Nampenda na Kumtakia Heri Paul Makonda

mcubic

JF-Expert Member
Mar 3, 2011
10,307
6,514
Ukiwa mzazi, hutampenda tu mwanao bali pia utamtakia heri. Hata mimi, sitaki mtu anipende tu, bali nimwone pia akinitakia heri.

Upendo wenye kutakiana heri ndiyo hasa upendo wenyewe. Ni upendo wenye kukosoana na kusahihishana, siyo upendo wa upofu, wenye kupotoshana na kuingizana shimoni.

Mzazi mwenye upendo wa upofu na kumwingiza mwanaye shimoni, humtetea mtoto wake anapokuwa anafanya mambo maovu. Mwana anaharibu mzazi anamkingia kifua.

Mzazi mwenye kumtakia heri mwanaye humkosoa anapokwenda nje ya mstari. Tena mzazi huwa imara na mkali sana anapoona mtoto anashika njia za hatari.

Wakati mwingine mtoto anapoona mzazi anakuwa mkali juu yake hudhani anamchukia. Tena anaweza kutamka baba au mama yake anamchukia. Kumbe hajui mzazi anamtakia heri, anaona anaelekea pabaya na hataki afike huko.

Hutokea mtoto kumwona mzazi wake anayemdekeza, asiyemkaripia, anayemtetea na kumuunga mkono hata kwa vitu vya kipuuzi kuwa ni mzazi mwenye upendo mkubwa. Baada ya kuharibikiwa ndipo hugundua kuwa kumbe mzazi wake alikuwa shimo lake.

Ni kama mzazi anapoona mwanaye ameharibika jumla au ameingia kwenye janga zito, ndipo huanza kujilaumu kwa tabia yake ya kumdekeza na kumuunga mkono hata kwa mambo mabaya.

Ukimpenda rafiki yako utamkosoa na kumsahihisha anapokosea kwa sababu unamtakia heri. Kama unataka atumbukie shimoni, utamuunga mkono na kumshabikia hata anapofanya mambo ya hatari.

NGOJA NITOE CHA UVUNGU

Iddi Amin Dada alipoivamia Tanzania, aliungwa mkono na watu wake wa karibu, walimpa kichwa. Muammar Gaddafi alimjaza upepo na kumpa msaada kuwa angeweza. Hawakumuonya kuwa alichokuwa anataka kukifanya hakikuwa sahihi.

Upepo ulijaa, Amin akaivamia Tanzania. Baada ya kukutana na kichapo kisha kuondolewa madarakani, ndipo alibaki akijuta maisha yake yote. Ukimpenda mtu lazima umtahadharishe, umpe angalizo na umkosoe.

Usidhani yanayompata Charles Taylor leo alikuwa hana watu waliomuunga mkono na kumwitikia kila kitu. Zingatia kuwa Taylor alipendwa na Waliberia haijapata kutokea kwenye nchi hiyo. Alishinda Urais kwa zaidi ya asilimia 75. Leo yupo jela maisha!

Laurent Gbagbo alipokuwa anagoma kutoka Ikulu ya Ivory Coast baada ya kushindwa na Alassane Ouattara, waliompenda pasipo kumtakia heri walimshangilia, walimwambia alivyokuwa ameamua ndiyo ilikuwa sawa.

Sasa hivi yapo wapi? Gbagbo na mkewe, Simone Gbagbo leo hii wapo jela. Mtu na mkewe walishauriana vibaya, watu wao wa karibu hawakuwaonya, waliwashabikia.

Ukisoma Biblia, utakutana na kisa kwamba Sauli yasingemfika makuu kama alipokuwa anafanya mipango hatari ya kumuua Daud, angekuwa anakosolewa na waliompenda. Wapambe wa Sauli wakiongozwa na Abneri walimsifu na kumjaza upepo.

Wanaompenda kwa kumtakia heri Yahya Jammeh, walimshauri aachie ngazi baada ya kushindwa na Adama Barrow, Gambia. Walijua angeendelea kung’ang’ania yangemfika makubwa.

