JOHN Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amemvaa Justus Kamugisha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kwamba alikuwa mzigo,anaandika Moses Mseti.
Amesema, Kamanda Kamugisha ndiye aliyesababisha kuwepo kwa matukio ya uhalifu mkoani humo na kisha kushamiri.
Mongella alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na watumishi wa Halmashauli ya Wilaya ya Magu ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa watumishi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo.
“Huyu kamanda wetu (Justus Kamugisha) ndani ya wiki mbili tangu anaingia Mwanza, matukio ya uhalifu wa kutumia silaha yalizidi kuongezeka, ni bora umehamishiwa Mbeya labda huko ni kwepesi,” amesema Mongella.
Mongella amesema kuwa, Mkoa wa Mwanza hususan jijini Mwanza, matukio ya uhalifu yalikuwa tishio kutokana na kutokea mara kwa mara.
Hata hivyo, Mongella amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria Wakuu wa Polisi Wilaya watakaoshindwa kudhibiti vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe.
Chanzo: Mwanahalisi Online