Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,591
- 1,191
SERIKALI YAJENGA DARAJA KUUNGANISHA VIJIJI VINNE MEATU, SIMIYU
Serikali Kupitia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) imetoa kiasi cha shilingi Mil. 197 kwa ajili ya kujenga daraja la Mto Makomangwa linalounganisha vijiji vinne vya wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.
Awali wananchi wanaozunguka vijiji hivyo walikuwa wanasombwa na maji na kusababisha vifo na pia walikuwa wanashindwa kusafirisha mazao huku wakikosa mahitaji ya kibinadamu nyakati za masika.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari, mara baada ya kamati ya Siasa kutembelea Mradi huo, baadhi ya wananchi wameipongeza serikali kwa kuwajengea daraja hilo ambalo litarahisisha mawasiliano na kuunganisha vijiji hivyo.
Adventina Njile, Mkazi wa Mikomangwa alisema daraja hilo likamilika litawasaidia kuvuka na kupata mahitaji upande wa pili na pia wanafunzi watakuwa wanawahi vipindi darasani.
Anthony Charles Mkazi wa Kijiji cha makomango alisema awali walikuwa wanashindwa kupaata mahitaji katika mji wa Mwandoa kutokana na mto huo kujaa maji.
Alisema wanaishukuru serikali kwa kuwajengea daraja hilo ambalo limekuwa kiunganishi baina yao na vijiji jirani na pia wanafunzi watakuwa wanakwenda shule bila adha yoyote.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa daraja hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Elieza Mayengo alisema mradi huo umegharimu shilingi Mil. 197 ambapo vijiji vya Mwandoya na Makomango vilikuwa vimekosa mawasiliano kutokana na mto huo.
‘’Kijiji cha Mwandoya, Makomango, Isangijo na Mwandu Itinje vimekosa mawasiliano kutokana na sababu ya mto huu ambapo usafiri na usafirishaji ulikuwa umekwama…tunaishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa daraja hili’’ alisema Mhandisi Mayengo.
Alisema baada ya daraja hilo kukamilika, kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya pamba na alizeti ambapo huko nyuma mto huo umesababisha vifo kwa wananchi wanaozungua eneo hilo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shemsa Mohammed aliwapongeza watendaji wa TARURA kwa kusimamia miradi ya barabara kwa viwango na ubora.
Aliwataka kusimamia na kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kukamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika ili kuboresha usafiri na kurahisisha mawasiliano baina ya Vijiji na Kata.