Kutana na mwanamke aliyejifanya mwanaume kwa miaka kumi ili afanya kazi mgodi wa Tanzanite

Ukishangaa ya Mussa utayaona ya firauni.



Ni msemo unaojidhihirisha katika maisha ya zaidi ya miaka 10 ya Pili Hussein (55), mwanamke anayejulikana zaidi kwa jina la utani la “Mjomba Hussein” ambaye sasa ni muajiri.

Mjomba Hussein alimudu kuishi kwa kipindi hicho chote akijifanya mwanaume, akitumbukia ardhini katika mgodi wa Mirerani kusaka madini wakati wanawake hawaruhusiwi. Yote hayo aliyafanya bila ya kujulikana kuwa ni mwanamke. Lakini baada ya kufanikiwa kupata jiwe la Tanzanite aliloliuza kwa Sh100 milioni, sasa ni mfanyabiashara na mkombozi wa vijana na wanawake wengine.

Akizungumza katika tamasha la 14 la jinsia lililofanyika katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia (TGNP), mwanamke huyo alisimulia jinsi alivyoishi maisha hayo wakati akitaka kutimiza ndoto zake kimaisha kuondokana na umaskini.

Pili alisema kilichomsaidia kuishi bila kujulikana ni mavazi yake ya kiume, sauti nzito na umbile la kifua chake ambacho hana maziwa makubwa, hivyo kuonekana kama mwanaume na kumudu kuingia mgodini tofauti na wanawake wengine.

“Walikuwa hawataki wanawake, kwa hiyo nilichofanya ni kunyoa zungu (upara), kuvaa makofia makubwa, kaptula na mavazi ya kimasai wakati mwingine,” alisema. Huku akishangiliwa na wanachama wa TGNP, mwanamke huyo alisema alianza kazi ya uchimbaji madini kama mwanaume halisi.

“Nilikuwa nainua nyundo ya kilo 15, napasua miamba na wakati mwingine nawasaidia wanaume kwa sababu walikuwepo ambao hawakuwa wakiweza kuingia mgodini kwa kamba,” alisema.

Akiwa na umri wa miaka 31, Pili aliamua kwenda mgodini kutafuta kazi huku akijifanya mwanaume.

“Kabla sijaenda mgodini nilikuwa nimeolewa na mwanaume wa kichaga. Kama mnavyojua, niliachwa kijijini na mume wangu aliyeenda kutafuta maisha. Nilikuwa na mtoto mmoja nikaamua kumpeleka kwa wazazi wangu,” alisema.

Pili, ambaye hakuwahi kusoma hata darasa moja kutokana na baba yake kumpa kazi ya kuchunga ng’ombe tangu akiwa mdogo, alisema pamoja na kuwa mwanamke hakuwahi kuonewa katika miaka yote aliyoishi mgodini.

“Nikimaliza kazi zangu za uchimbaji wa madini, nilikuwa narudi kwangu. Maisha yanaendelea,” alisema.

“Kuna wakati tulikuwa tunatakiwa kwenda kuoga wote, nilichokuwa nafanya ni kuvaa kaptura na nguo ya juu. Hawakunijua hata kidogo.”

Alisema maisha yake ya kibabe yaliwafanya wanaume kuwa wanamuogopa na mara zote aliwatetea wanawake hasa wanaofanya biashara kwenye maeneo hayo ya migodi. “Walikuwa wananiogopa, sikuwahi kuchezewa na nilishiriki kila kitu ambacho wanaume walikifanya,” alisema.

Ili asijulikane, alienda kwenye maeneo yanayouzwa pombe na kuwanunulia wenzake bila yeye kunywa.

“Nilikuwa na mirungi kwenye mifuko yangu ya kaptura na mtu akiomba nilimpa. Pamoja na kujifanya hivyo sikuwahi kuonja, kwa sababu kiuhalisia niliigiza tu,” alisema.

Jiwe la Tanzanite

Jitihada zake zilizaa matunda, alifanikiwa kupata jiwe la Tanzanite lililokuwa na thamani ya Sh100 milioni.

Hapo aliweza kupunguza baadhi ya matatizo yake na familia yao.

“Baba yangu ana wake sita, hivyo kila mwanamke nilimjengea nyumba,” alisema Pili. “Nikanunua trekta na hivi nizungumzapo nimefanikiwa kuwasomesha zaidi ya watoto 30, baadhi yao wapo chuo kikuu.” Akimzungumzia Pili, mwenyekiti wa wanawake wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini, Sara Lusambagora alisema kuthubutu kulimsaidia.

“Ili kuingia mgodini lazima ujitose na mazingira magumu ya huko yanawafanya wanawake wasiingie kabisa. Hivyo huyu mwanamke ni mfano kwetu na kwa wanawake wote Tanzania,” alisema.

Naye mwenyekiti wa shirikisho hilo, Doreen Kissia alisema aligundua Pili ni mwanamke baada ya kesi ya ubakaji.

“Siku zote nilikuwa nikijua ni mwanaume. Hili lilitushangaza sana na kwa kweli amekuwa mwanamke wa mfano na ameajiri zaidi ya vijana 70,” alisema.

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi alisema tamasha hilo limelenga kuwafundisha wanawake namna ya kujituma, kutafuta fursa na kuona namna ya kusaidiana hasa kwa wale waliofanikiwa.

Tuhuma za kubaka

Maisha yake mgodini hayangeweza kudumu milele bila ya kugundulika. Sifa yake kubwa ya ubabe ndiyo iliyotafutiwa sababu iliyomtoa mgodini.

Alisema kuna watu ambao walikuwa wavivu na mara nyingi walikuwa wakimsumbua. Watu hao ndio waliomchukiza hadi akaamua kufanya kitendo kilichokuja kugeuzwa kuwa ni ubakaji.

“Siku hiyo nilichukua mayai nikawapiga nayo kwenye makalio yakapasuka. Kwa sababu walikasirika, wakanibadilikia na kunisingizia kuwa nimewabaka,” alisema. Alisema tuhuma hizo zilisababisha akamatwe na mgambo na kupelekwa kituo cha polisi ili baadaye ashtakiwe.

“Nikiwa polisi niliwaambia wanikague, lakini nilitaka mwanamke ndiye afanye kazi hiyo. Polisi walikubali na maajabu yake wakashangaa mimi si mwanaume,” alisema.

Ndoa ya uongo

Maajabu ya Pili hayakuishia kujifanya mwanaume ili afanye kazi mgodini tu, bali hata kuoa mwanamke mwenzake.

Katika maeneo ya migodi kulikuwa na mwanamke ambaye alikuwa na watoto wadogo akihangaika kupata kazi walau ya kumuwezesha kuishi na watoto wake.

“Nilimuhurumia, nikajua kama nikimuacha anaweza kupotea na mwisho watoto wakateseka,” alisema.

“Nilimwambia nataka kumuoa, naye alikubali nikamjengea nyumba ndogo akaanza kuishi kwangu.”

Lakini anasema hakuwahi kuvua nguo mbele ya mwanamke huyo hata siku moja.“Akitaka haki ya ndoa, namwambia amekuja kutafuta (fedha) kwa hiyo aachane na masuala hayo. Tuliishi na alinizoea hivyo. Cha ajabu hakuna mwanaume aliyemgusa kwa sababu wote walijua ni mke wa Mjomba Hussein,” alisema.

Hata hivyo baada ya kesi, mwanamke huyo aligundua siri hiyo.



Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom