. Mtu mtundu sana, ambaye utundu wake ni madhara kwa watu wenye dhamira maalumu. Hakuna atakayeshuku kuwa kauawa. Daktari atampima na kuona kafa kwa kansa ya moyo. Atauawa kitaalamu na kufa kistaarabu. Msiwe na shaka".

Kimya kifupi kikafuata. Wajumbe wakatazamana usoni. Kimya kilimezwa na sauti ya Mwenyekiti alipoongeza maneno.

"Kwa hiyo, naahirisha kikao hiki kama alivyoshauri mjumbe. Tutakutana tena hapa baada ya wiki mbili, siku na saa kama za leo, kwa njia zetu zile zile, bila kusahau kuwa joram Kiango hatakuwa Joram tena ila hayati Joram Kiango. Na ifahamike kuwa kuitoa nje siri hii ni sawa na kujiwekea saini ya kifo chako mwenyewe".

"Ni kweli Mwenyekiti", sauti mbili tatu za wajumbe wenye hofu, ziliitikia.


Nyumba mbovu zilizojengwa bila utaratibu katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ambazo huishi kina mama kutoka sehemu mbalimbali nchini
 
SEHEMU YA 5

ambao humudu kupanga katika nyumba hizi kwa ajili ya makazi na biashara isiyosemekana wala kuitamka. Biashara ambayo ni aibu kubwa kuitaja hadharani, japokuwa inafanyika hadharani bila kificho. Biashara ya kuuza miili kwa pesa chache za matumizi.

Tupo Mburahati, mbele ya moja ya majumba ya aina hii. Kaketi mwanamke ambaye umri wake haujaruhusu kumwita mwanamke. Yu msichana mwenye sura nzuri, mwendo mzuri na kila kitu kizuri, Hata mavazi yake si duni kama wenzake walioketi hatua chache karibu yake, mbele ya milango ya nyumba zao, Kwa jina msichana huyu anaitwa Waridi.

Ni juzi tu Waridi alipotokea hapa Mburahati na kujipatia chumba. Sifa na uzuri wake zilizagaa haraka haraka zikawafikia hata wale ambao si wateja wa biashara hii. Kwamba kaja msichana mzuri.Hakuna aliyetaka kujua katokea wapi, Hakuna aliyetaka kujua kwanini binti mzuri kama huyu aamue kutouthamini uzuri wake ambao ungemfanya aishi vizuri zaidi, akila na kunywa pesa za walionazo. Hakuna aliyejali.

Leo Waridi alikuwa katika hali yake ya kawaida. Hali ya ukimya na majonzi pamoja na kwamba alionekana akiwachekea mara kwa mara wateja wake. Hakuna aliyejua jeraha kubwa lililokuwa moyoni mwake. Jeraha ambalo lilikuwa siri yake na alipenda liendelee kuwa siri. Kutunza siri ni kazi kubwa kama kubeba mzigo mzito usiobanduka kichwani. Mzigo aliobeba kwa dhiki sana. lakini alistahamili kwanki maisha yake yenyewe yalitegemea utunzaji wa siri hii.

Mara akatokea mteja ambaye sura yake, mwendo wake na mavazi yake
 
SEHEMU YA 6

vilimtofautisha na wateja wa kawaida. Huyu alimtaka Waridi afunge biashara yake siku hiyo ili wafuatane wote nyumbani kwake.

"Haiwezekani. Ninaye bwana wangu ambaye huja kulala hapa".

"Twende kwangu halafu nitakurejesha hapa haraka iwezekanavyo".

"Haiwezekani vilevile".

"Ziko pesa nyingi kwa ajili yako kama utakubali kwenda nyumbani kwangu".

"Nimesema hapana". Ghafla hasira zikampanda Waridi. AKashangaa kwanini kamchukia mtu huyu. "Toka kama hutaki", alifoka na kumwacha mtu huyo kakalia kitanda chake.

Mteja huyu akatabasamu. Kwa waridi lilikuwa tabasamu la kebehi ambalo halikumshitua kuliko alivyotegemea. Swali fupi likaulizwa kwa sauti ndogo. "Huendi na mimi? Hata nikisema kuwa marehemu Bomba ni ndugu yangu pia nafahamu mpaka mahali alikozikwa?".