Usipende mpaka ukapoteza uwezo wa kuona kasoro za unayempenda, ukiwa hivyo maana yake humtakii mema. Binadamu kwa upungufu wake, anahitaji watu wazuri wamsahihishe pale anapokosea ili awe bora kila siku.

NAMPENDA MAKONDA

Nampenda Makonda, namtakia heri. Alipotaja kwa mara ya kwanza majina ya watu aliowaita wauza unga, niliandika makala, nikaipa kichwa “SMS ndefu kwa RC Makonda kuhusu dawa za kulevya.”

Kama hujaisoma basi ipitie Facebook kwenye ukurasa binafsi na ule wa kijamii, jina ni Luqman Maloto. Utaona jinsi ambavyo nilionesha upendo mkubwa kwa Makonda.

Kwanza, nilimpongeza kwa ujasiri na nia yake njema aliyoionesha. Nilimwombea kwa Mungu, nikaahidi kuendelea kumwombea, nikamtaka naye awe na Mungu, maana vita aliyoichokoza gharama yake ni kubwa.

Pamoja na pongezi, vilevile nilimsahihisha kuwa jinsi alivyoanza tayari alikuwa ameshakosea, maana vita ya dawa za kulevya haiendeshwi kwa namna alivyoanza yeye. Vita ya dawa za kulevya haihitaji miluzi mingi.

Katika andiko hilo, nilieleza kuwa wauza dawa za kulevya wakubwa ni wataalamu wa kupoteza alama zenye kurahisisha wao kukamatwa. Hufanya biashara kwa njia ya ‘rimoti’.

Nilibainisha kuwa watumiaji na wauzaji wadogo wanapaswa kutumika kuwafikia wale wakubwa, vinginevyo ukiwafunga watumiaji na wauzaji wadogo, wale wauzaji wakubwa watatengeneza mtandao mwingine, hivyo kuendelea kuharibu kizazi cha Tanzania.

Shabaha ya kuandika siyo kujifurahisha, isipokuwa nina imani kubwa lazima imfikie na aisome. Hata ninapoandika kuhusu Rais wangu John Magufuli, bila shaka anafikishiwa na kusoma. Angalau hili nina uhakika nalo.

Kwa upendo mkubwa nilimtaka aanze upya kisha aendelee. Nilimtaka asiishie njiani ili aweke rekodi iliyotukuka.

Siku nne baada ya kuandika hivyo, Makonda alitokeza na orodha nyingine na kutangaza vilevile. Aliwataja Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, wafanyabishara maarufu, Yusuf Manji na Idd Azan, vilevile waliwepo wengine wengi.

Baada ya kumwona anarudia kilekile nilichomshauri asikifanye, niliandika kuwa Makonda ataweka rekodi ya dunia kisha dunia, ikiwemo mataifa makubwa kama Marekani watakuja kujifunza, maana niliona wazi anakosea na asingefanikiwa.

Sikukaa kimya, niliandika makala nyingine yenye kichwa “Kipeperushi cha dawa za kulevya kimfikie Rais Magufuli.” Ndani yake pia nilishauri mengi jinsi ya kuendesha biashara ya dawa za kulevya kwa mafanikio, vilevile kuwa na angalizo.

Nilimshauri Rais Magufuli asiamini mtu, maana wauza unga hujichomeka serikalini. Wauza unga hupenda kusingizia wenzao ili kujiweka salama.

Baada ya yote hayo, bado waliendelea kushikilia misimamo yao kuhusu mtindo wa kutaja majina.

UTANZANIA WANGU

Kama Mtanzania ninao wajibu wa kuijenga nchi yangu. Nikiwa na fahari kubwa kuhusu Utanzania wangu, ninayo tamaa ya kuona nchi yetu inaongozwa vizuri. Ndiyo maana nimekuwa nikiandika kwenye magazeti na mitandaoni, kupongeza, kushauri na kukosoa kwa namna ya kujenga.

