Kisa cha Kweli: Sitasahau nilivyopendwa na mchawi nikaishia kurogwa

Mr the dragon

JF-Expert Member
Apr 14, 2017
1,938
3,703
Nimeamua kushare hapa hiki kisa cha kweli kilichonitokea kwenye maisha yangu. Nikiamini wengi mtajifunza na kuburudika pia.

NB: Majina ya watu na baadhi ya Majina ya sehemu yatakuwa sio halisi ili kuficha indetity yangu. Pia sio mwandishi mzuri Ila nitajitahidi kuandika kwa mtiririko mzuri.

Naitwa Mr the dragon ni mzaliwa wa wilaya ya Bunda mkoa wa Mara. Nilizaliwa katika hospitali ya Bunda district designated hospital (DDH) katikati ya miaka ya tisini, yaani miezi sita kabla ya kifo cha 2pac na miezi miwili kabla ya kuzama kwa Mv Bukoba. Ukiwa pale ilipo Crdb bank kwa sasa ndio maeneo niliyozaliwa.

Nikiwa ndio kwanza nina umri wa miaka mitano. Baba yangu mzazi aliugua kichaa, namaanisha alianza kupata uwendawazimu ikabidi apelekwe kwa waganga wa kienyeji. Baba yangu alikuwa ni mfanyabiashara aliyejulikana vizuri mitaa hiyo. Japo baadae alikuja kupona, lakini mpaka sasa imebaki ni kitendawili juu ya chanzo cha ugonjwa ule wa akili. Inasemekana ni mkakati maalumu ulioandaliwa na baadhi ya wafanyabiashara wenzake ukitaka wafanyabiashara wote waliovuka rubana warudi kwao. Mkakati huu ulihusisha imani za kishirikina, wafanyabiashara baadhi waliovuka mto rubana kuja bunda walipoteza maisha. INASEMEKANA LAKINI!!!

Mhenga aliyesema mwanaume ni kichwa cha familia hakukosea. Baada ya baba kuugua mambo yote yaliharibika maisha yalituchapa kwelikweli. Ikabidi mama achukue familia kurudisha nyumbani kwao, yaani kwa Babu yetu mzaa mama. Nyumbani kwao na mama ni mkoa wa Simiyu wilaya ya Busega kijiji cha Mwanono (Sio jina halisi). Mimi na kaka zangu na dada zangu tukaanza kuishi kwa Babu, kipindi hicho nina miaka minane nikiwa darasa la pili.

Babu yangu aliitwa mzee Manumbu alikuwa very prominent pale kijijini. Kijana wake wa kiume yaani mjomba wetu (kaka mama mmoja na mama yangu) alikuwa na cheo kikubwa serikalini. Alimjengea babu nyumba nzuri kijiji kizima, alimnunulia ng'ombe wengi na trekta jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa matajiri wa kile Kijiji. Babu yangu alikuwa na wake sita walioishi sehemu moja, jambo lililofanya awe na familia kubwa sana. Watoto wake na wajukuu tulikuwa wengi sana tulioishi pale.Mabinti wa Kijiji kile na vijiji jirani walitamani kuolewa kwa mzee Manumbu.

Nakumbuka mwaka uliofuata 2005 nikiwa darasa la tatu siku moja mama yangu alialika kikundi cha watu wa kulima. Kwa jina maarufu kwa kisukuma huitwa "Luganda". Alialika hicho kikundi wakamlimie palizi ya pamba. Kikundi hiki kilitumia zeze na ngoma pindi wakiwa wanalima ili kupandisha mzuka watu wasichoke wakiwa wanalima. Muda wa usiku nikiwa nimelala nilisikia sauti ya ngoma na vifijo nje ya nyumba. Nilifikiri ni wale wa kikundi wamekuja kuwapitia watu wa nyumbani waende shamba. Nilikurupuka kutoka nje ili nikawaone wanavyocheza.

Nilifungua mlango nikiwa na shauku kubwa. Nilipofungua niliona kundi kubwa la wanawake na wanaume wanaimba na kucheza katikati ya uwanja wa pale nyumbani wengine wakiwa uchi, wengine wamevaa nguo nyeusi. Kwanza nilipigwa na butwaa na kujikuta nikikaza jicho langu kuangalia wanavyocheza. Baadae ndipo wazo la kwamba wale ni wachawi ndio lilikuja akilini, nikatimua mbio kurudi ndani nikajifunika shuka gubigubi. Cha ajabu niliporudi ndani tu zile ngoma zilikoma, niliogopa sana japo sikufanikiwa kumtambua yeyote katika kundi lile.