Hilo lilimshitua kidogo Waridi. Mshituko ulipomtoweka yalifuata machozi mengi yaliyomtoka katika macho yake yaliyoduaa kwa hofu yakimtazama mteja huyo. Mwili wake ulikuwa umemlegea kiasi cha kumfanya ashindwe hata kusimama kikamilifu.

Waridi hakuwa na uwezo wa kufanya lolote. Ndipo mteja huyu alipomsukuma Waridi na kuanguka chali kitandani, akampambua mavazi yote na kumtenda kikatili yote aliyojisikia kumtendea.

Baada ya hapo mteja alimwamru Waridi kufuatana naye. "Tutatoka mara moja. Ukiendelea kukataa nami nitashindwa kutunza siri yako. Twende zetu. Nitakupa kazi ndogo tu, unisaidie. Kuna mtu anahitaji kufa. Utamsaidia wewe. Haitakuwa kazi kubwa kuua mtu wa pili mama. Au vipi? Tofauti pekee ni kwamba yule aliitwa Bomba na huyu anaitwa Joram".

Waridi alimfuata kikondoo.


**********************************
Huyu hakuwa mwingine zaidi ya Jodor Prosper kama alivyojiita katika ule
 
SEHEMU YA 7

mkutano wa siri uliofanyika usiku wa juzi. Yeye akiwa Mwenyekiti.

Jina hilo lilikuwa moja miongoni mwa majina yake kadha wa kadha ambayo huyatumia wakati tofauti na kwa dhamira tofauti. Kadhalika alikuwa mtu mwenye sura mbalimbali na miondoko aina aina. Kila jamii ilimfahamu Prosper yule yule katika jina na sura tofauti. Vivyo hivyo, tabia zake kubadilika mara kwa mara kama kinyonga anavyojibadili rangi. Katika kundi la wahuni Prosper yu mhuni mkubwa, katika jamii ya waungwana yu muungwana halisi, katika familia ya masikini Prosper alikuwa mmoja wao, na miongoni mwa matajiri yeye ni kama wao.

Huyo ndiye Prosper. Mswahili aliyezaliwa mahali fulani katika Pwani ya Bahari ya Hindi. Akiwa na miaka kumi na miwili, alitoweka numbani kwao kwa kudandia meli moja iliyotia nanga katika Bandari ya Tanga.

Meli hiyo iliyokuwa na mabaharia katili kupita kiasi. Walimpokea Prosper kwa ukatili usiosemekana. walimtendea mengi maovu, akitukanwa na kusimangwa. Aliishi kwa taabu mno, akiyastahamili yote hayo, mwishowe, akawa mnyama kama mabaharia wale.

Alisuguliwa akasugulika, akageuka kuwa Baharia binadamu mwenye moyo wa mnyama. Akamchukia kila mtu na hata kuichukia nafsi yake mwenyewe. Wakati wote Prosper alitawaliwa na fikra potofu. Alitamani kutenda jambo ambalo lingeiumiza jamii. Kwa bahati mbaya, hakuwa mwana sayansi mwenye vipaji vya ugunduzi, ugunduzi ambao ungemwezesha kuiteketeza jamii. Angekuwa na uwezo wa kujitengenezea bomu la nuklia angeifanya dunia itoweke katika uso wa ulimwengu.
 
SEHEMU YA 8


Kwa kuwa, hayo yalikuwa mbali na uwezo wake, lakini alifanya ukatili mdogo tu. Hakuona shida kumtosa baharini mtu yeyote aliyebainika kudandia meli kama alivyofanya yeye alipokuwa mtoto. Wala, kwake haikuwa dhambi kufanya mapenzi na mwanamke na kisha kukata koo la mwanamke huyo asubuhi.

Pamoja na ukatili huu kuufanya kwa siri, lakini sifa zake ziliyafikia masikio mbalimbali. Mmoja kati ya watu waliovutiwa na unyama wa Prosper aliona fahari kukutana nae katika meli hiyo kwa siri. Wakaiacha meli hiyo. Safari yao ikaishia katika chuo kimoja kilichofichika kikiwa na watu wachache wenye moyo kwama wa Prosper. Kilikuwa chuo cha ujasusi kilichokuwa chini ya nchi kadhaa kubwa na tajiri. Kilifundisha mbinu kadha wa kadha kuhujumu siasa, uchumi na msimamo wa nchi kongwe na changa ambazo hazikuwa tayari kulegeza misimamo yao na zile zenye msimamo mkali.

