Ngosha kapawa limbwata, hajiwezi mtimani,
Alivyo kama zezeta, kapoteza umakini,
Mwepesi kukunja ndita, kumlinda mwafulani.
Uchao azua vita, athama Bwana fulani,
Sasa kuna vutavuta, ndani hawaelewani,
Watu apeleka puta, kama mbuzi hitimani.
Hasikii wanoita, kiumbe hawezekani,
Pia hataki kuwata, watu wanayolaani,
Hebu fanyeni kumwita, wazee mwaogopani?
Haya hatukuyaota, wala hatukuyadhani,
Kama atawakung'uta, hata wake wa ubani,
Malaika tulopata, amegeuka shetani.
Hivi leo ameshuta, kachafuwa hewa ndani,
Tena ule wa tatata, kama honda la zamani,
Sasa yanalia mbwata, kisa kapata jamani.
Zinatosha beti sita, kalamu naweka tini,
Nachelea kunikuta, kama ya kamanda Beni,
Mkaanza nitafuta, kama vile marijani.
23 Machi 2017 Alhamis 21:08
JiniKinyonga
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whatsp 0622845394 Morogoro.