Maandiko yangu ya awali kwa Makonda na Rais Magufuli, yalijengwa na imani kubwa kuwa dhamira ni mapambano dhidi ya dawa za kulevya na makosa yaliyofanyika ilikuwa bahati mbaya. Hivyo nilishauri cha kufanya kulingana na uelewa wangu.

Hata hivyo, nilipoona mtindo uliokuwa umeanzishwa ulikuwa unaendelezwa, huku Makonda akiweka mkazo kuwa alichokuwa anakifanya ni sahihi zaidi bila kutaka kujisahihisha, niliona dhahiri kuwa dhamira haikuwa dawa za kulevya, isipokuwa kitu kingine.

Ni imani yangu kuwa Makonda siyo wa kushindwa kujua kuwa ukimtangaza mtu kuwa ni mtuhumiwa wa dawa za kulevya kisha ukamwambia ajisalimishe baada ya siku mbili, hata kama ni kweli anahusika, hutampata na chochote, maana atapoteza ushahidi.

Suala la upelelezi ni la kitaaluma. Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro anajua kuwa hakuna upelelezi wa kumwita mtuhumiwa wa dawa za kulevya kituo cha polisi baada ya siku, kisha ndiyo uende naye nyumbani kumkagua.

Haya mambo yalinifanya nibadili mtazamo kuwa walikuwa wakifanya makosa kwa bahati mbaya au kutojua na kuona wazi kwamba walikuwa wanafanya makosa ambayo wanayajua.

Nikashika hili kuwa dhamira haikuwa dawa za kulevya, isipokuwa kuna lingine ambalo hatulijui ila wahusika wanalijua. Ni hapo ikawa na ulazima kuonesha wazi na kuweka mkazo wa kutokukubaliana na kinachofanywa.

Vema nifafanue hapa; mwandishi na mchambuzi hupaswa kutokuwa na upande pale palipo na hoja mbili au zaidi zenye kukinzana lakini zenye maslahi kwa nchi au jamii.

Mchambuzi anapaswa kutokuwa na upande kama kuna hoja mbili kuhusu Mungu. Ukristo unasema hivi, Uislamu unazungumza vile, Bundha wanatamka vile, Hindu kwa namna yao. Hapo ni Mungu, kwa hiyo hakuna kuelemea upande mmoja.

Hakuna mchambuzi anaweza kuitwa bora kama atakuwa anatengeneza mzani kati ya Mungu na Shetani, kwamba eti hataki kuwa na upande. Hakuna mzani wenye kukwepa upande kati ya dhambi na thawabu. Lazima mzani uegemee kwa Mungu na thawabu.

Nyakati ambazo nchi inaongozwa vibaya, wenye mamlaka wanaamua kutumia nafasi zao isivyofaa. Jicho la uchambuzi linaona wazi kuwa kuna makusudi ndani yake. Hapo mchambuzi lazima uchambue kulionesha kosa lilipo na siyo kupaka rangi upepo.

Vita ya dawa za kulevya jinsi Makonda alivyoianzisha na mahali alipoifikisha. Na kwa sababu makosa yalikuwa wazi tena ya makusudi. Maana yake ilitakiwa kuchambua kati ya uongo na ukweli.

Linapokuja suala la uongo na ukweli, mchambuzi hatakiwi akose upande, anapaswa kuusema ukweli kama ulivyo na kuushambulia uongo na rangi zake. Siyo kupepesa macho.

Mwandishi mashuhuri wa mashairi, Dante Alighieri, aliyeishi Italia kati ya Karne ya 13 na mwanzoni mwa Karne ya 14, aliandika: “The darkest places in hell are reserved for those who maintain their neutrality in times of moral crisis.”

Tafsiri yangu: Maeneo ya Jehanamu yenye giza totoro, yamehifadhiwa kwa ajili ya watu ambao wanabaki na msimamo wa katikati kipindi ambacho kuna utovu wa maadili.

Hapo Alighieri anafundisha kuwa palipo na utovu wa maadili hakuna katikati, isipokuwa ni kuusema ule utovu kama ulivyo.