Prosper alipohitimu tayari alikuwa hodari wa yote, kuandaa mauaji, kusababisha mapinduzi, kudhorotesha uchumi. Alikuwa mtu aliyeipenda sana kazi yake, na alifanya mengi yaliyowafurahisha na kuwatisha viongozi wake. Aliweza kusafiri hadi Afrika Kusini ambako alijitangaza kama mpigania uhuru na aliaminika na kushirikishwa katika harakati za ukombozi. Lakini aliweza kutoroka na siri zote huku akiwa tayari ameua na kuwaacha wapigania uhuru wakiuana wenyewe kwa wenyewe. Mtindo huo ameutumia sehemu mbalimbali duniani. Ingawa waliohujumiwa walimhisi baada ya kuondoka, lakini kwa jinsi alivyokuwa akiwaendea katika sura tofauti, na majina bandia,
 
SEHEMU YA 9

hakuna aliyeweza kumweka katika kumbukumbu.

Mfano ni leo alipokuwa akitoka na msichana huyu aliyechanganyikiwa; Waridi. Wajumbe wote wa mkutano ule ambao walibahatisha kuuona uso wake wasingeweza kumfikiria kuwa ndiye mtu yule yule waliyekuwa naye mkutanoni kwa jinsi alivyobadilika. Hata mwendo wake ulikuwa tofauti. Leo alitembea huku akichechemea kidogo.

Gari dogo aina ya Toyota lilikuwa likiwasubiri mara tu walipoifikia barabara.

"Ingia ndani ya gari", Prosper aliamuru.

"Samahani..., samahani kaka, tu... tunaelekea wapi?", Waridi alifanikiwa kuupata ulimi wake ambao alihisi ulikuwa mzito kutokana na hofu.

Prosper akaukunja uso wake huku akisema, "Sitaki maswali", akapita upande wa dereva na kumfungulia mlango Waridi. Alipoingia ndani ya gari na kuketi, gari likatiwa moto na kuteleza juu ya barabara, likijitahidi kukwepa mashimo. Walipoifikia barabara ya Morogoro, gari hilo liliekezwa katikati ya jiji. Wakaiacha Magomeni, wakaingia Upanga, wakipita hapa na pele hata waridi asijue kama walikuwa wapi,

Gari lilisimama mbele ya jumba moja kubwa sehemu ambayo hisia zilimwambia Waridi kuwa ni katikati ya Jiji. Prosper alitelemka na kumwagiza Waridi amfuate. Walipokaribia mlango mmoja kati ya milango kadhaa ya jumba hilo, Prosper alimnong'oneza Waridi akisema; "Unasikia? sitiki vurugu la aina yoyote hapa ndani. Uwe binti mtulivu kama ulivyo sasa. Utafaidika na kutoka salama. Vinginevyo..." akaiacha sentesi hiyo ikielea na kuanza kushugulikia funguo.

Walipoanza kuingia, mlango wa pili ulifunguka na uso wa mzee wa Kihindi
 
SEHEMU YA 10

kujitokeza ukichungulia. "Aha... ni bwana Chain siyo? Karibu sana".

"Shukrani", Prosper alijibu.

"Naona leo uko na mama, au siyo?, Mhindi huyo aliendelea akitabasamu. "Shauri kazi ya vitabu iko chosa kidogo. Lazima starehe na dada kidogo".

Prosper naye akajitia kucheka, "Eh, ndiyo. Lakini huyu ni sekretary wa kampuni yetu. Yeye amekuja kuchukua maandishi fulani kwa ajili ya kuchapishwa kwenye mashine wakati nitakapokuwa safarini".

"Ah", Mhindi alijibu huku akimtazama Waridi kwa tamaa ya wazi. Hili lilikuwa moja kati ya majumba ambayo Prosper alikuwa amepangisha vyumba ambavyo aliviyumia kwa shughuli zake. Hapa, mbali na kufahamika kwa jina la Chain Kimara, pia walimtambua kama msomi ambaye alikuwa akiutumia muda wake mwingi kufanya utafiti wa mambo kadha wa kadha ambayo alikuwa akiyaandikia kitabu. Hivyo, muda wote ambao Prosper alijificha chumbani akifanya shughuli zake za siri, wao waliamini kuwa alikuwa akiendelea na mipango ya kuhakikisha kitabu chake kinatoka. Akiwa hapa, hata sura yake ilionekana kama ya Profesa asiyependa kuuchezea muda wake kama ilivyokuwa tabia yake ya kisomi na kistaarabu.

