Taarifa ndani ya dayosisi hiyo zinasema, katibu mkuu wa DMP, Godfrey Nkini, amenukuliwa akimueleza Mchungaji Leita kuwa utendaji wa Askofu Malasusa wa kuhudumu ofisini umezorota tangu kuibuka kwa tuhuma hizo.
Akamtaka kwenda likizo ili kurejesha amani ya kiongozi mkuu wa dayosisi.
Haya yameibuka baada ya jitihada za kutaka wachungaji kutetea Askofu wao kushindikana. Hoja ya kutaka kanisa limfanyie maombi Askofu Malasusa iliwasilishwa kikaoni na msaidizi wa Askofu.
“Baada ya mpango huu kukwama, katibu mkuu wa dayosisi alimwita Mchungaji Leita ofisini mwake na kumtaka achukue likizo ya muda mrefu ili asionekane machoni mwa waumini na wageni wengine.
“Mchungaji Leita alitoa masharti mawili: Kwanza, yuko tayari kuchukua likizo endapo katibu mkuu atampa barua rasmi ikieleza sababu ya hatua hiyo na pili endapo mtuhumiwa mwenzake, Askofu Malasusa, naye atapewa likizo.”
Amesema, “katibu mkuu Nkini ameshindwa kutekeleza masharti hayo, jambo ambalo limesababisha Mchungaji Leita kuendelea kubaki ofisini.”
Haya yanaibuka, siku mbili baada ya Asime Modern Mwakilima,muumini wa dayosisi ya Mashariki na Pwani akisema, anatafakari upya uumini wake katika kanisa hilo.
Alisema, “suala la imani ni langu mwenyewe na Mungu. Lakini katika hili, naona mkuu wetu amepoteza sifa ya kuhudumu.
Badala ya kusimamia ukweli,kanisa limeamua kukandamiza haki.”
Mchungaji mmoja wa kike aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini ameutuhumu uongozi wa dayosisi hiyo kukumbatia alichoita, “mfumo dume.”
Alisema, “hapa kuna mfumo dume. Ndiyo unaotaka kutumika kumuonea huyu mama na kumlinda Askofu aliyetuhumiwa naye. Haya ni makosa makubwa sana.
Hata Bwana Yesu alipoletewa mwanamke aliyefumaniwa akizini, alimwuliza yuko wapi mtuhumiwa mwenzako?”
Taarifa zinasema, mkuu mpya wa KKKT, Askofu Fredrick Shoo amemuita Mchungaji Leita kwa lengo la kujadiliana naye juu ya suala hilo; lakini amegoma hadi mahojiano hayo yamshirikishe Askofu Malasusa.
“Hii inaonyesha mchungaji huyu wa kike alivyonusa mbinu chafu za kutaka kutelekezwa na kanisa ili kumuokoa Askofu Malasusa,” ameeleza mtoa taarifa ndani ya kanisa hilo.
MwanaHALISI Online ilipokea nakala ya waraka wa kichungaji uliosambazwa kwa watu mbalimbali, ukiwataka waumini wa kanisa hilo kuchukua hatua za haraka kuikoa dayosisi yao iliyotumbukia katika mgogoro wa kuongozwa na anayemuita,“kiongozi aliyepungukiwa na uadilifu.”