Nami pamoja na kuunga mkono mapambano ya vita dhidi ya dawa za kulevya, nilipoona Makonda anakwenda nje ya mstari wa uongozi na Katiba yetu, sikuwa na namna zaidi kuyasema yale makosa.

Na katika kuyasema makosa haimaanishi unamchukia unayemsema au yupo unayemtetea, la hasha! Unayasema makosa ili yaachwe na ikiwezekana yasirudiwe. Hakuna kusimama katikati palipo na makosa.

Muhimu zaidi, unapomkosoa kiongozi, maana yake unataka aongoze kwa faida ya kila anayeongozwa. Kama kiongozi anakosea na unajiridhisha kuwa makosa yake siyo ya bahati mbaya, unapaswa kuyachambua makosa yake ili jamii inayoongozwa isalimike.

NAMTAKIA HERI MAKONDA

Nilipoandika makala “SMS ndefu kwa RC Makonda kuhusu dawa za kulevya” nilieleza kuwa nakubali yeye ni kiongozi na namheshimu, maana uongozi hutoka kwa Mungu.

Niliandika kuwa ni vizuri kumkosoa kijana kama Makonda ili kumjenga awe na maono bora zaidi ya uongozi. Maana Makonda kwa sababu ni kijana anaweza kulifaa taifa kwa miaka mingi ijayo.

Hivyo, ndani yangu natamani kuona viongozi vijana wanakuwa na maono bora ya uongozi kwa sababu wanayaishi maisha yenye kubeba kundi kubwa la rika, yaani vijana.

Inafikia wakati kijana kiongozi anatoa maneno makali ya kudhalilisha watu. Anatisha watu, jambo ambalo ni kinyume na Katiba. Hapo je, unatakiwa ubaki bila upande au umwambie kuwa anakosea? Na kumsema anakosea, haimaanishi una upande wa pili, isipokuwa upande wako ni ule ukweli unaouamini na kuusimamia.

Katiba ya nchi, ibara ya 17, imempa uhuru Mtanzania kwenda atakako ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufanya makazi, hatakiwi kufukuzwa wala kushurutishwa kuhama. Anatokea Mkuu wa Mkoa anasema atamfukuza mtu kwenye mkoa wake.

Je, kwenye eneo hilo unahitajika uwe na katikati? Ukifanya hivyo utakuwa kwenye kundi la watakaoingia kwenye giza totoro la Jehanamu kama alivyosema Alighieri. Unatakiwa usema hapana, hapo mkuu umepotoka, hatupaswi kwenda hivyo.

Kiongozi anasimama anataja majina ya watu na kuwatuhumu kuhusika na dawa za kulevya. Anataja kwa matangazo. Kumbe anataja bila hata kuwa na chembe ya ushahidi.

Duniani kote, kiongozi mwenye mamlaka, anapomtuhumu mtu mbele za watu, tena tuhuma kubwa kama dawa za kulevya, maana yake anamtangaza kuwa adui wa umma.

Muuza dawa za kulevya ni mtu hatari kwa umma, kwamba anaharibu nguvu kazi. Familia nyingi zimepata hasara kwa vijana wao kutopea kwenye lindi la matumzi ya dawa za kulevya.

Hivyo, unapomtangaza mtu kuwa ni mtuhumiwa wa dawa za kulevya ni wazi unamtambulisha kwa umma kuwa huyo ndiye adui yao. Maana kwa jamii kiongozi akisema tayari ni mapokeo. Ikitokea Mahakama kumweka mtuhumiwa huru, doa halifutiki.

Unamtangaza mtu wazi kuwa anahusika na biashara ya unga, unamwita polisi kana kwamba tayari ana hatia. Ibara ya 13, ibara ndogo ya 6 (b), imekataza siyo kwa kuremba, imetamka ni marufuku mtu anayeshitakiwa kwa kosa la jinai, kuchukuliwa kama mwenye hatia.