Huko ndani picha ilikuwa hiyo hiyo, Waridi alilakiwa na chumba kikubwa kilichojaa vitabu vya kila aina , vilivyopangwa kistaarabu katika dawati maalumu. Katikati ya chumba hiki kulikuwa na meza kubwa yenye dalili zote za mashughuliko. Chumba cha pili kilikuwa na kitanda kipana, friji, radio na mahitaji yote ya chumba cha malazi. Ni katika chumba hicho alikokaribishwa Waridi.
 
SEHEMU YA 11


Akajibwatika juu ya kochi lililomwelekea Prosper, aliyeketi juu ya kitanda.

"Nimekuita hapa ili nikutume kuua mtu", Prosper alimweleza Waridi. Dakika ishirini zijazo nataka mtu huyo awe safarini akielekea kuzimu. Sasa hivi yuko katika baa moja hapa mjini akinywa pombe. Hiyo iwe pombe yake ya mwisho", Prosper alisita akamtazama Waridi. "Utanisaidia kuifanya kazi hiyo bi mdogo", akaongeza kwa sauti ya unyenyekevu.

"Siwezi kuua..." Waridi aligugumia.

Prosper alikunja uso akamwangalia Waridi kwa hasira huku akisema. "Sina haja ya kukukumbusha mara kwa mara kuwa najua yote yaliyompata marehemu Bomba. Naweza kutoa siri hiyo wakati wowote nawe ukajikuta ukining'inia juu ya kitanzi. Nitakufanyia hisani ya kuficha habari hiyo iwapo tu nawe utanisaidia kumtoa duniani mtu huyu. Tumeelewana?",

Waridi hakujua ajibu nini. Kwa kila hali. alimwona mzee huyu kampatia na kamweka mahali panapomstahili. Hofu yake kubwa haikuwa kitanzu tu bali ilimuumiza kutajiwa mara kwa mara jina hilo la Bomba. Ilimuumiza sana kukumbuka kifo cha mtu huyo kilivyotokea na jinsi alivyotoa macho wajati anakata roho. Ilimuumiza zaidi Waridi kukumbuka kuwa dhambi hiyo ya kuua alikuwa ameifanya bure kabisa.

Ni miezi kadhaa tu iliyopita. Wakati huo Waridi alikuwa Waridi wa ukweli. Ua la uhakika ambalo kila nyuki alilitamani, kila kipepeo alilimezea mate. Lakini si wote waliolifikia. Na wachache waliofaulu kuligusa, hawakuwa vipepeo wala nyuki wa kawaida. Walikuwa zaidi.

Uzuri wa msichana huyu ulianza kujitokeza tangu alipokuwa kinda. Alipofikia
 
SEHEMU YA 12

umri wa miaka mwili tu, kila mtu alibaini kuwa mtoto huyu alikuwa hazina ya uzuri. Alipofika miaka sita watu walianza kunong'ona. Alipohitimu miaka kumi, wanaume wasiokuwa na staha, walianza kumnyatia. Miaka kumi na miwili Waridi alikuwa tayari akiwa kama malkia wa nyuki na kama nilivyosema awali; kwa vipepeo.

Pengine uzuri wake huo ulitokana na ule mchanganyiko maalumu katika umbo lake. Mchanganyiko wa damu za watu weusi, Wahindi, waarabu na Wazungu ambao walishiriki kumtengeneza. Kwani mama yake pia alikuwa mtu wa nipe nikupe. Alifanya biashara yake katika mji wa Mwanza, katika mojawapo ya vibana vibovu, akimkaribisha yeyote mwenye 'chochote'. Mama huyu hakumfahamu kabisa mtu maalumu aliyeshirikiana naye kumpata Waridi binti yake wa pekee. Alichofahamu ni kuwa, kumpata binti mzuri ambaye watu walianza kumwita Waridi, hata jina lake la awali likasahaulika.

Kwa Waridi hakujua kama alikuwa mzuri kupidukia, lakini alishangaa kuwaona watu wazima kwa vijana wakimfuata na kumtaka kitu ambacho hakukifahamu maana ama umuhimu wake. Kitu kile ambacho alimwona mama yake akikifanya mara kwa mara kitandani.

