JANUARY MAKAMBA AWE KIPIMO CHA MAWAZIRI WA RAIS SAMIA
OKTOBA 12, 2022, nilihudhuria mkutano wa Waziri wa Nishati, January Makamba na waandishi wa habari. Mada ni “Clean Cooking” – “Upishi Nadhifu". Ulifanyika Ukumbi wa Museum, Benki Kuu, Dar es Salaam.
Nilipokuwa nikimsikiliza January, akielezea mipango na mikakati ya kuwaokoa wanawake wa Kitanzania na upishi hatari kiafya, nikawa napokea kama hadithi ya kisiasa. Mapishi ya kuni na mkaa si ndio yamelilea Taifa la Tanzania?
January alipomkaribisha Daktari wa Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Pauline Chale, akanifanya nibaini kuwa suala la “Upishi Nadhifu" sio la kisiasa. Ni mtambuka. Linagusa Wizara ya Afya, Mazingira, Tamisemi, Madini, Elimu na Nishati yenyewe. Linaihusu Ofisi ya Rais moja kwa moja.
Ni suala linalomhusu mama anayehangaika kila siku kuandaa mlo wa nyumbani kwa kutumia kuni na mkaa. Wajasiriamali wa chakula ni wadau wakubwa. Wauzaji wa mkaa na kuni hili ni lao. Kila Mtanzania anakula chakula kilichopikwa. Upishi Nadhifu ni suala mtambuka!
Dk Chale yupo kitengo cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalum (ICU), Muhimbili. Alitoa ushuhuda wa idadi ya wagonjwa wanaofika Muhimbili na kukaa ICU kwa muda mrefu kwa sababu ya athari za matumizi ya nishati zenye kutoa moshi wakati wa kupika.
Alizungumzia gharama ambazo hakuna Mtanzania wa kawaida anaweza kumudu. Sh400,000 kila siku kulala ICU. Shida inaongezeka kwa sababu wagonjwa wengi wanaofika Muhimbili kutibiwa kutokana na athari za moshi, ni lazima wasaidiwe kupumua kwa mashine za oksijeni.
Wingi wa wagonjwa ambao Dk Chale aliueleza, ulinifanya nipate hofu kubwa. Watanzania wengi, hasa wanawake wanapata matatizo ya mapafu na kifua. Mwisho wanakufa baada ya mateso makali ya maradhi.
Kwa mujibu wa Dk Chale, Watanzania kati ya 33,000 mpaka 45,000 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati zisizo salama kupikia. Hiyo ni idadi ndogo kama utalinganisha na ripoti ya Nigeria. Nchi ambayo kimazingira inafanana kabisa na Tanzania. Kuanzia mapishi mpaka ulaji.
Waziri wa Mazingira wa Nigeria, Sharon Ikeazor, alieleza mwaka jana (2021), kuwa idadi ya wanawake na watoto 90,000 wanapoteza maisha kila mwaka kwa sababu ya athari za matumizi ya kuni kama nishati ya kupikia.
Daktari wa Hospitali wa Hospitali Kuu ya Abuja, Abdulshahid Sarki, alifafanua kwamba matumizi ya muda mrefu ya kuni husababisha magonjwa ya kifua, kichwa, mapafu, saratani na changamoto za uzazi kwa wanawake.
TUREJEE TANZANIA
Kwa mujibu wa January, takwimu za Wizara ya Nishati zinaeleza kuwa asilimia 89.7 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kama nishati ya kupikia. Kuni ni namba moja, zikiwa na asilimia 63.5, mkaa ukifuatia kwa asilimia 26.2. Upishi kwa gesi ni asilimia 5.1, wakati umeme ni asilimia tatu.
Kukamilisha asilimia 100, Watanzania asilimia 2.2 hutumia nishati za kupikia zenye kufanana na gesi pamoja na umeme. Kwa mantiki hiyo, Watanzania asilimia 10.3, ndio wapo kwenye kundi salama. Kwa kuchukua taarifa kuwa idadi ya Watanzania ni 60 milioni, maana yake 6.1 milioni ndio salama. 53.9 wapo hatarini.
Ripoti ya Nigeria inaonesha kuwa waathirika wakubwa ni wanawake na watoto. Naam, akina mama ndio wanaopika nyumbani, watoto wanakuwa pembeni ya mama zao, wanapokea moshi kwa wingi. Hatari kwa wanaume ni kidogo, ingawa ipo.
Ukishabaini hatari ilivyo kubwa ya mapishi kwa kutumia nishati zenye moshi, unapata jawabu kwamba si suala la Wizara ya Nishati peke yake, Wizara ya Afya ina mzigo mkubwa mno. Yenyewe ndio inapokea moja kwa moja matokeo. Mwisho kabisa, wagonjwa kimbilio lao ni hospitali.
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, suala la Upishi Nadhifu ni lake. Tamisemi hali kadhalika, maana ndio wizara inayoingia ndani kabisa kwenye maisha ya wananchi. Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Tamisemi pamoja na Mazingira, inapaswa kuhakikisha Watanzania wanaelimika kuhusu nishati safi za kupikia.
Wizara ya Madini haipaswi kuwa nyuma. Makaa ya mawe ni nishati safi ya kupikia. Ndio sababu nilitangulia kueleza kwamba suala la nishati za kupikia ni mtambuka. Linaweza kuzigusa wizara nyingi kwa pamoja.
UJUMBE NINAOUKUSUDIA
Ripoti za dunia zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kiwango cha chini kabisa cha mapishi kwa kutumia nishati safi. Inaonesha kuwa Tanzania ina asilimia chini ya tano ya matumizi ya nishati nadhifu za kupikia.