Ibara ya 13, ibara ndogo ya 6 (c), inatamka: “Kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai.”

Je, haki ipi ya usawa wa binadamu ambayo inakuwa imetunzwa kwa mtu kutajwa kuwa anauza unga pasipo ushahidi?

Ninapolisema hili, sina maana kuwa waliotajwa wote ni wasafi, la hasha. Shabaha ni kujenga hoja kuwa mkondo wa kisheria ufuatwe kwa mujibu wa taratibu zake.

Bila kumkosoa Makonda na kumwacha afanye alivyokuwa anafanya, maana ingejenga mazoea. Waswahili wanasema kawaida ni kama sheria. Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kingwangalla alisema anayo orodha ya mashoga. Naye angetaja!

Mwisho nchi inageuka taifa la viongozi wenye kuwadhalilisha raia wake. Katika orodha ya Kigwangalla umetajwa, naye anakutaja, unaitwa polisi na hujawahi kushiriki hivyo vitendo. Hata ukikutwa huna hatia, tayari ulishadhalilika.

Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa, Dag Hammarskjol, zaidi ya miaka 60 iliyopita, alisema: “Your position never gives you the right to command. It only imposes on you the duty of so living that others can receive your orders without being humiliated.”

Tafsiri yangu: Nafasi yako haikupi haki ya kutoa amri. Inaweka shinikizo juu yako la wajibu wa kuishi kwa namna ambayo watu wengine watapokea maagizo yako bila kujisikia wamefedheheshwa.

Hivyo, kwa vile namtakia heri Makonda, namtaka ajengeke katika mwongozo wa uongozi kama alivyosema Hammarskjol. Unaweza kuwa kiongozi mzuri bila vitisho. Unaweza kupambana na dwa za kulevya, kisha kukamata mapapa na kujenga heshima pasipo kudhalilisha wasiohusika.

AJABU YA TUHUMA

Narudia tena; mtuhumiwa wa dawa za kulevya huwa ni mtu hatari sana kwenye jamii. Anapotajwa na mamlaka za nchi, maana yake anakuwa ameshafanyiwa uchunguzi wa kutosha, kwa hiyo popote anapoonekana hutakiwa kukamatwa.

Huwezi kuona duniani kote, mtu ambaye ametuhumiwa kwa kutajwa na viongozi wa nchi kuwa muuza unga, aonekane karibu na viongozi wakubwa wa Serikali. Intelijensia inakuwa ipo wapi?

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai, vilevile kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, jana alikuwa msibani kwenye mazishi ya mama mdogo wa Rais mstaafu, Dk Jakaya Kikwete, anayeitwa Nuru Khalfan Kikwete.

Mbowe alionekana kwa ukaribu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Kikwete, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, vilevile Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Mbowe ni mtuhumiwa wa Makonda wa dawa za kulevya. Hivyo, kwa ukubwa wa tuhuma za dawa za kulevya, Mbowe hapaswi kuwa uraiani, achilia mbali kuwa na karibu mpaka na Waziri Mkuu wa nchi.

Hivyo, kitendo cha Mbowe kuwa karibu na viongozi wakubwa serikalini, kisha intelijensia kunyamaza kimya, ni uthibitisho kuwa tuhuma za Makonda zilitoka bila mpango mzuri.

Iwe akina Mbowe ni wasafi au si wasafi kuhusiana na dawa za kulevya, kwa sasa makosa yapo kwa Makonda kwa maonesho yake ya vita dhidi ya dawa za kulevya.

Aliwapa Watanzania matumaini makubwa mno, lakini imekuwa kazi bure, wote aliowataja wapo huru, waliofunguliwa mashitaka ni ya kutumia na siyo kuuza. Hilo ni kosa ambalo sikupenda lifanywe na kiongozi kijana.

Ndiyo maana msimamo wangu umenyooka kuwa kuwa Makonda anapaswa kuwaomba radhi Watanzania jinsi ambavyo aliendesha vita dhidi ya dawa za kulevya kwa mtindo wa kuwasaidia wahalifu. Matokeo yamekuwa hovyo kabisa.

