Urusi: waandamana kupinga matumizi mabaya ya madaraka
Polisi wanatuhumiwa kutumia nguvu kubwa kukabiliana na waandamanaji
Maelfu ya raia wamekusanyika katika maeneo tofauti nchini Urusi wakiandamana kupinga kile wanachodai matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mkusanyiko mkubwa upo katika mji wa Moscow ambapo shinikizo ni kumtaka waziri mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev kujiuzulu.
Wanaharakati wanasema kuwa hadi sasa watu 800 wanashikiliwa na Polisi.
Maandamano haya yanatajwa kuwa ni makubwa zaidi ya yale yaliyowahi kutokea nchini Urusi kwa miaka mingi, ambapo wanadai kuwa waziri mkuu wao Dmitry Medvedev amekuwa akutumia fedha za umma
katika mambo yake binafsi kwa kujenga majumba kifahari, kununua boti za kifahari, mashamba ya mvinyo na jumba la kufugia bata. Maandamano makubwa yalikuwa katika mji wa Moscow
Katika viunga vya Pushkin mjini Moscow, kuna kundi kubwa la waandamanaji waliokusanyika, mmoja wao amesema kuwa fedha za serikali zinaibiwa.
Marekani imeilaumu Urusi kwa hatua yake ya kuwashikilia mamia ya waandamaji kwa madai kuwa wanavuja haki dhidi ya maandamano ya amani kwa mujibu wa haki za binadamu.