Kisha akafahamu. Ilikuwa baada ya kukamatwa kwa nguvu na mzee mmoja aliyemtupa sakafuni, akamvua nguo na kumwingilia miguuni kwa namna ambayo ilimtia Waridi maumivu makali yaliyoambatana na faraja.

Waridi akayafahamu hayo, akaifahamu thamani ya uzuri wake, akaanza kuingiwa na kiburi. Akajidekeza na kutupilia mbali masomo. Huyo akamtoroka mama yake na kuingia mjini Tabora,ambapo aliishi kwa faraja
 
SEHEMU YA 13

kubwa. Daima wanaume walikuwa tayari kumhudumia kwa maneno matamu, malezi, mavazi huku akipewa fedha za kutosha.

Lakini Waridi hakutosheka. Daima alidai hiki na kile kwa wanaome ambao kila mmoja alijitahidi kutoa alichonacho. Lakini baada ya kupata walichohitaji wakamwepuka. Hivyo akauona mji wa Tabora haufai. Akasogea hadi Dodoma ambapo pia hakukaa sana, akapanda hadi Arusha. Mji huo ulipomchoka, akapaa na kushuka Jijini Dar es Salaam.

Ni hapo alipokutana na Bomba Kimara. Kijana huyu mwenye asili ya Kiarabu mtu ambaye Maua alimhitaji. Siku zote alionekana 'kajaa', Fedha kwa Bomba hazikuwa na tatizo. Wala hakuna uchungu kuzitumia. Kadhalika, fedha zake hazikuwa mfukoni kama wanaume wengine. Zake zilitoka katika soksi. Kitita cha elfu kumi kumi kikiwa kimefungwa kwa mpira kingewezaje kukaa mfukoni? Walizitumia fedha hizo na Waridi wakishirikiana kuhama baa moja kwenda nyingine, madansa, sinema, mahoteli na kila aina ya starehe.

Walikuwa wakiishi Magomeni Mikumi katika nyumba za msajili wa majumba ambayo Bomba alikuwa amekodi. Ni mara chache sana nyumba hii ilipowaona wapangaji wake, kwani mara nyingi walikuwa kama si Kunduchi Beach, basi wako Kilimanjaro Hoteli au Mbowe Hoteli na sehemu nyingine za starehe wakitumia.

Halafu ikafika ile siku ambayo Bomba alirudi nyumbani mapema kutoka kule alikokuwa akienda mara kwa mara na kurudi na pesa. Safari hii alirudi na mfuko wa ngozi ambao aliutua juu ya kitanda. Alionekana mtu mwenye wasiwasi mwingi kinyume na tabia yake. Hakujua kwa Waridi alikuwa
 
SEHEMU YA 14

chumbani humo akimtazama.

"Vipi mwenzangu?" Sauti ya Waridi ilimzindua. Akamgeukia akijaribu kutabasamu lakini tabasamu lilikataa.

"Waridi, kwenu ni wapi?" Bomba alihoji ghafla.

Swali hili lilimshangaza sana Waridi. Muda wote walioishi pamoja hawakuwahi kuulizana maswali ya aina hiyo.

'Kwanini?" Bomba akaendelea. "Nataka urudi kwenu. Mimi naona maisha hayaniendei vizuri", Bomba akaeleza. Baada ya kunyamaza kwa sekunde kadhaa, akasema.

"Waridi, ni hadithi ndefu ninayo. Hadithi ambayo haifai kulifikia sikio lisilohusika. Ninachoomba ni wewe kwenda zako kesho. Kama hutaki kwenda nyumbani kwenu, rudi kwenye baa niliyokukuta. Naamini ukirudi pale baa haitapita dakika tano kabla hujaokotwa na mwanaume mwingine".

"Kuokotwa?" Maua alijiuliza kwa hasira. Ghafla alijikuta kamchukulia Bomba kama mtu shetani. Hata sura yake sasa aliiona mbaya kama dhambi. Machozi yalimtoka na kuteleza juu ya mashavu yake. Akainuka na kutoka nje kimya.

Waridi alirudi ndani baada ya kumsikia Bomba akioga bafuni. Akafanya haraka kuuendelea ule mfuko ambao aliufunua. Macho yake yalikutana na furushi kubwa la noti ambalo hakuwahi kuliona katika maisha yake. Kwa kukadilia zilikuwa pesa nyingi. Kando ya pesa hizo, ililala bastola kubwa na tiketi moja ya ndege. Tiketi hiyo ilionyesha jina la Bomba kuelekea Nairobi.