NASISITIZA UPENDO

Nimeshazoea. Mimi huitwa mwana CCM kila nikikosoa vyama vya upinzani. Ninapoandika ukweli kuhusu Serikali pia huitwa mpinzani. Ni kama ambavyo ukimsahihisha Ali Kiba unaitwa Team Diamond, siku ukimgusa Diamond unaambiwa ni Team Kiba.

Huo ni udhaifu mkubwa ambao Watanzania tumeamua kuwa nao. Likiandikwa jambo halitafsiriwi kwa hoja zake, bali tafsiri inakuja ya ushabiki. Ukiona uniite CCM sawa, ukiniita mpinzani pia heri, ila nitaandika kwa ukweli ninaoupima mwenyewe, siyo kwa kupimiwa na watu.

Nampenda Makonda na kumtakia heri ndiyo maana nasema aombe radhi, kwa kufanya hivyo atawaonesha watu kuwa amegundua makosa yake, hivyo wakati mwingine akianzisha oparesheni atakuwa makini zaidi.

Nahitaji Makonda awe kiongozi mwenye kufanikiwa ndiyo maana namkosoa. Ambaye hampendi na hamtakii mema, ataendelea kumsifu hata kwenye mambo ambayo anakosea.

Naipenda sana Tanzania yangu, nawapenda na kuwajali Watanzania wenzangu, kwa hiyo anapotokea kiongozi anafanya ndivyo sivyo lazima nimsahihishe kwa maslahi ya kiongozi husika pamoja na nchi yetu kwa jumla.

Hili ni muhimu kulisema kwa mkazo ili watu waelewe bila shaka. Ukosoaji kwa Makonda ni kwa ajili yake binafsi pamoja na nchi yetu. Tunahitaji viongozi wazuri.

Kuhusu la kughushi cheti cha kidato cha nne ambacho Makonda anatuhumiwa kufanya hivyo ili kujipatia sifa ya kusoma elimu ya juu, hili lipo kwake.

Makonda anatakiwa kutusaidia sisi tunaompenda kwa kujibu yanayosemwa ili tupate nguvu ya kumtetea. Anavyokaa kimya, anatuweka kwenye wakati mgumu.

Je, yanayosemwa ni kweli? Atokeze ajibu kwa maelezo, maana wanaotuhumu wanatoa maelezo mengi yenye kutushinda nguvu sisi tunaotaka kumtetea.

Ndiyo maana msimamo wangu upo wazi kuwa ni ama Makonda ajibu tuhuma na kuondoa shaka ili atusaidie sisi tunaompenda na atupe nguvu ya kumtetea na kumjibia mashambulizi.

Ikiwa yanayosemwa ni kweli, basi isiwe nongwa, tukubali kuwa siri imebumbuluka, hivyo amsaidie Rais Magufuli kwa kujiuzulu nafasi yake. Hayo ni mawazo yangu mimi ambaye nampenda Makonda bila unafiki. Nampenda kwa kumtakia heri.

Ndimi Luqman MALOTO
 
kwanza story yako ni ndefu sana to read, ila ungekuwa au kama wewe ni mwanamke na umekiri kuwa unampenda basi ujumbe umefika na natmai atakupangishia nyumba na kukugeuza nyumba ndogo yake kama alivyofanya kwa masooooooooogan.......e
 
sijasoma insha yajo yetu kwa maana ni ndefu kupitiliza.
swali je wewe ni ke au me?
 
"Ukitaka kumficha Mtanzania jambo liweke kwenye maandishi" mtaalam mmoja alinena.
Nimesoma post. Comments za matusi are uncalled for. Watu wanataka ifupishwe. Hawasemi kwa kiasi gani.
Niwaombe wana jf wenzangu tuache matusi. Let's be objective. Kama hukubaliani na hoja, ikosoe kwa hoja. Ndivyo watu wasomi na wastaarabu hufanya.
 
Back
Top Bottom