Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira Waangazia Athari za Plastiki

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,091
1,094
Mkutano wa tano wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira (UNEA-5), unaendelea katika makao makuu ya UNEP jijini Nairobi. Mkutano huo ambao umewaleta pamoja mamia ya wajumbe kutoka nchi mbalimbali duniani, unajadili masuala mbalimbali kama vile marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki na uchafuzi wa mazingira yanajadiliwa.

Waziri wa Mazingira wa Kenya, Keriako Tobiko, ni miongoni mwa mawaziri waliohutubia washiriki kwenye ufunguzi wa mkutano huo, ambapo aliwataka wadau kutilia maanani masuala yanayoathiri mazingira, ikiwemo plastiki. Kulingana na waziri Tobiko, Kenya imepiga hatua kubwa sana katika vita dhidi ya mifuko ya plastiki na ameahidi kuwa sheria bado zitaendelea kubuniwa ili kutunza mazingira

‘Kupitia rasilimali chache tulizo nazo hapa Kenya, tumefaulu kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. Pia, haturuhusu aina yoyote ya mifuko ya plastiki karibu na hifadhi za wanyama, misitu na baharini. Kenya ina sheria ya usimamizi wa nishati endelevu,’ alisema Tobiko.

1646287713285.png

Khamis Hamza Khamis ni naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania (Muungano na Mazingira). Katika sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Khamis aliwasilisha ujumbe maalumu wa Tanzania kuhusu mazingira ambapo alieleza jitihada zinazokumbatiwa na nchi yake katika kukabilina na uharibifu wa mazingira.

Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kupambana na uharibifu wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki akisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo Tanzania imechukua hatua za kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji na matumizi ya mifuko hiyo.

Pia, naibu waziri huyo aliongeza kusema kuwa mwaka 2019 Tanzania ilitunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki huku akieleza kuwa ili kufanikiwa ushirikiano madhubuti wa kimataifa unahitajika ikiwemo sera ya pamoja na hatua za pamoja za kuhakikisha dunia inakuwa salama.

Aidha Khamis alisisitiza kuwa mbali ya jitihada hizo, Tanzania pia imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Inaelezwa kuwa takriban nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) zimepitisha maazimio yanayolenga kubuni makubaliano mwafaka ya kutokomeza taka za plastiki kwa kupunguza matumizi yake kutoka vyanzo vyake hadi baharini.

Aidha, wadau kwenye mkutano huo wanatarajia kufikia maamuzi ya pamoja katika hatua za mwanzo za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki ambayo inatajwa kama chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya chupa za plastiki milioni moja hununuliwa kila dakika kote ulimwenguni kwa matumizi ya maji ya kunywa huku mifuko ya plastiki zaidi ya trilioni 5 hutumiwa kila mwaka duniani.

Inger Andersen ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la UNEP anasema kwamba ni sharti mataifa yashirikiane kwa kauli moja ya kutokomeza matumizi ya plastiki ili kuhifadhi mazingira.

"Swala kuu katika linalojitokeza katika mkutano huo wa Baraza la UNEA ni kuhusu taka za plastiki. Tunayo mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambao wamepitisha maazimio yanayolenga kubuni makubaliano mwafaka ya kutokomeza taka za plastiki kwa kupunguza matumizi yake kutoka vyanzo vyake hadi baharini,’’ alisema Andersen.

1646287702453.png

Wajumbe hao, wakiwemo mawaziri, wanadiplomasia na wanaharakati kutoka makundi ya kutetea uhifadhi wamazingira wanapania kufikia haraka maamuzi ya pamoja katika kukabiliana na tatizo sugu la uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki.

Andersen anasema ana matumaini kuwa mkutano wa baraza la UNEA unafikia suluhu la kudumu.

"Tunataraji kuwa mkutano wa UNEA utafikia maamuzi ya kihistoria katika kukabiliana na swala la taka za plastiki kama vile makubaliano ya Paris yalivyokuwa kwa mabadiliko ya tabia nchi,” Andersen aliongeza.

Mkutano wa UNEA 5 uliofunguliwa Februari 28 unatarajiwa kuhitimishwa Machi 2, 2022 huku ukijumuisha wadau wakiwemo mawaziri na wadau mbalimbali wa mazingira duniani.
 
Back
Top Bottom