WAKATI utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ukijinisabu kwamba, umejipanga kupunguza makali ya maisha kwa wananchi, kwa Jiji la Tanga mambo hayapo hivyo, anaandika Regina Mkonde.
Halmashauri ya Jiji hilo imepeleka ujumbe kwa walimu wote jijini humo kuchangia pesa kwa ajili ya kugharamia mbio za Mwenge. Mwisho wa kupokea michango hiyo ni tarehe 25 Aprili mwaka huu.
Ujumbe wa barua hiyo umeandikwa na Gwakisa Lusajo kwa niaba ya Dk. Wedson Sichalwe, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga.
Barua hiyo imeelekeza kwamba, kila mwalimu anayefanya kazi kwenye jiji hilo anapaswa kuchangia Sh. 1,000 ambapo walimu wakuu kila mmoja ametakiwa kutoa Sh. 10,000.
Pia imeelekeza kuwa, pesa hizo zipelekwe kwa Rehema Said, Mratibu wa Mwenge wa Wilaya ya Tanga.
MwanaHALISI Online umemtafuta Sichalwe ili kujua uhalali wa walimu kuchangishwa fedha kwa ajili ya mbio za Mwenge jijini humo.
Sichalwe amekiri kutambua barua hiyo ya kuhitaji michango kutoka kwa walimu na kudai kwamba, ni jambo la hiyari.
“Lazima watu wajue kuwa, barua iliyotolewa haikuwa na lengo la kushinikiza watu watoe michango hiyo. Ni hiyari ya mtu, na ndiyo maana tulitoa kwa wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafisi na kampuni,” amedai Sichalwe.
Anasema, muhusika atakayepokea michango atatakiwa kutoa stakabadhi ili kuwahakikishia wachangiaji kwamba, fedha zao hazitatumiwa kinyume na makubaliano.
“Vile vile, haimaanishi kwamba ni michango ya fedha tu ndiyo inapokelewa, bali hata mwenye vifaa ambavyo vitasaidia kufanikisha shughuli yetu tunavipokea, kwa mfano mafuta ya gari na vyakula,” anasema.
Hata hivyo, Sichalwe ameshindwa kutoa ufafanuzi kuwa, kama ni mchango wa hiyari kwanini alipanga viwango vya kutoa kwamba, walimu wakuu watoe Sh. 10,000 na walimu wa kawaida watoe Sh. 1,000.
Amedai, michango hiyo ni kwa ajili ya ununuzi wa mahitaji ya wageni siku ya tukio ikiwemo chakula na mafuta ya gari kwa ajili ya usafiri.
Ametaja tarehe ya siku ambayo Mwenge utapokelewa jiji humo kuwa ni tarehe 4 Mei 2016 katika Uwanja vya Tunda Ua vilivyopo kwenye Kata ya Kilale na kwamba, tarehe 5 Mwenge utapelekwa visiwani Unguja.