Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Kgalema Motlanthe, anasema kuwa hana uhakika iwapo atakiunga mkono chama tawala cha African National Congress-ANC, kinachoongozwa na Jacob Zuma, katika uchaguzi mkuu ujao.
Bw Motlanthe ameiambia BBC kuwa, kura yake kwa ANC haifai kuchukuliwa kama 'iliyotiwa kwenye kapu' itapotimia uchaguzi mwaka wa 2019.
Bw Motlanthe, ambaye alihudumu kwa muda mfupi kama rais kati ya 2008 na 2009 na alikuwa wakati mmoja wa naibu wa rais Zuma, aliashiria kuwa alijaribu kumshawishi kiongozi huyo kuondoka mamlakani zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Aliongeza kuwa hafurahishwi na mtazamo wa baadhi ya mawaziri wa kutojali masuala ya uchumi wa nchi, huku waziri mpya wa fedha akijaribu kutuliza hofu katika mkutano wa Benki ya dunia mjini Washington (Ijumaa) kufuatia kushuka kwa kiwango cha uchumi nchini Afrika Kusini
Ijapokuwa Kgalema Motlanthe alikuwa kidogo asaliti chama chake ambacho amehudumu kwa miaka mingi, alisema kura yake kwa ANC "haingepeanwa" wakati wa uchaguzi mkuu mwaka wa 2019.
Ni mmojawapo wa viongozi wa kwanza watajika kushuku hali ya baadaye ya ANC chini ya uongozi wa Jacob Zuma ambaye alikuwa rafiki wake wa karibu katika uongozi.
Zuma atakumbana na kura ya kutokuwa na imani Bungeni mwezi ujao huku upinzani ukionekana kuwa mkali - ijapokuwa bado ana ushawishi mkubwa maeneo ya mashambani.
Atakayemrithi Zuma kama kiongozi wa ANC atachaguliwa na chama mwishoni wa mwaka lakini Kgalema Motlanthe amedokeza kuna haja ya dharura.
Alisema ANC " inazama kwa makosa iliyofanya ambayo yamefurika" na kutabiri kuwa kumuunga mkono kiongozi wake itamaanisha kwa uhakika kwamba ANC itapoteza utawala wa wengi katika uchaguzi miaka mbili zijazo.