Shule nane zimefungwa wilayani Kyela baada ya mafuriko ambayo yanatokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kuikumba wilaya hiyo na kusababisha maji kujaa kwenye vyumba vya madarasa,huku mito yote mikubwa ikiwa imefurika na kutishia usalama wa wanafunzi wakati wanapovuka mito hiyo kwenda shuleni.
Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Kyela ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo,Dk.Thea Merdad Ntara ndiye ambaye ameamuru kufungwa kwa shule hizo baada ya kujiridhisha kuwa usalama wa watoto upo hatarini kutokana na mafuriko hayo.
Athari za mafuriko hayo hazikuishia kwenye shule pekee,bali hata miundombinu ya barabara imedhurika na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa mawasiliano ya barabara, sambamba na baadhi ya wananchi nao kuathirika kutokana na makazi yao kujaa maji.
Akizungumzia athari za kibinadamu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Clemence Kasongo amesema kuwa mpaka sasa mtu mmoja amepoteza maisha na kwamba Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha madhara zaidi kwa binadamu hayatokei.
==============
UPDATE
Mpaka sasa jumla ya shule 10 zimefungwa zikiwemo za sekondari 3 na msingi 7 kwa muda usiojulikana kufuatia mafuriko wilayani Kyela,
Mkuu wa Wilaya ya Kyela Thea Ntara amethibitisha.