Wazo likamjia Waridi. Bomba alikusudia kumtupa baada ya kupata pesa nyingi kama hizo ili aende zake Nairobi akatumie peke yake! Waridi akajishauri kuchota pesa kidogo afiche. Akasita. Alizihitaji zote. Akaamua kuzipata. Akazirudisha kama zilivyokuwa akatoka zake nje.
 
SEHEMU YA 15


Usiku huo, Waridi alikuwa wa kwanza kulala. Alijitia kulia pole pole kwa namna iliyokusudiwa kumfanya Bomba aamini kuwa Waridi alimpenda kwa dhati. Ukweli ni kwamba katika maisha yake Waridi hakuwahi kumpenda mwanaume. Alipeda pesa. Mwanaume alimhitaji kwa ajili ya faraja ya mwili tu.

Bomba alikuwa amelala kando yake, alipoanza kukoroma, Waridi aliamka taratibu, akanyata hadi uani ambako alilibeba kwa taabu jiwe kubwa alilokuwa ameliandaa mchana. Akaingia nalo hadi chumbani ambako Bomba alikuwa akiendelea kukoroma. Akakilenga barabara kichwa chake na kuliachia jiwe lile.

Bamba alikurupuka kutoka usingizini na kupaa juu, alipotua kitandani. Alitoa mlio wa maumivu kwa sauti ndogo nyembamba ambayo ilimwingia Waridi rohoni na kumtia ganzi. Kichwa cha Bomba kilikuwa kimefumuka. Ubongo uliochanganyika na damu ulikuwa ukivuja kitandani na kuchafua mashuka. Lakini bado aliendelea kutapatapa huku na kule, akisema hili na lile, maneno ambayo Waridi hakuweza kuyaelewa. Ni macho yake ambayo yaliweza kumtisha Waridi zaidi... Macho ya Bomba yalikuwa yakimtazama kwa namna ya huruma na kutoamini alichokifanya.

Waridi hakuweza kustahamili. Akapiga kelele kwa hofu akakimbia nje ya chumba hiki ambako aliketi chini akitetemeka. Baada ya muda, alirudi ndani ambako alimkuta Bomba tayari amekuwa marehemu; domo wazi, ulimi ukiwa umesahaulikwa nje, upande mmoja ilikuwa kama picha ya kusikitisha inayotisha mno. Waridi akaona shida kuistahamili. Akajikaza kiume kwa kumfungafunga marehemu Bomba kwa blanketi kubwa kisha akajaribu
 
SEHEMU YA 16

kumuinua ili amtoe nje. Hakufaulu. Akamvuta hadi uwanni. Huko akajitahidi na kuifikisha mati chooni ambako kulikuwa na tundu kubwa lililofunikwa na bati. Akalifunua bati hilo, na kumtumbukiza marehemu Bomba. Kisha akalifunika kama lilivyokuwa awali.

Wazo lake sasa lilikuwa moja tu; kuzihesabu pesa zake kikamilifu, Lakini mwujiza ulikuwa ukimsubiri. Mfuko wa pesa ulikuwa umetoweka. Haukuwepo tena juu ya kabati, ambapo aliuona kwa mara ya mwisho kabla ya kuutoa mzoga wa aliyekuwa mpenzi wake Bomba ndani. "Uko wapi?", Waridi alijiuliza huku akiutafuta mfuko huo kila kona ya nyumba bila mafanikio. Akabaki ameduwaa.

Mapambazuko yalimkuta bado kaduwaa katikati ya chumba, macho yakilitazama kabati kwa mshangao kana kwamba limeumeza mfuko huo wenye pesa. Waridi hakujua afuate lipi aache lipi.

Mara akajikuta akitoka nje ya nyumba hiyo. Alitembea kwa mkiguu hajui aendako. Baada ya kutwa nzima ya mzunguko usio na dhamira maalumu, Alielekea Mburahati ambako hakukawia kupata rafiki aliyemkarimu kwa kumsaidia kupata chumba cha muda. Baadae, Waridi alipata chumba chake. Siku zote moyo wake uliteswa na huzuni akikukmbuka kumwaga damu ya mtu asiyekuwa na hatia, hofu kwa kudhani kuwa wakati wowote polisi wangeweza kutokea kwa ajili ya kumchukua, na zaidi, maumivu makali moyoi kwa kuhisi ile sauti ya Bomba alipolia kwa uchungu na picha ya macho yake yalivyokuwa yakisihi.