Kesho niliamka mapema ili niwahi kuhesabu namba shuleni, lakini nilisikia maumivu kwa mbali kwenye mguu. Kuangalia nikaona nilikuwa na kidonda mguuni japo sio kikubwa Sana. Nilijiuliza nimepata wapi hicho kidonda lakini sikupata jibu. Nikikumbuka hata jana yake usiku sikujigonga wala kujikwaa popote wakati nakimbia. Niliogopa sana lakini sikuwa na jinsi niliendelea na kunawa miguu na uso niende shule. Wakati tukiwa tunatoka kwenda shule mimi na ndugu wengine tulisikia taarifa mbaya. Mjomba wetu (kaka wa mama tofauti na mama yangu) aliyekuwa anakaa pale nyumbani alikuwa amechanjwa Chale mgongo mzima. Niliogopa sana nikawa natamani kusimulia nilichokiona usiku, ila kila nikijaribu napata uoga sana... Sikuzungumza chochote

Baadae tulienda shule, siku hiyo sikuwa na raha kabisa ukizingatia matukio yaliyotokea nyumbani. Kikubwa zaidi kilichoniogopesha ni hiki kidonda ambacho sikujua kimetokea wapi. Wakati nikiwa darasani binti mmoja tuliyekuwa tunasoma nae darasa moja alinifata, binti huyu bibi yake alikuwa ni mchawi aliyeogopeka zaidi pale kijijini. Ujio wake haukunishangaza kwa sababu nilimchukulia kama ndugu yangu, na mara nyingi tulikuwa tunapiga story. Nilimchukulia kama ndugu kwa sababu kaka wa huyo bibi yake alikuwa ni rafiki mkubwa wa baba yangu mzazi. Hata bibi yake yaani mchawi aliyeogopeka nilikuwa nikimuita shangazi. Alipofika aliniambia

" Mr the dragon kumbe ni muoga vile, nilikuona usiku ulivyokimbia kurudi ndani. Sisi tulienda kwenye mkwaju wa kwa lugota kula nyama"

Mkwaju wa kwa Lugota ulikuwa ni mti wa ukwaju mkubwa na mnene sana uliokuwepo pale kijijini.

Nilimuangalia tu nikakaa kimya, sikuzipendelea story zake kwa sababu nilikuwa naogopa sana.

Itaendea kesho...
 
Ukimaliza nitag hauchelewi kuimalizia kati
 
Huu upuuzi wa kusema ntaendelea kesho ni ukosefu wa maarifa na ulimbukeni wa hali ya juu sijui kwanini baadhi ya watu wa wasukuma hamtaki kuenda na wakati
Nashauri huu uzi ufutwe mapema foolish
 
Inaendelea! Sehemu ya 2

Niliendelea na ratiba zingine za shule kama kawaida. Ilipofika mchana saa sita nilirudi nyumbani kupata chakula cha mchana, kisha nikarudi tena shule kwa ajili ya vipindi vya jioni. Wakati wa kutawanyishwa jioni ulipofika nilirudi nyumbani kama kawaida, nilienda moja kwa moja hadi chumbani nikabadilisha nguo kisha nikatoka kwa ajili ya kwenda kucheza mpira. Wakati nikiwa ninatoka nilikutana na mtoto wa mama mdogo ambaye tulikuwa tunaishi nae pale nyumbani akanambia.

"Babu anakuita kule" alisema huku akinionyesha kwenye nyumba ya nyasi ambayo ilikuwa nyuma ya nyumba kubwa. Nilienda moja kwa moja hadi ndani ya nyumba. Nilivyoingia nilikuta ndani kulikuwa na watu watatu. Kulikuwa na Babu, mjomba Elias (yule aliyechanjwa chale usiku uliopita na mzee mmoja aliyekuwa amevaa kibagarashia ambaye sikumtambua. Niliwasalimia, nikamaliza nikauliza " Babu Elikana ameniambia unaniita" Babu aliniambia kaa hapo chini. Nilikaa chini nikatega sikio kuwasikiliza.

Kumbe yule mzee mwenye kibagarashia alikuwa ni mganga wa kienyeji. Baada ya mjomba kuchanjwa chale Babu alimpeleka kwa mganga kuangaliwa kama kutakuwa na shida yoyote. Kule kwa mganga waliaguliwa, halafu yule mganga akawaaambia Babu na mjomba nimeona kuna mtoto hapo kwako wachawi walimfanyia jambo jana. Sasa hilo jambo ambalo mganga aliwaambia nimefanyiwa ndio ilikuwa sababu ya mimi kuitwa pale.Babu aliniangalia machoni halafu kwa sauti ya upole sana akaniuliza

"mwanangu naomba utuambie ukweli jana usiku uliona nini" . Hii haikuwa kawaida ya Babu kumuona akiwa anaongea kwa upole kiasi kile. Licha ya kwamba alikuwa ni mtu mwenye upendo na watoto, wajukuu na ndugu wengine lakini Babu pia alikuwa ni mtata sana. Jambo la kukaripia na kuchapa viboko ilikuwa kama mlevi kugugumia chupa ya konyagi, hakujiuliza mara mbili. Alikuwa ni mkali asiyependa masihara hata kidogo, mpaka alikuwa amebatizwa jina akawa anaitwa "serikali" kwa lafudhi ya kisukuma "serekale". Hivyo aliponiuliza hivyo nilijua hilo ni ombi kwa mara ya kwanza tu, lakini nisipotoa majibu anayoyataka kinachofuata ni mkong'oto. Nilijiandaa kujibu lile swali aliloniuliza lakini moyo uliogopa sana mapigo ya moyo yakawa yanaenda kwa kasi.

