Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata wale wote waliotaka kusafirisha karafuu nje ya nchi kupitia bandari ndogo ya Kijiji cha Tondooni, Mkumbuu Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba hivi karibuni na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Akizungumza wakati alipotembelea Kituo Kikuu cha Karafuu cha Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) Wete kukagua karafuu zilizokamatwa, Dk Shein alisema uchunguzi ukifanywa kwa makini watu hao wanaofanya biashara ya magendo watapatikana kwa kuwa wananchi wanawafahamu.
Taarifa ya Ofisa Mdhamini wa ZSTC, Pemba Abdullah Ussi ilieleza kuwa Septemba 3, mwaka huu saa 11 alfajiri, askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) kilikamata viroba 17 vya karafuu kavu na vikonyo viroba vinne.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa baada ya uchunguzi karafuu hiyo ilikuwa imechanganywa na unga wa vikonyo uliosagwa pamoja na vipande, ambapo baada ya kupimwa karafuu hiyo ilikuwa na uzito wa kilo 549, wakati unga na uchafu mwingine, ulikuwa na uzito wa kilo 200.
Baada ya kuona uchafu huo uliochanganywa na karafuu hizo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema, vitendo hivyo ni lazima vipigwe vita kwa nguvu zote kwa kuwa vinaharibu sifa ya karafuu ya Zanzibar na alivitaka vyombo vya sheria kudhibiti hujuma hizo kwa kutumia Sheria ya Karafuu Namba 11 ya mwaka 2011 ambayo imebainisha adhabu dhidi ya watu hao.