RAIS John Magufuli jana amewatunuku Kamisheni ya Luteni Usu, maofisa wanafunzi 205 pamoja na kutoa Nishani kwa maofisa watano waliofanya vizuri kwenye masomo yao katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) kilichopo mkoani Arusha.
Miongoni mwa maofisa hao watano waliotunukiwa nishani, wapo wanawake wawili ambao ni Efrasia Bundala kutoka Tanzania na Winnie Indumuli kutoka Kenya, na wanaume ni Phinias Kiganga, Frank Kitalekwa na Ahmed Mmang’anda.
Baada ya kuwavisha Nishani askari hao watano, ambao ni miongoni mwa maaofisa wapya 205, Rais Magufuli aliwatunuku Kamisheni ya Luteni Usu maofisa hao wapya ambao miongoni mwao wapo wanawake 16 na wanaume ni 189.
Miongoni mwa wahitimu hao, wawili wanatoka nchini Burundi wanne nchini Kenya na wengine wanne wanatoka nchini Uganda. Mara baada ya kutoa Kamisheni kwa maofisa hao, burudani kutoka kwa Kikundi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Oljoro ilitolewa, ikiwemo wimbo wa kumpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi.
Waimbaji hao wamemuomba Rais Magufuli kusafisha wabadhirifu wote, wakwepa kodi taasisi mbalimbali, ili Tanzania iwe safi.
Waimbaji wa Bendi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iitwayo Chacharika, ilikonga nyoyo za wananchi waliofurika kushuhudia ndugu zao wakitunukiwa Kamisheni, walipokuwa wakimpongeza Rais Magufuli kwa utoaji wa elimu bure.
Awali akiingia uwanjani kwa ajili ya ukaguzi wa gwaride, Rais Magufuli alishangiliwa na wananchi mbalimbali, viongozi wa Serikali pamoja na wageni waalikwa waliohudhuria sherehe hiyo.