January alisema kuwa anataka Tanzania ipige hatua hadi kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi za kupikia ndani ya miaka 10 ijayo. Kwamba endapo nchi itafikia hapo, ataweza kusema taifa limefanikiwa.
Kuelekea kufanikisha malengo ya kuwezesha nchi kupiga hatua kwenye matumizi ya nishati safi za kupikia, Novemba Mosi na Pili, mwaka huu (2022), Wizara ya Nishati imeandaa kongamano la kitaifa, kujadili mbinu anuwai za kuwezesha kumfikia hadi mwanamke wa kijijini ili aelimike, aache kuni na kuzielekea nishati salama.
Kwa mujibu wa January, kongamano hilo litahusisha wadau mbalimbali. Wataalamu kwa wabunifu, wafanyabiashara na mamlaka ili kutafuta mwarobaini wa kumsaidia Mtanzania aache nishati zisizo salama kwa kupikia na kuzielekea zilizo nadhifu, nafuu na bora kiafya.
Mikakati hiyo ya January, inakumbusha hatua ambazo alishaanza kuzipiga. Julai mwaka huu, January alianza kampeni ya kugawa mitungi midogo ya gesi vijijini ili kuwezesha urahisi wa kupikia kwa kutumia nishati hiyo salama.
Hapa ndipo nilipokusudua kupazungumzia; kubeba agenda na kutembea nayo. Mawaziri wengi wapo ofisini, anahudumiwa vizuri na nchi, lakini ukimuuliza ni agenda gani kwa wananchi ambayo ameibeba kwa kipindi chake cha uongozi, anaweza asikupe jibu.
Suala la nishati nadhifu angalau linaweza kumpambanua January kuwa ni agenda ambayo ameibeba. Anatembea nayo. Anakwenda vijijini kufundisha ubora na unafuu wa gesi. Anarahisha pia upatikanaji.
Kuna watu wanapata tabu na kutumia gharama kubwa katika mapishi yao kwa sababu hawana elimu mahsusi kuhusu unafuu wa gesi. Wapo wanatambua lakini wanaogopa kwa sababu hawawezi kumudu bei za mitungi na majiko. Mwanakijiji akishapata jiko na mtungi, maisha yanakuwa mepesi.
Wapo watu wanatumia mkaa kwa kuamini ni nafuu kwa sababu hawajawahi kutumia gesi na kujua unafuu wake. Kumbe sasa, kinachotakiwa ni elimu. Wananchi wakishaelimishwa, watapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati zisizo salama kiafya katika mapishi yao.
Kama agenda ya Upishi Nadhifu itafanikiwa, afya za wanawake vijijini zitalindwa. Wastani wao wa umri wa kuishi utaongezeka. Urembo wa asili wa dada zetu wa vijijini utadhihirika. Mama zetu wanaoteswa na moshi mpaka macho yanakuwa mekundu, watapata nusura. Na hawataitwa wachawi.
Hivi sasa wanawake wengi vijijini wanaonekana wamezeeka kabla ya umri wao. Mikunjo kwa sababu kupuliza moto wa kuni na wakati mwingine zinakuwa mbichi, hivyo kufanya wakati wa kupika uwe muda wa mateso kwa mama na dada zetu. Ni chanzo cha warembo wengi kupoteza urembo wao wa asili.
Hekaheka za shughuli za utafutaji riziki, hasa kilimo cha jembe la mkono, mateso ya kuchota maji umbali mrefu, halafu wanateswa pia wanapoingia jikoni kuandaa mlo. Mtindo wa maisha ndio sababu ya wanawake wengi vijijini wanachoka na kuonekana wazee kabla ya umri wao.
UONGOZI WA HUDUMA
Nikakumbuka uchambuzi wa wanazuoni, Richard Batley na Daniel Harris wa Chuo Kikuu cha Birmingham, UK, wenye kichwa “Analysing the politics of public services: a service characteristics approach.” – “Kuchambua siasa za huduma kwa umma: mbinu ya sifa za huduma.”
Ndani ya kitabu hicho, wanazuoni hao wanaeleza kuwa siasa za kuhudumia umma lazima ziwe na majibu ya changamoto za kimaisha za watu. Sharti pia, wanasiasa wenye mamlaka, watumie kipindi chao cha uongozi kubadili maisha ya wananchi.
Nikaivuta pia akilini nadharia ya “Community Politics” – “Siasa za Jumuiya", iliyozaliwa UK mwanzoni mwa miaka ya 1980. Msingi ukiwa, siasa ni kwenda kuhudumia jumuiya hata kwa kipimo kidogo.
Kitendo cha January kuingia mpaka vijijini kugawa mitungi ya gesi na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi za kupikia, ndio siasa za jumuiya, vilevile siasa za huduma kwa umma.
Anachokifanya January kuhusu nishati, iwe polepole au kwa kasi, mwisho kabisa kinakwenda kumjenga Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya wananchi wa kawaida. Hakuna mwananchi mwenye shukurani kama yule ambaye anashuhudia maisha yake yakibadilishwa kwa ubora.
Rais Samia anapaswa kumtumia January na mawaziri wengine wanaobeba agenda kama mfano, ili kila mmoja kwenye Baraza la Mawaziri awe na agenda ya moja kwa moja kwa wananchi na maisha yao.
Taifa haliwezi kupiga hatua kwa mawaziri kutokuwa na agenda. Wanaingia wizarani na kuendeleza mtindo uleule, hakuna ubunifu wala kiu ya kumaliza jambo. Hawalali na kuamka wakiwaza kuacha alama, wao wanataka waenende kimazoea. Halafu mishahara mikubwa, wanapewa magari ya kifahari. Utumishi hauna tija.
Ndimi Luqman MALOTO