Mwanzoni mwa mwaka huu benki ya Tanzania BOT ilitangaza kuwa itachukua hatua mbalimbali ili kutatua suala la uhaba wa dola ya Marekani uliotokana na upungufu wa sarafu hiyo kwenye akiba ya taifa. Uhaba huo umekuwa changamoto kwa biashara ya kimataifa kwa Tanzania, na kuifanya Tanzania ionje machungu ya uwepo wa ukiritimba wa sarafu moja kwenye biashara ya kimataifa. Benki hiyo imetaja hatua kadhaa za ndani ili kuhakikisha kuwa changamoto hiyo itaondolewa mwaka huu.
Changamoto ya upungufu wa akiba ya dola ya Marekani haikuikabili Tanzania peke yake, bali pia ilizikabili nchi mbalimbali za Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya. Changamoto hii imetatiza mwenendo wa biashara kwa nchi mbalimbali za Afrika, na hata kurudisha nyuma hatua za maendeleo ambazo nchi hizo imezifikia kwa taabu kubwa.
Tukichukulia mfano wa Kenya, gazeti la Bloomberg lilitangaza kuwa msukosuko wa uhaba wa dola ya Kimarekani ulikuwa dhahiri kwenye hasara iliyoonekana kwenye uwekezaji na mtikisiko wa soko. Dhamana za serikali ya Kenya zilipata hasara ya 2.1% tangu Julai 2023, wakati faharisi ya hisa ya Nairobi iliposhuka kwa asilimia 32, na kuifanya kuwa soko lililofanya vibaya zaidi kati ya masoko 92 ya kimataifa yanayofuatiliwa na Bloomberg.
Nchini Tanzania, wafanyabiashara walilazimika kusubiri malipo ya bidhaa zao hata mwaka mmoja baada ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi, na wale wanaoagiza bidhaa kutoka nje walishindwa kuagiza bidhaa hata za msingi ikiwemo mafuta ya kula na bidhaa nyingine muhimu, baada ya kushindwa kupata dola ya Kimarekani licha ya kuwa na shilingi ya Tanzania.
Msukosuko huo uliwakumbusha wachumi maana na umuhimu wa hatua ya China kutaka uwepo wa sarafu mbadala kwenye miamala ya kimataifa, ili kuepusha hatari za kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na ukiritimba wa sarafu za magharibi hasa dola ya Marekani kwenye biashara ya kimataifa. Hasara ya asilimia moja au asilimia mbili ya kiuchumi kwa nchi zenye uchumi dhaifu kama Kenya na Tanzania, inachukua muda mrefu kuweza kurekebishwa.
Mara zote China imekuwa mtetezi wa maendeleo ya nchi za Afrika, na inatambua kuwa mfumo wa kiuchumi wa kimataifa uliojengwa na nchi za magharibi umekuwa na vikwazo vingi kwa maendeleo ya nchi za Afrika, na moja ya vikwazo hivyo ni ukiritimba wa dola ya Marekani kwenye kufanya miamala ya kimataifa. Kwenye mfumo wa sasa unaotegemea dola ya Marekani, kama Marekani ikiamua kubadilisha viwango vya riba kutokana na sababu zake za kiuchumi au kisiasa, matokeo yake kwa uchumi wa nchi za Afrika yanakuwa mabaya. Na hii ni mbali na ada mbalimbali ambazo nchi za Afrika zinatakiwa kulipa kwa kufanya miamala ya kimataifa kwa kutumia dola ya Kimarekani.
Umuhimu wa uwepo wa sarafu mbadala sasa umekuwa wazi kwa nchi mbalimbali duniani, hasa kutokana na ukweli kwamba nchi hizo zimekuwa ni wahanga wanaopata hasara kutokana na utegemezi kupita kiasi wa dola ya Marekani. Kwa sasa Tanzania inaweza kuchukua hatua za ndani kuhakikisha inakuwa na dola za kutosha, lakini kukiwa na mbadala wa dola kutakuwa na usalama zaidi wa kiuchumi kwa nchi mbalimbali za Afrika.