Wakati tukiendelea kuisubiri kwa hamu mechi ya Fainali ya Michuano ya UEFA Champions League kati ya Real Madrid dhidi ya Juventus ni wazi wapo baadhi ya wachezaji na wakufunzi ambapo kila mmoja kwa nafasi yake fainali hii ina umuhimu mkubwa sana kwake kutokana na uhalisia wa maisha yake ya soka kwa sasa. Wapo wengi ila nitazungumzia watu watano peke yake ambao kwangu mimi naona fainali hii ni muhimu sana kwao . Kwa upande wa Real Madrid kuna watu ambao fainali hii ni muhimu sana kwao lakini hali kadhalika kwa upande wa Juventus na kwenyewe kuna watu ambao fainali hii ni muhimu sana kwao. Kwa hivyo kipute cha leo hata hakielezeki jinsi kitakavyokuwa kikali na cha kuvutia sana.
Christiano Ronaldo:
Fainali hii ni ya muhimu sana kwake kuliko hata mtu mwingine akifanikiwa kuchukua Ubingwa huu wa UEFA 2016/17 itamuweka katika mazingira mazuri ya kubeba Ballon D'Or mara ya tano kama mchezaji mwenzake raia wa Argentina Lionel Messi anaekipiga Barcelona.
Gianluig Buffon:
Huyu jamaa akifanikiwa kuchukua ubingwa huu wa UEFA utamfanya atundike dalugha lake kwa heshima kubwa sana kwanza kwenye Taifa lake pamoja na Klabu yake ya Juventus ambayo amedumu nayo kwa muda mrefu.
Garreth Bale:
Pengine labda ulikuwa hujui hili jambo. Bale akifanikiwa kutwaa taji hili la UEFA itakuwa imemuongezea heshima kubwa sana katika nchi yake ya Wales, Ikumbukwe ndie mchezaji wa kwanza mwenye jina kubwa kwenye soka anaeiwakilisha Wales. Kwa hivyo anaiangalia kwa macho yote mawili fainali hii.
Zinedine Zidane "Zizzou":
Kocha huyu ambae alipokabidhiwa nafasi hii mashabiki, Wadau na wachambuzi mbali mbali walipata wakati mgumu kutambua kama Zidane angemudu kufanya ambayo ameshayafanya ndani ya Real Madrid mpaka leo amefika Fainali ya Michuano ya UEFA Champions League, Kwa hivyo akishinda mechi hii itamuongezea zaidi heshima kwanza kwa Boss wa Real Madrid, Wachezaji, Mashabiki pamoja na Wadau wa soka ulimwenguni. Mechi hii ni ya muhimu sana kwake pia.
Daniel Alves:
Wakati anaondoka Barcelona ni dhahiri kabisa alikuwa na kila kitu kinachotafutwa na mcheza soka yoyote katika soka lake, alishatwaa mataji mengi akiwa Barcelona lakini aliamua kubadilisha mazingira na kutua katika ardhi ya Italia katika klabu ya Juventus, Sasa anahitaji kuendelea kuudhihirishia ulimwengu kuwa bado ana uwezo wa kuyatwaa mataji hata akiwa nje ya Barcelona.
Wajuzi wa mambo wanasema "Tusiandikie Mate na Wino ungalipo" tusubiri kipenga cha mwisho kitakachoamua ni nani mbabe kati ya Juventus ama Real Madrid. Ambao katika michezo 10 waliyokutana Juventus wameshinda 5 Real Madrid wameshinda 3 na kutoa sare 2.
Mtoto hatumwi dukani.
Na: Jalilu Zaid