NDUGU NA MARAFIKI ZAKO NDIO MAADUI ZAKO WAKUBWA
Ndugu zako na marafiki zako wa karibu wanakupenda sana. Ndio maana mpaka sasa mpo karibu na mkishirikiana kwenye mambo mengi.Lakini hawa hawa ndugu na marafiki zako wa karibu, ni maadui wakubwa sana kwako.
KUWA MAKINI, WATU WENYE NIA NJEMA NA WEWE WANAWEZA KUWA MAADUI WAKUBWA.
Sio maadui kwamba wanataka kukuua au kukupoteza, hapana. Ni maadui kwa sababu wana nia njema sana na wewe. Katika nia hii njema wanageuka kuwa maadui.
Ndugu na marafiki zako ni maadui wako pale unapotaka kufanya kitu cha tofauti. Kitu ambacho hakijazoeleka.
Kitu ambacho kimebeba hatari kubwa. Watakushauri sana usifanye, watakusihi sana usiingie kwenye hatari hiyo. Watakupa mifano ya wengine waliojaribu kama wewe na wakashindwa. Na wewe utaona hawa ni ndugu zako au marafiki zako mnaopendana, na utawasikiliza, hutafanya, maisha yako yanabaki vile vile.
Maadui.
Ndugu na marafiki zako ni maadui zako wakubwa sana unapotaka kubadili tabia. Labda kuna tabia ambayo umejijengea, ambayo unaona ni kikwazo kwako kufikia malengo makubwa uliyojiwekea, kwa mfano kukutana kila jioni baa. Kwa bahati mbaya sana, tabia za aina hii hufanyi peke yako, bali na watu hawa wa karibu kwako.
Hivyo ili kuvunja tabia kama hizo, unahitaji kuacha kuwa na watu hawa wa karibu. Sasa utakapojaribu kufanya hivyo, watakuona umebadilika, unajitenga, hutaki kuwa nao na mengine mengi. Na wewe kwa kuogopa kuonekana wa tofauti au hujali, unarudi tena kwenye tabia ile, ukiona unawafanyia wema watu wako wa karibu. Maadui.
Sasa mchezo hauishii kujua kwamba hawa watu wema kwako wanaweza kuwa maadui wakubwa, mchezo mgumu kuliko wote ni wa kuweza kuwashinda maadui hawa. Kwa sababu hakuna vita ngumu kama ile unayopigana na adui anayekujua vizuri.
Anayejua uimara wako na madhaifu yako na watu wako hawa wa karibu watatumia vizuri madhaifu yako ili kuhakikisha huendi tofauti na mlivyozoea.Lakini kama wakale walivyosema, ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni, kwa kuwa sasa umeshawajua hawa ni maadui, na umeshajua wanatumia nini kuendelea kukufanya mateka, basi wakati mwingine utakapoamua kuondokana na kitu USIWAANGALIE USONI.
BAADAE WATAKUELEWA.