Waridi hakuwa na la kufanya. Maisha yalimwendea vyema katika mazingira
 
SEHEMU YA 17

yake mapya, wateja wakimiminika kwa wingi hadi leo alipotokea mtu huyu wa ajabu ajabu ambaye anafahamu kila kitu kuhusu mkasa juu ya kifo cha Bomba.

"Siwezi... Siwezi kuua tena...?"Waridi alisema huku akibubujikwa na machozi.

"Huna ujanja, lazima utaua".

"Utaua?", Prosper alifoka kwa nguvu akiachia kofi kali ambalo lilimwingia Waridi kama aliyepigwa na kipande cha ubao. Akiwa msichana asiyezoea kupokea vipigo kutoka kwa wanaume, kofi hili lilimshangaza zaidi zaidi ya jinsi lilivyomwumiza. Lakini mshangao wake ulikoma pindi Prosper alipoongeza vipigo vingine vikali zaidi ambavyo vilimfanya Waridi ajikute akighalaghala chini damu zikimvuja hovyo kutoka usoni, puani na mdomoni.

Prosper akaangua kicheko, "Well", akasema, nilikuwa sikupigi ila tu ilikuwa kukuandaa katika hali ambayo itakufanya umpate Joram Kiango kwa urahisi. Yeye ni mtu anayevutiwa sana na mambo ya damu. Hivyo atakapokuona atajileta mwenyewe kwako. Utakachofanya wewe ni kuhakikisha umempata dawa ambayo nitakupatia, Baada ya muda mfupi atakuwa marehemu. Itaonekana kafa kwa magonjwa ya kawaida tu. Hakuna atakayefikiria kama wewe na mimi tunahusika na kifo chake",

Prosper alinyamaza kidogo akimwangalia waridi kuona kama maelezo yake yalikuwa yakimwingia, alipoona maneno yake yameanza kumwingia Waridi. Akaendelea. "Unaona iivyo kazi rahisi. Ni kazi ndogo tu. Inatofati sana na ile kubwa uliyofanya wakati ukimuua marehemu Bomba".

Moyoni Prosper aliwaza; Waridi angejisikiaje kufahamu kuwa yeye Prosper
 
SEHEMU YA 18

muda wote ule alikuwa nje akisubiri fursa ya kumuua Bomba! Kwani, Bomba ambaye alikuwa mmoja wa magaidi wake, alikuwa ameshindwa kutimiza kazi fulani aliyopewa. Badala yake alipanga kutoroka na pesa ambazo alipewa kwa ajili ya shughuli maalumu. Ndipo ilipodi Bomba auawe usiku ule. Ni Prosper pia aliyepeya hadi ndani na kuzichukua pesa zile baada ya kuona kazi aliyokusudia kuifanya ilikuwa imefanywa na Waridi.

Prosper aliitazama tena saa yake. "Bado dakika tano Waridi", Prosper alimwita Waridi, "Simama haraka ujiandae".

Kiasi fulani Waridi alikuwa hoi, hivyo alishindwa hata kusimama, lakini Prosper akamsaidia na kumwongoza nje ambako walipanda gari. Humo garini, Prosper alitoa amri nyingine ambayo Waridi hakuitegemea.

"Vua nguo zako zote".

Waridi aliduwaa na akasaidiwa kuzivua. Prosper hakusita kuzitatua.

"Nataka ufanye kazi nzuri tafadhali. Shika hii... Kamata na hii... Ni kazi ndogo sana... Kesho Joram Kiango atakuwa marehemu"?.


Baa hii ilikuwa imejaa watu wa kila aina; waliokuwa wakinywa na kustarehe kwa namna mbalimbali. Miongoni mwa watu hawa, alikuwemo Joram Kiango.

Yeye alitulia pale kaunta, juu ya stuli ndefu, pombe ikiwa wazi mbele yake, sigara ikiteketea mdomoni mwake. Kama ni furaha, yake ilikuwa tofauti na walevi ama wanywaji wengine. Hakusinzia hovyo wala kucheka pasipo sababu. Ukimya wake ulimfanya hata msichana wake Neema, ambaye alikuwa kando akinywa soda, amgeukie na kusema polepole.

"Tatizo lako ndio hilo, Joram. Uwapo huru unashindwa kuutumia uhuru
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom