comrade igwe
JF-Expert Member
- Jan 12, 2015
- 7,295
- 3,945
Dar es Salaam.
Amri ya Rais John Magufuli ya kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi umeitingisha kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Acacia inayomiliki migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu.
Kila mwaka migodi hiyo husafirisha wastani wa tani 55,000 za mchanga huo unaojumuisha madini ya dhahabu, shaba, chuma, salfa na mekyuri na Rais ameagiza uchenjuaji wa mchanga wa madini ufanyike nchini.
Hii ni mara ya pili Rais Magufuli kutoa zuio hilo. Agosti mwaka jana akiwa Kahama alisema katika uongozi wake, hataki kuona usafirishaji wa mchanga huo. Machi 2 alitoa tena zuio hilo alipotembelea kiwanda cha Vigae cha GoodWill cha Mkuranga, Pwani, kinachotumia teknolojia ya kuchambua baadhi ya madini kwa ajili ya utengenezaji wa vigae.
“Watanzania tumekuwa tunaibiwa kwenye dhahabu, wanachukua mchanga wanausafirisha nje ya nchi, wakifika huko wanachambua dhahabu na mchanga unabaki hukohuko. Ule ni wizi, sasa naagiza hakuna kusafirisha tena mchanga nje ya nchi... tutajenga kiwanda hapahapa,” alisema.
Baada ya zuio hilo, taarifa ya Acacia iliyokuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii ambayo ilithibitishwa na Makamu wa Rais wa kampuni hiyo Tanzania, Deo Mwanyika inaeleza kuwa Ijumaa wiki hii hisa za kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa London, Uingereza zilishuka kwa wastani wa asilimia 20. Hadi jana jioni hisa hizo zilipanda tena kwa asilimia 10.
Mwanyika alisema wamepokea barua ya zuio hilo na kusema Acacia itafanya majadiliano zaidi na Serikali ili kufahamu zaidi juu ya utekelezaji wa agizo hilo.
“Inabidi kufanyike majadiliano, Acacia haikatai kuchenjua mchanga huo hapa ndani lakini siyo suala la kesho, itachukua muda kwa hiyo mchanga unaozalishwa sasa hivi ambao ni sehemu ya shughuli za uchimbaji itakuwaje! Je, utasitisha, utasimamisha mgodi?,” alihoji.
Hata hivyo, utafiti juu ya uwezekano wa Tanzania kuwekeza mtambo wa kuchenjua mchanga huo, uliofanywa na Wakala wa Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA) Februari, 2011 unaonyesha kuwa gharama za kusimika mtambo wenye uwezo wa kuchenjua wastani wa tani 150,000 kwa mwaka ni kati ya dola 500 milioni hadi 800 milioni.
Waziri Muhongo alinukuliwa na gazeti la The Citizen akiagiza kampuni zote kuanza uchenjuaji wa mchanga huo hapa nchini.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Madini na Nishati Tanzania (TCEM), Gerald Mtuli alisema nia ya Rais ni njema lakini inahitaji kampuni hizo kupewa muda.
Pia alisema kuwekeza mtambo huo ni hasara kwa mwekezaji kwa sababu kinachozalishwa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya mchanga unaotakiwa kuchenjuliwa.
“Mwekezaji hawezi kukubali hasara, ni sawa na unalima ekari moja ya nyanya halafu unataka mwekezaji, gharama za uendeshaji wa mtambo ni kubwa kuliko kile tunachozalisha, haina masilahi kwa hapa nchini,” alisema.
Pili, alisema endapo zuio hilo litaendelea, mgodi wa Buzwagi itabidi ufungwe kutokana na asili ya uzalishaji wake.
“Tani moja ya udongo unaochimbwa Buzwagi unatoa gramu mbili tu za dhahabu, maana yake uchafu ni mwingi hivyo ni lazima kusafirisha, Bulyanhulu itabidi kupunguza wafanyakazi ili kuepuka gharama,” alisema.
Aidha, Mtulia alisema upembuzi yakinifu ulifanyika mwanzoni wakati wa uwekezaji wa migodi hiyo na matokeo yalionyesha itahitaji kusafirisha mchanga huo kwa asilimia 30 hadi 40 nje ya nchi.
Pamoja na kuunga mkono zuio hilo la Rais Magufuli, Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti kutoka Taasisi ya Repoa, Dk Abel Kinyondo alisema, linaweza kujenga hofu kwa wawekezaji wengine.
Alisema kabla ya zuio hilo, kulihitajika majadiliano ya kina kati ya Serikali na wawekezaji hao.
“Rais ameibua mjadala mzuri na ametuma ujumbe wa hofu iliyopo kutonufaika na madini, kampuni zimebakiza muda mchache na mikataba iliyoingia inatia shaka, lakini zuio hili ni mara ya pili je, mara ya kwanza ilikuwaje wakaruhusu kuendelea na usafirishaji? Ili kuepuka hatari ya kupoteza wawekezaji wengine na kulinda Serikali ipate kilicho sahihi, ni lazima kukaa pamoja,” alisema.
Gazeti la The Citizen