Kampuni ya Madini 'Meek Maine Co.LTD' kufutiwa leseni

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,879
6,356
Serikali imemuagiza Afisa Madini Kanda ya Kati kuifutia leseni kampuni ya madini ya Meek Maine CO.LTD ya jijini Dar-es-Salaam kwa kushindwa kuanza uchimbaji katika vitalu vitatu kwenye machimbo ya dhahabu ya Sekenke wilayani Iramba kwa zaidi ya miaka sita, na kusababisha wachimbaji wadogo kushindwa kujipatia kipato kutokana na wao kushindwa kufanya kazi katika maeneo hayo.

Naibu waziri wa Nishati na Madini Daktari Medardi Kalemani amesema hayo katika kijiji cha mgongo wilayani Iramba kufuatia kampuni inayojulikana ya Meek Maine CO LTD kushindwa kuchimba madini ya dhahabu licha ya kupewa leseni hiyo miaka mingi.

Katika hatua nyingine naibu waziri amesema kampuni hiyo pamoja na kupata msamaha wa zaidi ya shilingi milioni ishirini na sita wa kuingiza vifaa nchini vya uchimbaji lakini havijafanya kazi, jambo ambalo ni uharibifu wa fedha za Serikali kwa sababu zingeweza kufanya kazi zingine.

Awali mkurugenzi wa kampuni ya Meek Maine ambayo imepewa kibali cha uchimbaji wa madini Bwana Ibrahim Mtulo pamoja na kukiri kuwa bado hawajaanza uchimbaji licha ya kuwa na leseni, amemwambia naibu waziri kuwa wao wanajipanga na wataanza uzalishaji ndani ya miezi sita ijayo.

Kwa upande wao wachimbaji wadogo ambao wameonekana kuwa na furaha baada ya naibu waziri kufika eneo ambalo mwekezeji hajalifanyia kazi, wamesema licha wao sasa kusingiziwa kuwa wamelipwa fidia katika mgodi huo, lakini wamefanya juhudi za kupata haki yao mpaka walipoamua kwenda Dodoma kuonana na naibu waziri.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…