Chukulia mfano, ni Jumapili wewe na familia yako mpo kanisani, mara mchungaji wenu mnayempenda na kumuamini anaanza kuwahubiria kwamba maisha ya hapa duniani hayafai kabisa kwa sababu dhambi zimetawala hivyo ni lazima waumini wote mfe ili mkayarithi maisha ya peponi.
Anawaita wasaidizi wake na kuanza kugawa sumu kwa kila muumini kanisani, anawaamuru wote mnywe kwa wakati mmoja na anawahakikishia kwamba muda mfupi baadaye, mtafufuka na kujikuta mpo peponi na kuachana na shida zote za dunia hii, utakubali utakataa?
Basi kwa taarifa yako, tukio kama hilo limewahi kutokea Jonestown, Guyana. Mchungaji aitwaye James Warren Jones almaarufu Jim Jones aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la Peoples Temple (Ngome ya Watu), alisababisha waumini 918 wa kanisa lake kunywa sumu kwa wakati mmoja na kupoteza maisha.
Ilikuwaje? Novemba 18, 1978, Jones aliwakusanya waumini wake kanisani na kuanza kuhubiri. Katika mahubiri yake, alikuwa akiwasisitiza waumini wake kuyakataa maisha ya duniani kwa sababu yalijaa mateso, huzuni, majonzi na kila aina ya dhambi.
Akawaambia Mungu amewaandalia maisha ya furaha baada ya kufa na kueleza kwamba ameoteshwa na Mungu kuwapa kinywaji (sumu) ambacho kitawafanya wavuke kwenye maisha ya duniani na kwenda peponi. Akawajenga kisaikolojia kiasi kwamba hakukuwa na aliyeogopa tena kufa.
Sumu ikagawiwa kwa watu wote waliokuwepo kanisani, wakiwemo watoto zaidi ya 200, saba kati yao wakiwa ni wanaye wa kuwazaa, na yeye akachukua yake kisha akasali na kuwataka watu wote wanywe. Dakika chache baadaye, kanisa lilikuwa limetapakaa maiti kila kona.
Tukio kama hilo limewahi pia kutokea nchini Uganda ambapo mchungaji Joseph Kibweteere, alisababisha wafuasi wake 778 wafe katika tukio lililokuwa linashabihiana sana na la Jones.
Imeandaliwa na Hash-Power kwa msaada wa mitandao.