Hali hii ilinishangaza kidogo kwani ni mara ya pili sasa kila nikitaka kuongelea hilo jambo, nakuwa naogopa sana. Nilitamani kujibu lakini uoga ulinizidi nikabaki kutoa macho na kujiumauma mdomo.

"Mr the dragon hebu nijibu mwanangu kuna kitu chochote uliona jana" aliuliza tena babu.

Nilitaka kukubali lakini bado nafsi yangu iliogopa na kugoma kabisa, hadi nikaanza kutetemeka kwa hofu. Nilishindwa hata kukubali angalau kwa kutikisa kichwa. Mganga yule alinikodolea macho kama ananichunguza kwa makini, halafu akasema.

"Mzee Manumbu nafikiri wewe mwenyewe umeona, nilikwambia huyu hawezi akasema lolote hata umwekee bunduki, si unaona anavyotetemeka, Kuna kitu amefanyiwa huyu" aliniangalia kidogo kisha akaendelea

"Nafikiri cha msingi tuharakishe twende nae kwangu, tukalifanyie utaratibu hili jambo kabla mambo hayajawa mabaya".

Baada ya pale niliamriwa niondoke pale niende nikamuite mama yangu. Niliondoka nikaenda hadi kwenye nyumba nyingine yenye jiko ambapo pembeni yake kuna mti wa "mhare" na ndio sehemu wanawake walipendelea kukaa. Nilimkuta mama amekaa nikampa maelekezo kwamba anaitwa kisha nikaondoka zangu kwenda kucheza. Kuna muda nilikuwa napata wasiwasi lakini kuna muda pia niliona kawaida tu. Nadhani ni kwa sababu ya akili zile za kitoto. Mpira tulikuwa tunacheza barabarani umbali kama wa mita miamoja na hamsini kutoka nyumbani. Baadae nilikuja kuitwa niende nyumbani mama ananiita.

Nilikimbia kwenda nyumbani kumsikiliza mama. Nilikuwa nimeshapata hisia ananiita juu ya suala hilohilo. Nilipofika swali la kwanza kuulizwa lilikuwa

"eti mwanangu jana usiku kuna kitu uliona" . Nilitaka kujibu lakini nilipatwa na hofu nikaishia tu kujibu "sijaona chochote mama". Mama aliniangalia kwa huruma kisha akasema

"Eti babu yako analazimisha uende kwa mganga ukaangaliwe" sikujibu chochote nilikaa kimya tu. Kiukweli nafsi ilikuwa inaniuma sana kwa kumficha ukweli mama yangu. Lakini ningefanya nini wakati kila nikitaka kuongea moyo unaingiwa baridi kama la Antarctica. Najua mtu mwingine anaweza ajiulize hofu tu ndio ilifanya ushindwe kuongea, mimi mhusika ndio najua jinsi nilivyokuwa najisikia.

"Hebu twende huku" aliniambia mama huku akinivuta kuelekea kwenye nyumba kubwa. Tulienda moja kwa moja hadi ndani ya chumba alichokuwa analala mama yangu. Tulipofika mama akaniambia

"Hata nisipokuwepo, babu yako akikwambia muende kwa mganga ukatae kabisa, jifunze kumtegemea Mungu kwenye maisha yako"

Nilishangazwa kidogo na kauli ile ya mama, maana kwa jinsi babu alivyokuwa mtata sidhani kama ningeweza kumgomea endapo angeamua jambo lake. Nilijua hata mimi hajanichukua kwa lazima kwenda kwa mganga kwa sababu ya babu alimpenda sana mama yangu hivyo hakutaka kulazimisha. Mama yangu alikuwa ni kipenzi cha babu yangu inawezekana kuliko watoto wote wa huyo mzee. Hili jambo hata watoto wengine walikuwa wanalijua. Inawezekana kwa sababu mama yangu alikuwa ni kitindamimba wa mke wake wa kwanza kuoa, ambaye alifariki akamwacha mama yangu bado ananyonya.

Lakini kuhusu suala la kumtegemea Mungu sikushangazwa sana na hilo, pamoja na akili yangu ya kitoto lakini nilitegemea hilo kutoka kwa mama yangu. Kwa sababu mama yangu alikuwa ni mtu wa dini msabato aliyeishika imani haswa. Sio wale wasabato wa kusubili jumamosi ndio wavae suruali nyeusi, shati jeupe na tai nyeusi huku wakikung'uta biblia iliyojaa vumbi ndio waende kanisani. Yeye kusali na kusoma neno ilikuwa ni jadi yake. Baada ya hapo aliniambia nifumbe macho akapiga ombi moja refu la uchungu sana lililoishia na sala ya bwana. Kisha akasema kauli moja tu

"MUNGU ATATENDA"

Itaendelea kesho mida kama hii

NB: huu ulikuwa ni utangulizi tu kesho ndio tutalianza sakata lenyewe. Kuanzia nilivyolazimishwa kuwa kwenye mahusiano na mchawi hadi alivyoniroga.

Usiku mwema.
 
..
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…