Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,742
- 40,873
Mwaka 1743 Siku ya Jumatano tarehe 13 Aprili alizaliwa Thomas Jefferson. Alizaliwa wakati Marekani ikiwa ni koloni la Waingereza. Thomas Jefferson alikuwa ni Rais wa tatu wa Marekani baada ya George Washington na John Adams. Alikuwa pia ndiye Waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje wa Marekani (Secretary of State) chini ya Rais George Washington. Historia inamtambua kama mtunzi mkuu wa Azimio la Uhuru (Declaration of Independence) ambamo ndani yake maneno yale maarufu ya kuwa “Binadamu wote wameumbwa sawa, na wote wamejaliwa na Muumba wao haki kabisa zisizoondosheka ambapo miongoni mwao ni haki ya uhai, uhuru na kutafuta furaha”.
Jefferson alikuwa ni mwanafalsafa, mwanasayansi na mwananadharia za kisiasa ambaye msimamo wake umeacha msingi mkubwa wa maisha ya kisiasa katika Marekani. Yeye pamoja na kina Washington na wenzake wanatambulika kama “Mababa Waasisi” (Founding Fathers) wa Marekani. Pamoja na utunzi wake wa Azimio la Uhuru ambalo lilianisha sababu ya Wamarekani kukataa kuwa chini ya himaya ya Waingereza Thomas Jefferson aliandika maandishi mengine mengi na wakati mwingine alipingana hata na waasisi wenzie. Mchango wake katika fikra na maisha ya Wamarekani ni mkubwa sana.
Pamoja na hayo yote Jefferson alikuwa binadamu. Alikuwa na matatizo yake na mapungufu ambayo historia inayatambua; licha ya kwamba alitunga yale maneno kuwa “binadamu wote wameumbwa sawa” yeye mwenyewe alikuwa na watumwa takriban 150; usawa wao ulikuwa wapi? Alikuwa hapendi mahusiano ya mapenzi ya watu wa rangi tofauti (interracial relationships) lakini yeye mwenyewe inaamini kuwa alikuwa na mpenzi hadi kuzaa naye mtumwa wake mmoja mweusi – Sally Hemingway.
Ukweli huo wote na mapungufu yake yote hayaondoi ukweli wa mchango wake kwa taifa lake na kwa Jimbo lake la Virgnia ambako alionesha jinsi alivyothamini elimu kwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Virginia na maktaba na vitu vingine vingi – ikiwemo mfumo wa elimu wa utatu (tertiary education system). Jefferson hakumaliza yote yaliyoikabili nchi yake, miaka hamsini tangu kuandikwa kwa maneno yale ya Azimio Jefferson alifariki akiwa na miaka 83 – siku hiyo hiyo Rais aliyemtantulia John Adams naye alifariki huko Boston (siku ya Julai 4, 1826). Ilikuwa ni Sikukuu ya Uhuru wa Marekani.
Miaka 179 baadaye, mbali kabisa kutoka Marekani katika iliyokuwa koloni la uangalizi la Waingereza la Tanganyika. Siku ya Alhamisi tarehe 13 Aprili, 1922 alizaliwa Julius Kambarage Nyerere. Alizaliwa chini ya utawala wa Waingereza. Julius Nyerere naye alipoingia kwenye siasa alijikuta anatambua jambo ambalo Jefferson naye alishalitambua; Nyerere aliweka mawazo yake katika Azimio la Arusha ambalo mtunzi wake mkubwa alikuwa yeye mwenyewe na sehemu yake ya kwanza inatangaza kuwa “binadamu wote ni sawa”.
Tofauti na Jefferson, Nyerere aliona usawa huu siyo suala la kuumbwa tu ni usawa unaotokana na utu wao. Kwamba, bila kujali rangi, kabila, dini n.k binadamu wote wana utu sawa. Nyerere yeye alienda mbali zaidi na kuhakikisha kuwa – tena kama kanuni – kwamba “kila mtu anastahili heshima”. Wakati Jefferson alifungwa na mazingira ya wakati wake ambapo utumwa ulikuwa unakubalika nay eye mwenyewe akiwa na watumwa Nyerere alikataa mapema kabisa ubaguzi wa rangi kwani unapingana na msingi huo wa kwanza kuwa binadamu wote ni sawa. Ni kwa sababu hiyo aliweka kama madhumuni ya TANU ya wakati ule kuwa mojawapo ya malengo ya TANU kama chama cha kupigani Uhuru ilikuwa ni “Kuona kwamba Serikali inatoa nafasi zilizo sawa kwa wote, wake kwa waume, bila kujali rangi, kabila, dini au hali;” na “Kuona kwamba Serikali inaondoa kila namna ya dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa na upotofu” (Neno “upotofu” lilivyotumika hapa wakati huo ndivyo tunavyomaanisha leo tunaposema “ufisadi”).
Viongozi hawa wawili wote wanapaswa kuangaliwa kwa zama zao. Wakati mwingine unaweza kukuta unahukumu vikali bila kujali maudhui ya kihistoria (historical context) ya viongozi hawa. Mojawapo ya mambo ambayo nimekuwa nikiyaangalia sana ni jinsi gani vijana au hata watu ambao hawajachukua muda kusoma na kumwelewa Nyerere wanakuwa wepesi sana kuhukumu kwa ukali. Ni sawasawa na mtu kusema kuwa Jefferson alifeli uongozi wake kwa sababu hadi anakufa utumwa ulikuwepo! Au kusema kuwa alifeli kwa sababu hakuweza kuondoa matatizo yote ya Wamarekani; hakuweka misingi yote ya utawala na kuhakikisha viongozi wanaokuja hawafanyi lolote jingine kwani lote lililohitajika kufanywa lilifanywa na Jefferson. Hii siyo haki kwa historian a hata kwa mtu mwenyewe.
Kuna watu ambao wangependa kuwa Nyerere angekuwa amemaliza kutengeneza mifumo yote, kuandaa viongozi wote (kwa miaka mia ijayo) na kutatua matatizo yote ambayo alikutana nayo. Kwamba, kila mtu angekuw ana nyumba nzuri, barabara zingekuwepo, umeme hadi wa kumwaga n.k Kwamba kwa vile alipokufa Tanzania bado ilikuwa ni nchi maskini basi ndugu zetu hawa wanasema tu kuwa “alifeli”.
Leo hii inawezekana anazaliwa Mtanzania mwingine, mtu mwingine ambaye anaweza kuja kutoa mchango mkubwa sana katika maisha ya Taifa letu huko mbeleni. Changamoto ambazo leo zipo zinaweza kumalizwa na sisi; lakini haina maana hakuna changamoto nyingine zinazoweza kuja huko mbeleni. Anayedhani Magufuli – pamoja na jitihada zote anazofanya – atamaliza matatizo yetu yote naye huyo ni muota ndoto. Magufuli atafanya kwa kadiri ya uwezo wake na kwa kadiri ya zamu yake. Na yeye kama ilivyokuwa kwa Jefferson na Nyerere – naye ana mapungufu yake. Mapungufu haya hata hivyo hayamfanyi apoteze mwelekeo au aone hafai kufanya lolote.
Hivyo, kwa sisi mashabiki na wanafunzi wazuri wa Mwalimu leo ni siku ya kutafakari mchango wetu wa kifikra kwa taifa letu. Tunamshukuru Mungu kwa kutupa mtu ambaye ameacha alama ambazo leo zinakumbukwa katika taifa letu.
#TunakukumbukaMwalimu