Rais Shein aongeza mshahara asilimia 100 RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ameahidi kuongeza kiwango cha mishahara wa kima cha chini kwa wafanyakazi wa sekta za umma visiwani humo, kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 300,000 sawa na ongezeko la asilimia 100.
Dk. Shein alisema hayo kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika mjini hapa jana. Alisema ongezeko hilo la mshahara litaanza kutolewa baada ya Baraza la Wawakilishi kupitisha bajeti ya serikali ya Zanzibar ya mwaka ujao wa fedha wa 2016/17, ambayo inatarajiwa kuwasilishwa Mei 18, mwaka huu.
"Niliahidi kutekeleza ahadi hii ya kuongeza kiwango cha mishahara kwa kima cha chini kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 300,000 endapo nitapata ridhaa ya kuongoza tena nchi katika kipindi changu cha pili. Nina waahidi kuwa nitaitekeleza katika mwaka wa fedha ujao wa 2016/17,"alisema Dk.
Shein huku akishangiliwa na wafanyakazi waliohudhuria maadhimisho hayo. Alisema ataendelea kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kama alivyoahidi wakati wa mkutano wake wa kwanza wa ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana uliofanyika kisiwani Pemba.
"Wapo waliobeza kauli yangu hiyo katika kuimarisha maslahi ya wafanyakazi, wapo waliokuwa wakiguna. Kila mmoja alisema lake na wapo walioamini kauli yangu hiyo wakiwemo ZATU (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar), lakini pia wapo waliyodhania nafanya mchezo wa kuigiza,"alisema na kuongeza:
"Nilikuwa msanii na mwigizaji nilipokuwa shule ya msingi na sekondari miaka ya 60 iliyopita, lakini sasa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, hivyo nina jukumu la kujenga nchi na kuwatumikia wananchi na wala siwezi kutoa kauli sizizotekelezeka na kufanya utani katika maslahi ya watu."
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali imemaliza kulifanyia kazi suala hilo la ongezeko la mishahara na taarifa rasmi za utekelezaji zitatolewa muda mfupi ujao.
"Leo sitaki kusema itakuwa lini lakini niseme subira yavuta heri. Endeleeni kuvuta subira si muda mrefu ujao mtayasikia yanatangazwa hadharani tena mchana kweupe. Sh. 300,000 kwa kima cha chini cha mishahara inawezekana. Tumefanya mengi sana ya zaidi ya Sh. 300,000, kwa hivyo hizo hazitushindi katika serikali hii kuwalipa wafanyakazi," alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Shein alisema atalipa mafao ya wastaafu kwa wakati na malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi hasa walimu kwa kuwa bado wanadai haki zao na bado hawajalipwa na kwasasa unaandaliwa utaratibu wa kuwalipa. Aliwataka wafanyakazi nao kutekeleza wajibu wao wa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu na na maarifa na wale wanaotegea kazi, wanaotoroka kazini na wanaosafiri bila taarifa kuacha tabia hiyo mara moja.
Source: Nipashe