TAARIFA KWA UMMA
kwa mara ngingine Jeshi la Polisi wilayani Arumeru, limewazuia kutimiza wajibu wao kwa jamii, kuwakamata na kuwaweka chini ya ulinzi waandishi wa habari kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Alexander Mnyeti kuwa waandishi hawapaswi kufanya kazi yoyote katika eneo hilo bila kibali chake.
Waandishi wa habari waliokumbana na kadhia hiyo leo, inayovunja sheria za nchi na kuingilia uhuru wa habari na wanahabari kutimiza wajibu wao ni; Bahati Chume (Mwananchi) na Doreen Aloyce (Redio Sunrise), ambapo walifika Arumeru kufuatilia suala la machimbo ya kokoto wilayani humo.
Mwishoni mwa mwaka jana Mwandishi wa Habari wa ITV, Khalfan Lihundi alikumbana na unyanyasaji huo wilayani Arumeru, alipokuwa akifuatilia habari za tatizo sugu la ardhi katika maeneo hayo.
Tunakemea na kulaani vikali tabia hiyo ya viongozi wa serikali, hususan wateule wa Rais kutumia madaraka yao vibaya, kukiuka sheria za nchi, kutishia usalama wa waandishi wa habari na kuminya uhuru wa habari katika maeneo yao na taifa kwa ujumla.
Tunatoa wito kwa mamlaka na vyombo vinavyohusika kusimamia haki na sheria nchini, kuchukulia tabia hiyo viongozi kutoa amri zinazovunja sheria, kuwa ni dalili mbaya na tishio kubwa kwa jamii, hivyo zichukue hatua zinazostahili haraka kukomesha vitendo hivyo kabla madhara yake hayajazidi kuwa makubwa.
Imetolewa na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA